KASHFA
nzito ya ufisadi wa dola za Marekani milioni 122 (sawa na sh bil. 200)
inayowakabili vigogo sita wa serikali, huenda ikaking’oa madarakani
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama ilivyotokea kwa chama tawala cha KANU cha
nchini Kenya mwaka 2002.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mmiliki wa Kampuni ya PAP inayodai
kuinunua Kampuni ya IPTL yenye mgogoro na Tanesco, Habinder Singh Sethi,
anatajwa kuhusika katika kashfa kubwa ya ufisadi nchini Kenya ya
Goldenberg, uliogharimu takribani dola milioni 600.
Ufisadi huo pia ulihusisha mahakama, watendaji, viongozi na wanasiasa
wakubwa nchini humo, ikiwemo familia ya aliyekuwa Rais wa wakati huo,
Daniel arap Moi.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
(NCCR-Mageuzi), aliwataja vigogo sita wa serikali, wakiwemo mawaziri
kadhaa kuwa wamehusika na ufisadi wa fedha hizo zilizokuwa zimewekwa
katika akaunti ya Baraza la Usuluhishi la Migogoro ya Kibiashara
(Escrow) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Waliotajwa ni Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospiter Muhongo na
Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Beno Ndullu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi
Mramba.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Tanzania Daima Jumatano, kashfa hii ya
pili baada ya ile ya EPA ya sh bilioni 133 katika BoT, huenda ikaiweka
pabaya Serikali ya CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao 2015.
Itakumbukwa kuwa kashfa ya ufisadi kama huu ya Goldenberg ndiyo
ilisababisha kuanguka kwa Chama tawala cha KANU nchini Kenya chini ya
Rais Moi aliyekuwa akimpigania Uhuru Kenyatta kurithi mikoba yake,
lakini akashindwa na Mwai Kibaki.
Bilionea huyo, Sethi, mwenye asili ya Singasinga, ndiye anatajwa
kuvuruga mfumo wa serikali kwa muda mfupi katika sakata hilo la ufisadi
wa BoT.
Akizungumza na gazeti hili, Kafulila alisisitiza kwamba kwa jinsi
hali ilivyo sasa, anathubutu kusema kuwa Sethi ameiweka Serikali ya CCM
mfukoni.
“Ufisadi wa akaunti ya Escrow ni lazima mbivu na mbichi zifahamike.
Siungi mkono uamuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza
kwa kuwa hili jambo linagusa mamlaka kubwa na ya juu sana katika dola.
“Ndiyo maana nilisisitiza kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge ili
kuepuka majibu ya ubabaishaji kama yalivyotolewa na Waziri Mkuu
bungeni,” alisema Kafulila na kutaja sababu tano.
Moja, alisema Waziri Mkuu kusema ameagiza CAG na Takukuru wachunguze,
lakini wakati huo huo anasema fedha za Escrow hazikuwa za Tanesco wala
serikali kabla ya ripoti za uchunguzi, ni sawa na kuingilia uchunguzi
kwani inazifanya mamlaka hizi zikose uhuru na badala yake yeye
angesubiri matokeo ya uchunguzi.
Pili, alisema CAG amewahi kutoa ripoti ya aibu alipopewa jukumu la
kukagua ufisadi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
David Jairo, hivyo hana imani kama atafanya tofauti.
Tatu, Kafulila anasema kuwa Takukuru nayo kwenye ufisadi wa Richmond walitoa ripoti dhaifu na hivyo hajui kama wameshajifunza.
Katika sababu ya nne, anasema kuwa fedha za Escrow zote ni za Tanesco
kwani hukumu ya awali ya ISCID ilieleza gharama za malipo ya umeme kati
ya Tanesco na IPTL ifanyike upya kwani ilikuwa juu kuliko kawaida na
kwa misingi ya ukomoaji, kiasi ambacho tayari Tanesco ilikuwa imetozwa
zaidi na IPTL kuanzia mwaka 2002, ni zaidi ya dola milioni 150, hivyo
hiyo fedha yote iliyokuwa Escrow ingekuwa mali ya Tanesco.
“Tano, hili jambo lote ni mchezo mchafu. Kwa mfano, anadanganya umma
kuwa eti amekuja kuiuzia Tanesco umeme kwa bei ya chini kabisa, na hivyo
lazima Watanzania wajiulize huyu mtu ni wapi amepata rekodi ya biashara
ya kuuza umeme hata ahaidi.
“Pia kama anasema amenunua asilimia 30 za IPTL zilizokuwa chini ya
VIP kwa dola milioni 75, ina maana asilimia zote 100 atakuwa amenunua
kwa zaidi ya dola milioni 200?” alihoji.
Kafulila alifafanua kuwa inawezekanaje mtu aje anunue IPTL yenye
migogoro na madeni ya miaka mingi wakati mitambo yake ni chakavu yenye
zaidi ya miaka 20 ilhali mitambo kama hiyo mipya ingeweza kununuliwa kwa
dola milioni 100?
“Huyu Singasinga wa PAP ukweli hajanunua asilimia 70 ya Mechmar na
ndiyo maana hana ‘share certificate’ ya Mechmar. Na serikali hii
inaingia hasara kubwa sana muda si mrefu kulipa deni la Standard Bank
pamoja na Liquidator wa Mechmar au Mechmar mwenyewe,” alisema.
Kwa mujibu wa Kafulila, uamuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
uliobarikiwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda wa kuzielekeza taasisi za
serikali za Takukuru na CAG kuchunguza ili kujiridhisha kuhusu uchotwaji
wa fedha katika akaunti ya Escrow umeibua shaka.
Akaunti hiyo ilifunguliwa mwaka 2004 kutokana na mgogoro wa
kibiashara kati ya IPTL na Tanesco ambapo Tanesco ilipeleka shauri hilo
kulalamikia gharama kubwa wanazotozwa na IPTL.
Hivi karibuni baraza hilo lilitoa uamuzi wa awali wa kutaka Tanesco
kukaa pamoja na IPTL kupitia upya malipo hayo, lakini Tanesco imekataa
kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa Kafulila, uchunguzi alioufanya na ushahidi alionao,
fedha hizo zimeshachotwa katika akaunti hiyo kwa ushirika wa vigogo hao.
Alisema kuwa fedha hizo zilihifadhiwa katika akaunti hiyo kusubiri
hatma ya mgogoro huo ambao kwa sasa umekuwa mkubwa zaidi baada ya
Kampuni ya PAP kudai imeinunua IPTL.
PAP inadai kuinunua IPTL kutoka kwa Mechmar iliyokuwa ikimiliki asilimia 70 ya hisa na VIP iliyokuwa na umiliki wa asilimia 30.
Kwa mujibu wa Kafulila, ushahidi wa cheti unaonyesha kuwa PAP
imenunua asilimia 30 ya hisa za VIP, lakini haina ushahidi wa ununuzi wa
hisa asilimia 70 za Mechmar.
Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Wawekezaji (ISCID), lilitoa
hukumu ya awali Februari 2014 na kutoa siku 90 kwamba Tanesco ikae na
IPTL wapige upya mahesabu ya bei ya umeme kwani inatoza zaidi.
Kafulila alisisitiza kuwa suala hilo liko wazi kwa vile
limethibitishwa na Gavana Ndullu alipoitwa kwenye Kamati ya Bunge,
alisema kuwa alipewa maelekezo ya kushinikizwa kutoa fedha hizo.