KITUO CHA HAKI ZA BINADAMU KUMFIKISHA WAZIRI MKUU MAHAKAMANI
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk
Hellen Kijo-Bisimba akiwaonyesha waandishi wa habari, stakabadhi na hati
ya mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika
Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es Salaam jana. Picha na Michael Jamson
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimemfungulia
mashtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutokana na kauli yake aliyoitoa
bungeni hivi karibuni kwamba wanaokaidi maagizo ya dola wapigwe.
Hatua hiyo ya LHRC imepingwa vikali na Mkurugenzi
wa Mashtaka ya Umma (DPP), Dk Elieza Feleshi akisema hakuna uhalali wa
mashtaka yoyote dhidi ya kiongozi huyo sababu kauli ya Pinda kuwa pigeni
haikuwa piga ua.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo Bisimba
alifungua mashtaka hayo katika Mahakama Kuu jana akisema kuwa
wanamshtaki Waziri Mkuu kwa maelezo kuwa amekiuka kifungu cha Katiba
Ibara 13 (1). Pinda ametajwa kuwa ni mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo
namba 24.
Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi wa LHRC, Harold
Sungusia alisema jana kwamba, mwingine aliyeunganishwa katika kesi hiyo
ya kikatiba iliyofunguliwa na LHRC na Chama cha Wanasheria Tanzania
(TLS) ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Alisema katika kesi hiyo, kuna jopo la mawakili
wasiopungua 20 na kwamba wamepata saini za wananchi 2,029 wanaopinga
kauli hiyo ya Pinda na kuunga mkono kufunguliwa kwa kesi hiyo.
Mjumbe wa Bodi ya LHRC, Wakili Dk Ringo Tenga
alisema katika kesi hiyo wameangalia zaidi sheria na hasa haki za msingi
za binadamu na kwamba kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda inahatarisha haki
hizo.
Kauli yenyewe
Wakati wa Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa
Waziri Mkuu bungeni, Juni 19, mwaka huu, Waziri Mkuu akijibu swali la
nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu
aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi gani kubainisha na kuchukua hatua
stahiki, badala ya kusakama makundi fulani, tujue chanzo halisi cha
vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani vyombo vya dola
vinavyoshughulikia kwa sababu yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo
kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo vya dola?”
Waziri Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema...
mwishowe unaona anasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo,
umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... hamna namna
nyingine, maana wote tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa
misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni
imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema
muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine... maana tumechoka.” Kesi
hiyo itakayosikilizwa na majaji watatu, haina uhusiano na kesi nyingine
ambazo wajibu maombi hupewa siku 90 kujibu hoja zilizowasilishwa. Kesi
hiyo imefunguliwa kwa mujibu wa Katiba Sura ya Tatu.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia