BARAZA la Madiwani wilayani Hai, limeelezea kutoridhishwa na
uandaaji wa kumbukumbu za vikao mbalimbali unaofanywa na wataalamu,
hali inayochangia kutumia muda mwingi kufanya marekebisho.
Wakizungumza kwenye kikao cha baraza, madiwani walitaka uongozi wa
halmashauri hiyo kueleza sababu ya kuendelea kuongezeka kwa makosa ya
kiuandishi kwenye mihtasari mbalimbali ya vikao, hivyo kusababisha
kutumia muda mwingi wa vikao kufanya masahihisho.
Madiwani walitaka kujua kama mihtasari hiyo baada ya kuandaliwa na
watendaji kama inapitiwa pia na timu ya wataalamu ya wilaya (CMT), ili
kupunguza makosa hayo yanayoonekana.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Melkizedeki Humbe, alisema suala hilo
hawezi kulizungumzia kwenye kikao hicho, ila tayari anazo hatua
binafsi atakazochukua kuhusiana na wahusika.
“Kuhusu makosa na usahihishaji naomba kwa ridhaa yako kwa leo
nisilitolee uamuzi hapa, ila ninajua hatua binafsi ambayo mimi
nitachukua ila sitazungumzia kwenye baraza kwa sababu ya wahusika,”
alisema.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Clement Kwayu, alisema mkurugenzi
amekwishayaona madhaifu hayo kutokana na kuwepo kwa maswali mengi juu
ya kuongezeka kwa makosa katika uandaaji wa taarifa muhimu za vikao vya
baraza.