JESHI
la Polisi limewataka wafanyabiashara wakubwa hasa wamiliki wa kumbi za
starehe jijini Arusha na Halmashauri zake zote kuhakikisha wanafunga
mitambo ya kamera (CCTV CAMERA) kwenye maeneo ya biashara ili iwe rahisi
kuwabaini wanaotaka kusababisha milipuko ya mabomu.
Kauli hiyo
imekuja ikiwa ni siku moja mara baada ya watu wasiofahamika kutega bomu
katika nyumba ya kulala wageni ya Arusha Night Park, huku bomu lingine
likiwa limetegwa katika baa nyingine ya Washington Baa mapema juzi.
Ushauri
huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya
Mngulu, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hali ya
usalama wa Mkoa wa Arusha kutokana na kukumbwa na milipuko ya mabomu ya
mara kwa mara.
Alisema hadi sasa takwimu zinaonesha kuwa matukio
hayo yanajirudia, hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari kuanzia
sasa kwani hata mabomu ya kienyeji nayo yanatumika sana kuua na
kujeruhi.
Alisema hata uongozi mzima wa Mkoa wa Arusha nao
unatakiwa kuhakikisha kuwa kuanzia sasa unaanza mikakati ya kufunga
vifaa mbalimbali ambavyo vitakavyoweza kuwabaini wahalifu wote wa mabomu
kwani uwezekano wa kuwatambua hata kupitia vifaa hivyo upo.
Aliongeza
kuwa wamiliki wa kumbi za starehe nao pia wachukue tahadhari kuanzia
sasa ambapo wanatakiwa kulinda uhai wa wateja wao na kamwe wasijisahau,
hivyo wanahitajika kuwa na vifaa vya kisasa hasa CCTV CAMERA ili
kuharakisha zaidi upelelezi.
"Kutokana na hali ya mabomu ilivyo
kwa sasa ni muhimu sana kwa kila mtu kuchukua tahadhari ingawaje na sisi
tutahakikisha tunawalinda ipasavyo wananchi wetu na hatutaweza kuruhusu
tena Arusha ikapatwa na janga lingine la mabomu, ingawaje pia
tunaimarisha ulinzi kila kona hususan kwenye mikusanyiko mikubwa ya
watu," aliongeza Isaya.
Katika hatua nyingine alisema kuwa Jeshi
la polisi nchini limetangaza kitita cha milioni 10 kwa mtu yeyote
atakayewezesha kutoa taarifa sahihi na kukamatwa kwa mtuhumiwa
aliyesababisha mlipuko wa bomu katika nyumba ya kulala wageni (Arusha
Night Park)
Wakati huo huo, Polisi mkoani hapa wameahidi
kuimarisha ulinzi zaidi wakati wa Sikukuu ya Pasaka ambapo watatumia
vifaa mbalimbali ili kuweza kuepusha jamii na milipuko ya mabomu.
Kamanda
wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema kuwa ulinzi katika
maeneo yote ya mikusanyiko ya watu utakuwa wa kutosha na hivyo jamii
haipaswi kuwa na woga wala hofu ya aina yoyote ile
Sabas alisema
watatumia vifaa mbalimbali kuimarisha ulinzi kwenye mikesha na
mikusanyiko ya watu kuanzia siku ya Ijumaa Kuu hadi Pasaka. "Tutatumia
rasilimali watu, farasi, mbwa na nyinginezo na hii ni kutokana na kuwa
tunataka wananchi waweze kusherehekea siku hiyo kwa amani na utulivu,"
alisema.