SERIKALI imelaumiwa kwa kutosapoti michezo, hali inayozifanya klabu za mikoani kushindwa kupanda daraja hadi kufikia ligi kuu.
Akizungumza na LIBENEKE LA KASKAZINI jijini hapa , Katibu wa
Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), Adam Brown, alisema kuwa, klabu
za mkoani hapa zinashindwa kushika nafasi nzuri kwenye mashindano hasa
ya kitaifa na kimataifa, kutokana na viongozi wa serikali kuanzia ngazi
ya mkoa hadi kata kushindwa kuzisapoti.
Mbali na serikali, Brown alisema kuwa, mkoani hapa kuna wawekezaji
wengi wenye viwanda, mashamba makubwa ya biashara pamoja na
wafanyabiashara wakubwa, lakini wamekuwa wagumu kusapoti suala la
michezo pale maombi yanapopelekwa, hali inayosababisha ukata na
kushusha kiwango cha michezo.
“Wewe mwenyewe unashuhudia klabu za hapa mkoani ni tofauti na za
mikoa mingine inayopata sapoti kwa wadau wa michezo, kwa mfano JKT
Oljoro wakishindwa kuwafunga Yanga, watarudi nyumbani na madhara yake
Kanda nzima ya Kaskazini itakosa timu ya ligi kuu,” alisema na
kuongeza:
“Mimi niwaombe tu wadau wa michezo na viongozi wa serikali, wawe
wanachangia na kudhamini klabu hizi, siyo kufurahia tu mafanikio au
kuponda, bali wawe na michango itakayowezesha klabu hizi kushiriki ligi
mbalimbali na mechi za kirafiki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, alipokuwa
akijibu malalamiko hayo, alisema kuwa hakuna mafungu yaliyopo kwa ajili
ya michezo, hivyo kama watahitaji fedha ni vema kuandika maombi
(proposal), ambako kwa msimu ujao wa bajeti, fedha zikiwepo watapewa.
“Sisi kama serikali hakuna fedha inayotengwa kwa ajili ya michezo,
halafu tambua pia kuwa hakuna fedha inayokaa haina kazi, si
wanakurupuka na kusema wanataka fedha na wakapatiwa, bali waandike
proposal ya kuombea fedha, na msimu wa bajeti ukifika, kama itapatikana
watapewa kama hakuna basi,” alisema Mongela.