TIMU ya Simba imeonesha jeuri ya fedha na kuuhakikishia umma kuwa haitaki mzaha msimu ujao, baada ya kumwaga kitita cha Sh milioni 42 kumnyakua straika wa Mbeya City, Saady Kipanga.
Habari za kina kutoka kwa rafiki wa nyota huyo zinadai kuwa, Simba imempatia kitita cha Sh milioni 30 ‘keshi’, kama njia ya kumshawishi pamoja na kumuahidi mshahara wa Sh milioni moja kwa mwezi.
Mshahara huo unamfanya Kipanga kukunja kibindoni Sh milioni 12 kwa mwaka, hesabu inayoleta jumla ya Sh milioni 42 ukijumlisha fedha za ushawishi.
Mbali na hiyo, Simba tayari wanahaha kumtafutia nyumba kwani ni moja ya masharti aliyowahi kuwapa viongozi wa Simba kama wanahitaji huduma yake.
Lakini licha ya yote, bado nyota huyo wa zamani wa Rhino Rangers ya Tabora, hajasaini rasmi mkataba, ingawa wamemalizana kila kitu.
“Jamaa ameishamalizana na Simba kwa kila kitu. Amepewa milioni thelathini keshi na wamemwambia atakuwa akilipwa kiasi cha Sh milioni moja kwa mwezi.
“Hata jamaa mwenyewe anasema asingeweza kuacha bahati hiyo. Zaidi ya yote, kwa sasa Simba wanahaha kumtafutia nyumba ya kuishi maana aliwahi kuwambia kuwa lazima ahakikishiwe malazi,” alisema mtoa taarifa wetu.
Simba imekuwa kwenye rada za kumnasa Kipanga tangu kumalizika kwa ligi kuu msimu uliokwisha ambapo alikodiwa hadi ndege kutoka Mbeya kuja Dar kwa ajili ya kuonana na Simba kuzungumzia suala la usajili wake.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia