Diwani wa Kata ya Endiamtu Wilaya ya Simanjiro
Mkoani Manyara Lucas Zacharia (kulia) ambaye jana alikamata gari aina ya canter
lililokuwa limebeba magunia 120 ya mkaa bila kuwa na kibali,akizungumza na
baadhi ya watu waliokuwa kwenye gari hilo eneo la Tilili,sehemu kubwa ya wilaya
hiyo imegeuka na kuwa jangwa kutokana na ukataji miti kwa ajili ya biashara ya
mkaa ambapo gunia moja linauzwa sh18,000 wilayani humo.
DIWANI wa Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa
Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,Lucas Zacharia amekamata gari
lililokuwa limebeba zaidi ya magunia 120 ya mkaa bila ya kuwa na kibali cha
kuwaruhusu kukata mkaa.
Hivi sasa wilaya hiyo imepiga marufuku ukataji
miti na uchomaji mkaa kwenye wilaya hiyo ili kuinusuru na jangwa kutokana na
kukithiri kwa vitendo hivyo vinavyofanywa na watu wanaodaiwa kuwa wanaishi
mkoani Arusha.
Zacharia alilikamata gari hilo aina ya Canter juzi
kwenye eneo la Tilili wilayani humo akiwa anaelekea kwenye vikao vya
halmashauri hiyo na Ofisa mtendaji wa kata hiyo Edmund Tibiita na Ofisa mtendaji
wa kata ya shambarai Anna Mlomi.
Akizungumza wakati alipokamata gari
hilo,Zacharia alisema amelazimika kukamata gari hilo kwani ukataji miti na
uchomaji mkaa unachangia uharibifu wa mazingira na kusababisha jangwa wilayani
humo.
“Hivi sasa hatupati mvua kutokana na ukataji
miti na uchomaji wa mkaa hivyo tutasimama kidete katika kuhakikisha kuwa miti
haikatwi na uchomaji mkaa hauendelezwi katika wilaya yetu,” alisema Zacharia.
Alisema kuwekuwa na uwajibikaji mdogo katika
suala zima la ulinzi na usalama wa maliasili za wilaya hiyo kwa baadhi ya
watumishi kushiriki katika vitendo vya upokeaji rushwa na kuwaachia wachomaji
mkaa kwenye eneo hilo.
“Hivi sasa wilaya yetu imegeuka na kuwa jangwa
kutokana na kukithiri ukataji miti na uchomaji mkaa na kusababisha mvua
kutonyesha na kuathiri malisho ya mifugo na shughuli za kilimo,” alisema
Zacharia.
Alisema madiwani wa wilaya hiyo waliweka
sheria ndogo ya kutaifisha magunia yote ya mkaa yanayokamatwa na kila gari
litakalokamatwa litapigwa faini ya sh1 milioni ili kuhakikisha wanakomesha
vitendo hivyo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia