Mjumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Bi. Jessica Mkuchu (kulia) akiongea
kabla ya kuanza kwa mkutano wa Baraza Maalum la Katiba kwa Watu Wenye
Ulemavu mjini Dodoma leo (Alhamisi, Agosti 15, 2013). Wengine ni
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba (katikati) na Mjumbe
mwingine Bw. Ally Saleh.
Baadhi
ya Wajumbe wa Baraza Maalum la Katiba kwa Watu Wenye Ulemavu wakijadili
rasimu ya katiba mjini Dodoma leo (Alhamisi, Agosti 15, 2013).
Mkurugenzi
wa Shirikisho la Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Bw. Novatus Rukwago
akiongea leo (Alhamisi, Agosti 15, 2013) katika mkutano wa Baraza Maalum
la Katiba kwa Watu Wenye Ulemavu linalofanyika mjini Dodoma.
Mkalimani
wa Lugha ya Alama Bw. Kudra Mnisi akiongea na wajumbe wa Baraza Maalum
la Katiba kwa Watu Wenye Ulemavu leo (Alhamisi, Agosti 15, 2013) mjini
Dodoma.
Makamu
Mwenyekiti wa Shirikisho la Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Wakili Amon
Anastaz akiongea katika Baraza Maalum la Katiba kwa Watu Wenye Ulemavu
leo (Alhamisi, Agosti 15, 2013) mjini Dodoma.
Mwenyekiti
wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo (CHAWATA) Bi. Shida Salum
akiongea katika Baraza Maalum la Katiba kwa Watu Wenye Ulemavu leo
(Alhamisi, Agosti 15, 2013) mjini Dodoma.
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akiongea na
Waandishi wa Habari pembezoni mwa mkutano wa Baraza Maalum la Katiba kwa
Watu Wenye Ulemavu leo (Alhamisi, Agosti 15, 2013) mjini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba amewataka watu
wenye ulemavu kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya katiba ili kuiwezesha
Tume yake kujua mahitaji yao na kuyafanyia kazi.
Akizungumza
katika siku ya kwanza ya mkutano wa Baraza Maalum la Katiba kwa ajili
ya watu wenye ulemavu mjini Dodoma leo (Alhamisi, Agosti 15, 2013), Jaji
Warioba amesema Tume yake inatarajia kupata maoni mazuri yanayohusu
watu wenye ulemavu kutoka katika baraza hilo.
“Mtusaidie
kupata maoni kuhusu maeneo yote ya rasimu ya katiba yanayohusu watu
wenye ulemavu,” alisema na kuongeza kuwa hilo lisiwazuie kutoa maoni
kuhusu maeneo mengine ya rasimu ya katiba.
“Nyie
pia ni sehemu watanzania na hata mkiwa viongozi mtakuwa viongozi wa
watanzania wote... kwa hiyo ipitieni rasimu yote na mtoe maoni katika
maeneo yote pia,” alisisitiza Jaji Warioba na kuongeza kuwa Tume yake
pia iliandaa Baraza Maalum kama hilo Zanzibar kwa kushirikiana na Umoja
wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ).
Akiongea
katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Shirikisho la Walemavu Tanzania
(SHIVYAWATA), Bw. Novatus Rukwago aliishukuru Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kwa kuwezesha kufanyika kwa baraza hilo na kusema kuwa mkutano
huo umeshirikisha vyama vyote kumi vya watu wenye ulemavu.
Alivitaja
vyama hivyo kuwa ni Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo (CHAWATA),
Chama cha Wasiiona (TLB), Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Afya ya Akili
(TUSPO) na Chama cha Watu Wenye Ulemavu Walioumia Uti wa Mgongo
Kilimanjaro (KASI).
Vyama
vingine vinavyohudhuria mkutano huo ni Chama cha Viziwi Tanzania
(CHAVITA), Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Mabaka ya Ngozi (PSORATA),
Chama cha Albino Tanzania (CAT), Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Akili
(TAMH), Chama cha Viziwi Wasioona (TASODEB) na Chama cha Watu Wenye
Ulemavu wa Vichwa Vikubwa na Mgongo Wazi (ASBAHT).
Kuhusu Gharama za Muungano
Katika
hatua nyingine, Jaji Warioba amefafanua kuhusu gharama za uendeshaji wa
muungano wa shirikisho la Serikali tatu ambao umependekezwa na Tume
yake katika rasimu ya katiba iliyozinduliwa Juni 3 mwaka huu.
Akijibu
swali la mjumbe mmoja wa Baraza hilo aliyeomba ufafanuzi kuhusu gharama
za uendeshaji wa Serikali ya Muungano ndani ya shirikisho, Jaji Warioba
amesema Tume yake imependekeza Serikali ya Muungano iendeshwe na mapato
yatakayotokana na ushuru wa bidhaa ambao unakua kila mwaka.
“Tumependekeza
chanzo hiki kikubwa cha ushuru wa bidhaa baada ya kupokea maoni ya
wataalam na kujiridhisha,” alisema na kufafanua kuwa mapato yanayotokana
na ushuru wa bidhaa yanatosha kuendesha shughuli za Serikali ya
Muungano inayopendekezwa.
Akiongea
kuhusu suala hilo katika mkutano huo, Mjumbe mwingine wa Tume hiyo Bw.
Ally Saleh amesema kwa sasa mapato ya ushuru wa bidhaa ni zaidi shilingi
trilioni moja na kuwa maoni ya wataalam ambayo Tume yake imeyapokea
yanaonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa mapato hayo yanakua kila mwaka.
“Kwa
hiyo mapato haya ya ushuru wa bidhaa yanatosha kuifanya Serikali ya
Muungano ijisimamie na mapato mengine waachiwe washirika wa Muungano,”
amesema.
Mkutano
huo wa Baraza Maalum la Watu Wenye Ulemavu unamalizika kesho (Alhamisi,
Agosti 16, 2013). Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea na mikutano
ya Mabaraza ya Katiba ili kupokea maoni kuhusu rasimu ya katiba.
Mikutano hiyo inatarajia kumalizika Septemba 2 mwaka huu.