Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Dar Brew maarufu
zaidi kama Chibuku, imezindua rasmi bia mpya ya asili ijulikanayo kama ‘Chibuku
Super’, ambayo imewekwa katika chupa maalumu ambayo mteja anaweza kuondoka
nayo.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Dar Brew, Kirowi Suma,
alisema wanaingiza bidhaa hiyo mpya sokoni iliyo na ubora wa hali ya juu, huku
ikiwa na uwezo wa kukaa sokoni kwa muda mrefu zaidi.
Suma alisema, kinywaji hicho
kitauzwa kwa sh. 1,200 na ikiwa na ujazo wa lita moja, huku kikiwa hakina
kemikali yoyote, kwani kimetengenezwa kwa kimea halisi, huku mtumiaji akiweza
kutumia bila kukumbwa na mzio wowote ule.
“Leo (jana) ni siku ya furaha
kubwa sana kwetu Dar Brew na kwa watumiaji wote wa bia, kwani tumeweza kinywaji
kipya cha Chibuku Super ambayo inatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika soko
la bia hapa nchini.
“Bia hii imetengenezwa kwa
utaalam wa hali ya juu na kwa kutumia mitambo ya kisasa kabisa, hivyo
kuwahakikishia wanywaji ubora wa hali ya juu,” alisema Suma.
Alisema, bia hiyo
inatengenezwa kwa kutumia malighafi za Tanzania, ikiwemo nafaka ya mtama ulio bora
toka kwenye ardhi yetu, huku akitaka Watanzania kujivunia kilicho chetu na
kukumbuka asili yetu.
“Chibuku Super ina kilevi cha
asilimia 4, kinachokufanya uweze kuitumia kwa muda mrefu ukiwa na marafiki,
lakini pia inakupa lishe nzuri kutokana na virutubisho vinavyopatikana katika
nafaka zinazotumika kutengeneza bia hii.
“Kwa sasa bia hii itaanza
kupatikana katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma, kisha
itaenea nchi nzima.”
Akizungumzia juu ya
usambazaji, Meneja Mauzo wa Dar Brew, Saidi Mremi, alisema Chibuku Super
itaanza kupatikana leo katika baa zote, maduka makubwa na sehemu nyinginezo
zinazouza vileo.
“Tuna imani kubwa wapenzi wa
bia wataipokea bia hii mpya kwa shangwe na furaha kubwa na pia watatumia bia
hii kuonesha kuwa wanajali asili yao.”
Uzinduzi huo uliojawa na
burudani zisizo kifani, ilihudhuriwa na wafanyakazi wa kiwanda hicho kilichopo
Ubungo, wauzaji wa jumla na rejareja na wageni wengi waalikwa.
|