Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk Hamis
Kigwangala amezitaka Sekretarieti za mikoa na halmashauri zote nchini
kuhakikisha kwamba inawashirikisha wananchi katika maandalizi ya bajeti
kubuni vyanzo vya mapatao.
Akiwasilisha
maoni ya Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
bungeni leo kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2013, mwenyekiti
wa kamati hiyo, Dk Kigwangala amesema pia wananchi washirikishwe katika
utungaji wa sheria ndogo za ukusanyaji ili kurahisisha zoezi la
makusanyo bila manung’uniko.
Amesema
ushiriki wa wananchi pia utasaidia katika zoezi zima la kuchangia
ujenzi wa miradi ya maendeleo hasa pale ambapo Serikali kuu pamoja na
Serikali za Mitaa zitakapokuwa zinatoa mchango wake kikamilifu katika
miradi husika na hivyo nguvu ya wananchi kutopotea.
Dk
Kigwangala ametanabaisha pia kamati yake inazitaka Halmashauri zote
nchini kuacha kuwabughudhi na kuwanyanyasa wananchi wenye kipato cha
chini kabisa kwa kuwalazimisha walipe kodi kubwa kuliko hata mtaji na
thamani ya mali zao wanazouza, hususan wafanya biashara ndogo ndogo.
Ametolea
mfano wa wafanyabiashara anaotembeza bidhaa za mikononi maarufu
wamachinga na mama lishe, ambao mara kadhaa wamekuwa wakinyang’anywa
biashara zao na migambo wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kama wezi ndani
ya nchi yao na migambo hao kinyume kabisa na maadili ya kiafrika
wakizitupa, wakihodhi ama kumwaga chini.
“Vitendo
vya kinyama dhidi ya watu wa aina hii ni vingi na kwa namna yoyote ile
havikubaliki katika Taifa letu na hivyo basi Kamati inaitaka Serikali
itekeleze Sera yake nzuri ya kuwalinda na kuwawezesha wananchi wenye
uchumi wa chini kwa vitendo ili nao wajikwamue na umaskini, wakidhi
mahitaji yao na waendelee kuiheshimu na kuipenda nchi yetu na Serikali
yake,” alisema.
Amesema
Kamati inaziagiza Serikali kutoa maelekezo sahihi kwa Tawala za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuwajengea mazingira mazuri,
wezeshi na ya kisheria wafanyabiashara wote wanaohangaika kutafuta mkate
wao wa kila siku kwa uchuuzi wa bidhaa zinazohesabika kwa macho tu bila
matumizi ya nguvu ili kulinda haki ya wananchi kujifanyia kazi.
Vilevile,
Dk Kigwangala amezitaka Halmashauri zote nchini katika bajeti ya mwaka
huu kutenga asilimia 60 ya makusanyo yake ya ndani kutekeleza miradi ya
maendeleo kwa wananchi.
Dk
Kigwangala alisema Kamati inaendelea kusisitiza kwamba sekretarieti za
mikoa zikiongozwa na wakuu wa mikoa, kuimarisha ufuatiliaji kwa
kuzisimamia halmashauri na kuhakikisha kuwa fedha za miradi ya maendeleo
zitokanazo na makusanyo ya ndani na zinatoka nje zinatumika kuwaletea
wananchi maendeleo.
Kamati
yake pia imependekeza Serikali kuweka mikakati madhubuti ya ukusanyaji
wa mapato ya majengo katika majiji, manispaa, miji na miji midogo, kwani
fedha nyingi zinapotea kwa kutokusanywa kwa kodi hii.
Amezitaka
Halmashauri kutumia mapato yake ya ndani kukamilisha miradi ya ujenzi
wa majengo ya madarasa, majengo ya zahanati na vituo vya afya, nyumba za
walimu, nyumba za wauguzi vijijini, mabarabara ya vijijini, kuchimba
visima.
Dk Kigwangala alisema serikali kutegemea hela za wahisani hakuwezi kusaidia kuwapatia wananchi wake maendeleao.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia