Mkurugenzi
wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraim Kwesigabo
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu
mfumuko wa bei nchini.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imeeleza kuwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi
Aprili umeongezeka ikilinganishwa na mwezi uliopita kutokana na kupanda
kwa bei za bidhaa na huduma mbalimbali.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu
za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa
mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Aprili 2014 umeongezeka na kufikia
asilimia 6.3 kutoka asilimia 6.1 za mwezi uliopita.
Amesema
kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali kwa mwezi Aprili
2014 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na ile iliyokuwepo mwezi Machi
huku kukiwa na ongezeko dogo la upandaji wa bei kwenye baadhi ya bidhaa
na huduma kwa mwezi huu ikilinganishwa na bei za mwezi uliopita.
Ameeleza
kuwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na migahawa kwa mwezi Aprili
umeongezeka hadi asilimia 8.5 kutoka asilimia 7.9 za mwezi Machi mwaka
huu na kuongeza kuwa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi
imeongezeka hadi asilimia 7.8 kutoka asilimia 7.2 za mwezi uliopita huku
badiliko la fahirisi za bidhaa zisizo za vyakula likipungua hadi
asilimia 4.9 kwa mwezi Aprili 2014 kutoka asilimia 7.2 iliyokuwepo mwezi
uliopita.
Kwa
upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi,amefafanua
kuwa kumekuwa na ongezeko dogo la asilimia 0.7 ikilinganishwa na
ongezeko la asilimia 0.6 kwa lililokuwepo mwezi Machi mwaka huu, huku
fahirisi za bei za taifa zikiongezeka hadi kufikia 150.50 kwa mwezi
Aprili 2014 kutoka 149.49 za mwezi Machi.
Amezitaja
bidhaa zilizochangia ongezeko la fahirisi za bei nchini kuwa ni pamoja
na mchele, mahindi,unga wa Muhogo,Kuku wa kienyeji, dagaa,samaki
wakavu, matunda, karanga na mihogo.
Kwa
upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia ongezeko la fahirisi
amesema ni pamoja mkaa wa kupikia, huduma za matibabu, mafuta ya
dizeli,na gharama ya kusaga nafaka.
Kuhusu
uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma kwa
mwezi Aprili Bw. Kwesigabo amesema kuwa umepungua na kufikia shilingi
66 na senti 45.
“Kupungua
kwa thamani ya Shilingi kunamaanisha kwamba, kama mtu alikuwa na uwezo
wa kununua bidhaa kwa Shilingi 100 kwa mwaka jana, kwa kipindi hiki
itampasa aongeze zaidi ili aweze kununua kitu kama kile kile mfano
badala ya shilingi 100 inabidi atumie shilingi 134”
Kuhusu
ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika
Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko
wa bei nchini Kenya umeongezeka na kufikia asilimia 6.41 kwa mwezi
Aprili 2014 kutoka asilimia 6.27 za mwezi Machi , huku Uganda ikiwa
na mfumuko wa asilimia 6.7 kwa mwezi huu ikilinganishwa na 7.1 za mwezi
uliopita.