HIZI NDIZO ATHARI ZA KUTOTUMIA SARAFU MOJA KATIKA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI

Meneja wa benki ya CRDB tawi la Kahama,Luther Mneney.
Imeelezwa kuwa kutokuwapo kwa matumizi ya sarafu moja katika Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, kumeleta athari kubwa zitokanazo na matumizi makubwa ya fedha za kigeni katika nchi wanachama wa jumuia hizo.
Hayo yalielezwa na mwezeshaji kutoka benki ya CRDB makao makuu, Ngeleja Mcharo, katika semina ya wanahisa wa benki hiyo iliofanyika wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Lengo la semina hiyo ilikuwa ni kukuza uelewa wa soko la mitaji.

Mcharo alisema kuwa matumizi ya fedha za kigeni katika Soko la Mitaji la Afrika Mashariki, yameleta changamoto hususan kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara katika nchi hizo.

Sambamba na hayo, pia alisema uelewa mdogo katika masuala ya Soko la Pamoja ni changamoto ikiwa ni pamoja na baadhi ya sheria, kanuni, sera na vikwazo kutoondolewa katika muda uliopangwa.

Kuhusu upande wa wafanyabiashara wa Tanzania, Mcharo alisema kuwa wanashindwa kuhimili ushindani wa soko la pamoja kutokana na kutokuwa na mitaji mikubwa.
Alisema hali hiyo inawafanya wafanyabishara wa nje kushikilia soko hapa nchini.

Kwa upande wao, washiriki wa semina hiyo walisema kuna umuhimu wa semina za elimu ya hisa ziwapo mara kwa mara ili kuwajengea uwezo zaidi wanahisa juu ya masuala ya kukuza mitaji.

Mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Joseph Manyala, alisema kuwa vikao vingi vya benki ya CRDB hufanyika jijini Arusha, hali inayofanya washiriki wengi kutoka sehemu za mbali kushindwa kuhudhuria.

Awali, akifungua semina hiyo, Meneja wa benki ya CRDB tawi la Kahama, Luther Mneney, aliwataka wanahisa kuifanya benki hiyo kama mali yao na wazidi kununua hisa kwa faida zao.

Mneney alisema kuwa kwa sasa vijana wengi nchini hawataki kujua mambo ya kibenki kama ya kukuza mitaji au mambo ya hisa, hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kutokuwa na uelewa kuhusu mambo ya kibenki.

“Vijana wengi wameshika mambo mengi ambayo hayawasaidii katika maisha kama vile mambo ya mipira ya Ulaya, hali ambayo inawafanya kupitwa na wakati na mambo ya kibenki na Watanzania msiwe makarani kwa mitaji ya watu wengine,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post