Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, Mbumge wa Karatu mchungaji Israeli
Nase(Watatu kushoto),Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe(Wapili
kushoto),Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo(kushoto) na Mkurugenzi wa
Utumishi na utawala wa TRA aliyemwakilisha Kamishna mkuua wa TRA Bwana
Abubakari Kunenge(wapili kulia) na kulia ni mwakilishi wa ofisi ya TRA
Mkoa Bi.Caroline Ntinku.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akifunu kitambaa katika jiwe la msingi
kuashiria kufungua rasmi ofisi ya Mamlaka ya mapato Wilaya ya Karatu leo
mjini Karatu.
RAIS Jakaya
Kikwete amesisitiza msimamo wa Serikali, kwamba mashine za elektroniki
za ukusanyaji kodi (EFDs), lazima ziendelee kutumika nchini. Alisema
hayo jana wakati alipozungumza kwenye uzinduzi wa Ofisi za Mamlaka ya
Bandari (TRA) mjini Karatu katika Mkoa wa Arusha, na kuongeza kuwa
changamoto za mashine hizo zinajadilika.
“Najua kuna
maneno mengi kuhusu suala hili. Kwa hiyo maelekezo yangu ni kwamba kaeni
chini, mjadili matatizo yaliyopo na kupata ufumbuzi. Kama ni suala la
bei pia linazungumzika lakini tunahitaji mfumo huu wa malipo ya kodi,”
alisema.
Aliagiza
viongozi wa TRA kukaa chini na wadau na watumiaji wa mashine hizo
kuzungumza na kutafuta majawabu yanayolalamikiwa na wadau.
Alisema
kuacha kutumia mashine hizo ni kurudi nyuma kwa kuwa zimeshaanza
kutumika duniani kote na hata nchi jirani baadhi zimeshaanza kutumia na
nyingine ziko katika maandalizi ya kutumia.
“Kwenye hili
tusirudi nyuma kwa sababu tukifanya hivyo, tutakuwa tunarudi nyuma sana
kwa sababu dunia nzima inaelekea huko na hata majirani zetu wote ama
wameanzisha mfumo huo ama wanajiandaa kuuanzisha.”
“Hatuwezi
kurejea kwenye mfumo ule wa kutumia vijirisiti. Mfumo wa sasa unaifanya
kazi ya kukusanya kodi kuwa rahisi kwa Serikali yenyewe na kwa walipa
kodi. Najua watu hawapendi kulipa kodi lakini hakuna njia ya jinsi ya
kuendelea isipokuwa kwa kulipa kodi,” alisisitiza Rais Kikwete.
Kwa muda
mrefu TRA imekuwa ikisisitiza kuwa utaratibu wa kutumia mashine za EFDs
ulianzishwa kwa lengo la kumrahisishia mfanyabiashara utunzaji wa
kumbukumbu za biashara za kila siku pamoja na kuondoa usumbufu wakati wa
ukadiriaji wa kodi. Mfumo huo wa kutumia mashine za kodi za
kielektroniki ulianza kutekelezwa kwa awamu.
Awamu ya kwanza ilianza mwaka 2010 kwa wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Awamu ya
pili ilianza 2013 ikiwahusu wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kwenye
VAT ambao mauzo ghafi kwa mwaka ni Sh milioni 14 na zaidi.
Kwa mujibu
wa taarifa za TRA, wafanyabiashara zisizo rasmi zikiwemo za mama lishe
na wale wanaotembeza bidhaa barabarani, hawahusiki kwa sababu hawana
sehemu maalumu ya kufanyia biashara.
Miongoni mwa
wafanyabiashara wanaotakiwa kutumia mashine hizo ni wenye maduka ya
vipuri, mawakili, maduka ya jumla, wafanyabiashara wakubwa wa mbao,
migahawa mikubwa, maduka ya simu na vipuri vyake, baa na vinywaji
baridi, studio za picha, biashara za kutoa huduma za chakula, wauzaji wa
pikipiki, maduka makubwa ya nguo na biashara zinginezo Kwa mujibu wa
taarifa za TRA, kwa nchi nzima walengwa ni wafanyabiashara laki mbili tu
kwa awamu ya pili kati ya wafanyabiashara zaidi ya milioni moja na nusu
ambao wamesajiliwa kulipa kodi.
Rais
Kikwete alikuwa katika ziara ya siku moja kukagua shughuli za maendeleo
wilayani Karatu katika Mkoa wa Arusha na jana na leo ameanza ziara kama hiyo
ya siku moja katika Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.