Dar es Salaam. Vifo,
uharibifu wa mali, miundombinu na mafuriko, msongamano wa magari,
baadhi ya wakazi wa jiji hilo kukimbia makazi yao, wengine kulala kwenye
magari na nyumba za wageni vimewakumba wakazi wa Jiji la Dar es Salaam
na vitongoji vyake, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa siku ya
nne mfululizo.
Timu ya waandishi wa gazeti la Mwananchi
walifanya uchunguzi maeneo mbalimbali na kushuhudia hali halisi ilivyo,
huku wanawake na watoto wakionekana kupata shida zaidi kwa kukaa nje ya
nyumba zao, wengine kuhamia kwenye majengo ya shule.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam alisema jana kuwa
walikuwa wakiendelea kukusanya taarifa za maafa ikiwamo vifo alivyosema
ni vingi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadik alisema kuwa yupo kwenye kikao na watatoa taarifa zaidi za maafa baadaye.
Tegeta, Boko na Bunju
Mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka minne, amefariki dunia baada
ya nyumba aliyokuwa akiishi kujaa maji na kushindwa kujiokoa kutokana na
ulemavu, wakati mama yake akiwa kwenye shughuli za biashara.
Majirani wa mtoto huyo walisema tofauti na kawaida yao kumtoa mtoto huyo
mvua inaponyesha, jana walimsahau na mama yake aliporejea alikuta maiti
ya mtoto wake ikielea chumbani.
Katika mvua hizo takribani kaya 180 zimekumbwa na mafuriko huku wakazi wake wakijikuta hawana pa kwenda.
“Mimi nimekuwa hapa tangu Tanu imezaliwa, nyumba yangu imejaa maji
nimeshazeeka sina mtu wa kunisaidia, wala sijui wapi nitakwenda. Nomba
Serikali inisaidie,”alisema Hussein Ngaoma ambaye ni mjumbe wa nyumba
kumi katika eneo hilo.
Naye Husna Ally ambaye pia nyumba yake imekumbwa na mafuriko alisema:
“Nasikitika, maana nimepata hasara kubwa. Mimi ni mfanyabiashara katika
eneo hili la Boko, nina duka la kuuzia samani limejaa maji na sijaweza
kuokoa chochote. Mzigo wa Sh30 milioni umeharibika wote.”
Jeti Lumo
Katika eneo hilo licha ya kujaa maji, mfanyabiashara ndogondogo
amefariki dunia kwa kusombwa na maji alipokuwa akijaribu kuokoa jiko
lake la kuchomea mishikaki lililotumbukia kwenye mtaro.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia