WADAU wa michezo mkoani Arusha wamesikitishwa na uchakachuaji wa
mapato katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Oljoro JKT na Yanga
ulioingiza sh milioni 25.3.
Katika mechi hiyo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Kwa uwezo wa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta na idadi ya watu
walioingia kwa kiingilio cha sh 5,000 na 15,000 imeonekana dhahiri
uchakachuaji ulikuwa mkubwa na hali hii inazidi kuwakatisha tamaa wadau
wa soka mkoani Arusha.
Uwezo wa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ni watu 13,000 ukijaa na
mahudhurio ya juzi mashabiki waliojitokeza wanakadiriwa kufikia asilimia
75 ya uwanja, ambao ni kadirio la watu zaidi ya 9,000, ambayo
ukizidisha kwa kiingilio cha sh 5,000 ni sh milioni 45 achilia mbali
watu 900 waliokaa jukwaa kubwa ambalo kiingilio chake kilikuwa ni sh
15,000.
Alipoulizwa juu ya mapato hayo, Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa
Arusha (ARFA), Adam Brown, alisema ni kweli mchezo huo uliingiza sh
milioni 25 lakini hakuwa na mnyambulisho wa makato, kwani jukumu hilo
liko chini ya mweka hazina wa chama na msimamizi wa kituo.
Uchunguzi wa LIBENEKE LA KASKAZINI umebaini baadhi ya mgawanyo wa
mapato hayo kuwa ni pamoja na kila timu kuambulia sh 5,327,319 Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT), sh 3,940,000, mfuko wa maendeleo ya ligi
(FDF), sh 892,757 gharama za kuchapa tiketi sh 1,755,000, Bodi ya Ligi
sh 1,755,000 na gharama za mchezo sh 1,700,000.
Hata hivyo, Brown amekiri watazamaji kuwa wachache, kulikochangiwa na
ukweli kwamba, Oljoro walikuwa wanashuka daraja na Yanga walishapoteza
uwezo wa kutetea ubingwa na mashabiki wengi walikwenda kushuhudia
pambano la Ligi ya Uingereza kati ya Liverpool na Manchester City
lililokuwa likioneshwa kwenye runinga.
“Ili kurejesha imani kwa mashabiki wa soka, lazima sekta husika
kufanyia kazi mapato ya viingilio uwanjani, kwani bila hivyo inakatisha
tamaa kwa wadau, mashabiki na hata wachezaji,” alisema shabiki
aliyejitambulisha kwa jina moja la Jumanne