Jackline Sakilu akimaliza mbio za kilomita 10 kwa wanawake |
MWISHONI mwa wiki, Aprili 12 mwaka huu, macho na masikio ya
Watanzania wengi yalielekea katika Kijiji cha Monduli Juu, kilichopo
Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, kufuatilia kumbukumbu za miaka 30
tangu kufariki kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Moringe
Sokoine.
Maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu
wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, yaliadhimishwa kwa matukio mengi ya
kukumbukwa, lakini moja ya matukio yaliyotokea katika kumbukumbu hizo,
ni msimu wa pili wa mbio za Sokoine Mini Marathon mwaka 2014.
Mbio hizo zilianza majira ya saa mbili asubuhi, ambapo pamoja na
kuwepo kwa ushindani mkubwa, kulikuwa na matukio mengi yasiyo ya
kawaida, likiwemo la wanariadha kulazimika kupisha magari.
WANARIADHA WANASA KWENYE TOPE
Zikiwa zimesalia takribani kilomita mbili mbio za kilomita 10
zimalizike, wanariadha walijikuta wakibadilishana baada ya njia kujaa
matope huku kukiwa na mgari mengi yaliyokwama barabarani.
Tukio hilo lilibadili mwenendo mzima wa mbio, ambako mwanaridha
aliyekuwa akiongoza mbio hizo kwa muda mrefu, Alfonce Felix kutoka
klabu ya Holili (HYAC), alijikuta akishindwa kwenda na kasi yake ya
awali, kitendo kilichompa nafasi mwanariadha mkongwe, Fabian Joseph
kutumia uzoefu wake kumpita na kuongoza mbio hadi mwisho.
FABIAN JOSEPH NA JACKLINE SAKILU WASHINDA KILOMITA 10
Mwanariadha Fabian Joseph kutoka Arusha, ambaye ni bingwa wa zamani
wa dunia km 21, alishinda mbio za km 10 upande wa wanaume akitumia dk.
34:28.04 akimpita mwanariadha chipukizi, Alphonce Felix ikiwa imesalia
kilomita moja mbio hizo zimalizike.
Nafasi ya pili ilikwenda kwa Alphonce Felix kutoka klabu ya Holili,
ambaye alitumia dk. 34:45.39 huku bingwa mtetezi, Dickson Marwa kutoka
wa HYAC, akiridhika na nafasi ya tatu akitumia dk. 34:57.47.
Mshindi wa pili mbio za wanaume, kilomita 10, Alphonce Felix kutoka Holili |
Kwa upande wa wanawake, bingwa wa mbio za Kilimanjaro Marathon Km 21,
Jackline Sakilu, kutoka klabu ya JWTZ Arusha, aliibuka mshindi
akitumia dk. 40:01:26, huku nafasi ya pili ikienda kwa Nathalia
Elisante wa Arusha dk. 40:51:27 na nafsi ya tatu ikaenda kwa Failuna
Abdi wa Winning Spirit dk. 41:13:54.
VIJANA HOLILI WATAWALA KM 2
Tukio jingine lililojiri kwa upande wa michezo mwaka huu, ni kitendo
cha wanariadha wasichana wachanga kutoka HYAC mjini Holili, mkoani
Kilimanjaro kuteka mbio za kilomita 2.
Katika mbio hizo, mshindi wa kwanza alikuwa ni Adelina Audax,
aliyewaongoza wasichana wenzake kutawala mbio hizo akifuatiwa na Neema
Mathias na nafasi ya tatu ikienda kwa Lidiuna Godfrey.
MICHEZO MINGINE
Kulikuwa na michezo mbalimbali ukiacha riadha, ambapo mchezo wa jadi
wa kurusha mkuki nao haukuachwa nyuma, huku kukiwa na mabadiliko
makubwa.
Kati ya mabadiliko hayo, ni waandaaji wa mwaka huu kuandaa zawadi kwa
ajili ya walemavu, tofauti na ilivyokuwa katika msimu wa kwanza wa
mbio hizo.
Nyumba ya marehemu Sokoine iliyoko Monduli Juu, ilifurika viongozi
mbalimbali ambao kwa pamoja, walijumuika na familia kuadhimisha
kumbukumbu ya miaka 30 ya kifo cha kiongozi huyo mzalendo na
mwanaharakati wa kweli, Edward Moringe Sokoine.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia