Wakati Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ametoa
wito kwa nchi mbalimbali, mashirika ya kimataifa na Umoja wa Mataifa
kuiunga mkono mahakama hiyo kwa kusaidia kuwatia mbaroni watuhumiwa,
Rwanda kwa upande wake inadai bado inawasaka watuhumiwa 50,000 wa mauaji
ya kimbari ya mwaka 1994.
ICC
Aomba kuungwa mkono kuwatia mbaroni watuhumiwa: Rais Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Jaji Sang-Hyun Song Alhamisi ametoa
wito kwa nchi mbalimbali, mashirika ya kimataifa na Umoja wa Mataifa,
kuiunga mkono mahakama hiyo kwa kusaidia kuwatia mbaroni watuhumiwa
ambao bado wanaosakwa na mahakama yake. Alikuwa anawasilisha ripoti ya
Mahakama hiyo mjini New York, mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
katika maazimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake. Alitoa mfano wa
hati ya kukamatwa kwa Kiongozi wa waasi wa LRA nchini Uganda, Joseph
Kony na wenzake watatu ambao bado hawajatiwa mbaroni tangu 2005. Alisema
ni vigumu kwa mahakama hiyo kufanikiwa kuwanasa watu hao bila kuungwa
mkono na mataiafa mbalimbali.
Ataka mahakama imtoe Gbagbo kizuizini: Wakili wa Utetezi wa Rais wa
zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo Jumanne aliiomba Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) imtoa kizuzini kiongozi huyo akidai
kwamba mteja wake ni mgonjwa na ana hali mbaya ya kiafya kiasi kwamba
hawezi kutoroka. Wakili huyo aliieleza mahakama kwamba mteja wake hana
fedha na kutokana na kuugua, hawezi kutoroka. Mwendesha mashitaka kwa
upande wake alionya kwamba Bgagbo ambaye sasa yuko kizuizini akisubiri
hatua ya awali ya kusikilizwa kwa kesi yake,ana mtandao wa watu wengi
wanaomwunga mkono na kwamba wako tayari kusababisha ghasia kumrejesha
madaraka iwapo atatolewa kizuizini.
RWANDA
Rwanda yadai watuhumiwa 50,000 wa mauaji ya kimbari hawajakamatwa:
Rwanda Jumatano wiki hii imedai kwamba watuhumiwa zaidi ya 50,000 wa
mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 bado hawajatiwa mbaroni.Watuhumiwa hao
wamesambaa katika nchi mbalimbali za Kiafrika na Ulaya. Kwa mujibu wa
ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Rwanda, ni hati za kukamatwa kwa
watuhumiwa 146 tu ndizo zilizokwisha tolewa na kwamba ofisi hiyo bado
inashughulikia majalada ya wengine waliobaki.
WIKI IJAYO
Bemba aendelea kuwailisha mashahidi wa utetezi: Upande wa utetezi
katika kesi inayomkabili kiongozi wa zamani wa waasi wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean Pierre Bemba, Jumatatu ijayo
utaendelea kuwasilisha mashahidi wake wa utetezi. Kiongozi huyo
anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.