Miaka 42 iliyopita,
Aprili 7, 1972; Rais wa Serikali ya awamu ya kwanza ya Mapinduzi na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abeid Amani Karume, aliuawa kwa kupigwa risasi
katika mazingira na sababu za kutatanisha.
Risasi nane zilitolewa
mwilini kwake mwili wake ulipofikishwa kwenye Hospitali ya V. I. Lemin, mjini
Unguja kwa uchunguzi, sawa na idadi ya miaka minane ya utawala wake tangu 1964
hadi kifo chake.
Ilikuwa hivi:
Rais Karume na Makomredi wenzake wa Chama cha Afro-Shirazi (ASP) alikuwa na
mazoea ya kucheza karata, damma au dhumuna kwenye ukumbi wa ofisi za makao
makuu ya Chama hicho Kisiwandui, kila jioni kama sehemu ya mapumziko.
Siku hiyo alifika saa 11.00 jioni akiwa na walinzi wake, akaingia ndani nao
wakabaki nje kulinda.
Ikafika zamu yake
kucheza; akawa anacheza na Mzee Maalim Shaha Kombo ambaye alionekana
kulemewa. Ndipo Karume akamwita Mzee Mtoro Rehani ajitayarishe baada ya
Kombo, naye akaitikia kwa kuaga kwanza aende msalani kujisaidia.
Sekunde chache baada
ya hapo na kabla Mzee Mtoro Rehani hajarejea kutoka msalani, ghafla watu wawili
wenye silaha walivamia chumba alimokuwa Karume na wenzake na kumimina risasi
wakimlenga; na kufumba na kufumbua, akawa katika dimbwi la damu kimya,
amepoteza uhai. Hakuna mtu mwingine aliyeuawa mbali na kujeruhiwa tu,
mmoja wao akiwa Katibu Mkuu wa ASP, (sasa) Hayati Thabit Kombo Jecha.
Risasi uaji (the fatal bullet), mbali ya risasi zote, iliyochukua uhai wa
Karume ilitoka kwenye bunduki ya Luteni Hamoud Mohammed Hamoud wa Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWT), ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa uvamizi huu na
aliyefyatua risasi ya kwanza wakati Karume akicheza na wenzake.
Inasemekana, Hamoud aliuawa papo hapo na mlinzi wa Karume.
Wauaji wengine
waliofuatana na Hamoud katika uvamizi huo ni Kapteni Ahmada Mohamed, Koplo
mmoja wa jeshi ambaye jina lake halijafahamika hadi leo, na raia mmoja
aliyekwenda kwa jina la Ali Khatibu Chwaya, ambao inaelezwa wote hao waliuawa
kwenye mapambano ya silaha nje ya eneo la tukio.
Dakika chache baada ya
mauaji kutokea, alifika Kanali Ali Mahfoudhi na askari mwingine, Kapteni Makame
Hamis, wakauchukua mwili wa Karume na kuukimbiza hospitali.
Itakumbukwa, Kanali
Mahfoudhi ni mmoja wa vijana wa Umma Party (UP) cha Abdulrahman Mohamed Babu,
kilichoungana na ASP baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kuunda Serikali
ya mseto. Ni kati ya vijana waliopelekwa Cuba kwa mafunzo ya kijeshi, na ni
mmoja wa wapiganaji walioendesha mapambano ya kisayansi usiku wa Mapinduzi na
kukamata uwanja wa ndege mchana Aprili, 1972.
Ni mmoja wa
wanaharakati wa siasa za mrengo wa Kikomunisti ambao hawakutakiwa Zanzibar
wakati wa utawala wa Karume, hivi kwamba kufuatia Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, Aprili 26, 1964, Karume alishinikiza kwa Nyerere wapewe kazi Tanzania
Bara aweze “kupumua” ambapo Mahfoudhi alipewa cheo cha Mkurugenzi wa Operesheni
katika JWT.
Wengine ambao
hawakutakiwa ni pamoja na Babu mwenyewe aliyepewa Uwaziri wa Mipango ya Uchumi,
na kama tulivyoona makala zilizopita, hasimu mwingine wa Karume, Othman
Sharrif, ambaye alifanywa Afisa Mifugo wa Mkoa, Mtwara au Mbeya, na Balozi
Salim Ahmed Salim wakati huo Balozi wa Zanzibar nchini Misri ikaridhiwa
aendelee kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano nchini humo.
Tuache hayo, lakini
hapa swali linazuka: Kwa kuwa Kanali Mahfoudh hakuwa kipenzi cha utawala
wa Karume tangu mwaka 1964, ilikuwaje akawa Afisa wa kwanza kuwa kwenye tukio
kabla ya maafisa wengine vipenzi, kama vile Kanali Seif Bakari ambaye alikuwa
pia Mkuu wa Usalama wa Taifa Zanzibar ambalo halikuwa jambo la Muungano, na
wengineo?
Je, alikuwa katika
ziara ya kikazi wakati mkasa huu ukitokea au alijua kilichotarajiwa kutokea?
Kwa nini alikuwa mmoja wa washitakiwa zaidi ya 100 kwa tuhuma za mauaji hayo,
na mmoja wa watuhumiwa 18 miongoni mwa hao walioshitakiwa wakiwa Tanzania Bara,
Abdulrahman Babu akiwa mmoja wao.
Kuna dhana mbili
kinzani kuhusu jinsi Karume alivyouawa na hatima ya wauaji. Dhana moja inadai
kwamba, watu wanne walivamia mahali alipokuwa Karume na wenzake, wakamimina
risasi mara nne au mara tano hivi, risasi ya kifo ikampata Karume shingoni
akafa, huku zingine zikiendelea kumiminwa kulenga meza walipokuwa.
Inadaiwa kuwa Hamoud
aliuawa kwenye eneo la tukio, ambapo wawili waliuawa baadaye na vyombo vya
usalama (kwa mapambano?) na mmoja alijiua.Dhana ya pili inadai
kwamba Hamoud alikufa kwenye eneo la tukio katika mazingira ya kutatanisha, ama
kwa kujipiga risasi kuepuka kukamatwa hai na kuteswa baada ya kuona asingeweza
kutoroka; au alijeruhiwa vibaya na walinzi wa Karume, kisha Ahmada akampiga
risasi na kumuua kumwepusha kuteswa na kutoa siri kama angekamatwa hai, kisha
(Ahmada) akaweza kutoroka kwenye eneo la tukio.
Juu ya utata huu
kuhusu hatima ya wauaji, ni ukweli kwamba ni Luteni Hamoud pekee aliyeuawa
kwenye eneo la tukio na washiriki wengine katika mauaji waliweza kutoroka eneo
la tukio na baadaye kuuawa katika mazingira yasiyofahamika.
Kufuatia mauaji hayo,
watu 1,100 walikamatwa na kuhojiwa juu ya kuhusika au kutohusika kwao na
mauaji, wengi wakiwa viongozi na wanachama wa zamani wa Umma Party, chama cha
Babu na wanachama mashuhuri wa ASP wenye siasa za mrengo wa kikomunisti.
Yote haya
yanaturejesha kwenye swali letu la awali: je, kuuawa kwa Karume kulikuwa
na lengo la kulipiza kisasi kwa chuki binafsi, kama baadhi ya watu wanavyodai,
au lilikuwa jaribio la Mapinduzi lililoshindwa kwa Serikali ya Mapinduzi? Ni
nani huyu Luteni Hamoud Hamoud aliyeongoza mauaji na kwa nini?
Je, lengo lilikuwa ni
mauaji hayo pekee au kulikuwa na mpango mkubwa zaidi nyuma? Ukiongozwa na nani?
Kupata majibu ya
maswali haya, hatuna budi kuiangalia hali ya kisiasa Zanzibar baada ya
Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na baada ya Muungano na Tanganyika, Aprili 26,
1964.
Kama nilivyoeleza
katika mfululizo wa makala nne hivi karibuni katika gazeti hili kuhusu jinsi
“Field Marshal” John Okello alivyoongoza Mapinduzi ya 1964, na kuundwa kwa
Serikali ya Mseto kati ya vyama vya ASP na Umma, lengo kuu la Karume lilikuwa
ni kuzivunja nguvu za wanaharakati wa Umma Party na za wakomunisti wa ASP
walioshabihiana kimawazo na kimtazamo wa kitaifa na wana-Umma Party na kumnyima
Karume usingizi.
Lakini tofauti na
matarajio ya Karume, hatua hiyo iliwaleta karibu zaidi wanamapinduzi hao na
kumnyima zaidi usingizi kwa hofu ya kupinduliwa, wakimtuhumu kushindwa kuongoza
na kusimamia madhumuni ya Mapinduzi Visiwani.
Mungu bariki kwa
Karume, ukatokea Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika mwaka huo, akaona
vyema awasambaratishe kwa kuwatafutia nafasi Tanzania Bara ambako wasingeweza
kufurukuta.
Waliokumbwa na kadhia
hiyo ni pamoja na Abdulrahman Babu (Umma) na aliyepewa Uwaziri wa Mipango na
Uchumi kwenye Serikali ya Muungano; Kassim Hanga (ASP) aliyeteuliwa Waziri
katika Ofisi ya Rais wa Jamhuri, Mambo ya Muungano; Salim Ahmed Salim (Umma)
aliyeteuliwa Balozi nchini Misri.
Wengine ni Othman
Sharrif (ASP) aliyeteuliwa Balozi nchini Marekani, lakini Karume akampinga
Nyerere akidai hastahili, uteuzi ukafutwa; badala yake akateuliwa kuwa afisa
mifugo katika moja ya mikoa ya Kusini Tanzania, Mbeya au Mtwara, na Kanali Ali
Mahfoudh (Umma) aliyeteuliwa Mkurugenzi wa Operesheni katika Jeshi la Wananchi
(JWT), na wengineo.
Kwa wale wenye maoni
tofauti na ya kukosoa Serikali waliobaki Visiwani, hasira ya Karume aliyetawala
kwa mkono wa damu iliwashukia, wengi walikamatwa na kutiwa kizuizini na pengine
kupoteza au kuuwawa kikatili na katika mazingira ya kutatanisha. Mmoja ya
waliouawa kikatili kizuizini ni Mzee (mwanaharakati) Mohamed Hamoud, baba yake
Luteni Hamoud Mohamed muuaji wa Karume.
Tangu Mapinduzi ya Januari 12, 1964, Zanzibar haikuwa na Katiba
wala Sheria; iliongozwa kwa Amri za Rais (Presidential Decrees) kadri alivyoona inafaa. Na kwa mujibu wa Gazeti la “The
Tanganyika Standard” la March 9, 1968, Karume aliapa kutofanya uchaguzi wala
kuwa na Katiba Kisiwani kwa miaka 50 tangu 1964 – 2014 Kwa madai kwamba
“chaguzi zote ni vyombo vya mabeberu kuwakandamiza wananchi”.
Na kadiri kalamu ya
Karume ya wino wa damu ilipozidi kuandika historia ya ukatili, udikteta na
umwagaji damu kwenye kurasa ngumu za kukwaruza ndivyo alivyojichongea na
kujiongezea upinzani na uadui kwa jamii ya Kizanzibari.
Kufikia mwaka 1967
hofu ya Karume dhidi ya wenzake na kwa nafasi yake ilitia fora kiasi cha
kuogopa kivuli chake mwenyewe. Na ili kuendelea kuwamaliza wenzake, mwaka huo
zilitungwa tuhuma za uongo dhidi ya watu 14 makada wa ASP katika kumpindua,
zikiwalenga hasa wenye fikra za kikomunisti.
Walioingizwa kwenye
tuhuma hizo ni pamoja na mawaziri wa Serikali yake mabwana Abdallah Kassim
Hanga, Salehe Saadallah Akida, Abdul Aziz Twala na makatibu wakuu wa wizara,
Aboud Nadhif na Mdungi Ussi na baadaye Othman Sharrif.
Wote waliokuwa
Visiwani walikamatwa, kisha Karume akamwomba Nyerere kuwarejesha Zanzibar
kutoka Bara, Othman Sharrif na Hanga ili “wakahojiwe” lakini wote wakaishia
kuuawa kikatili bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mmoja wa mashahidi wa
uongo walioandaliwa dhidi ya “watuhumiwa” kwa vyombo vya Karume, alikuwa Ahmada
ambaye kwa uongo wake, watu wanne akiwamo Hanga, Twala, Saadallah na Othman,
walinyongwa mwaka 1969. Kwa uongo huo, Ahmada alizawadiwa cheo cha
kapteni jeshini. Ni Kapteni Ahmada huyu, aliyeshiriki kwenye mauaji ya
Karume miaka mitatu baadaye.
Kwa hofu ya jamii ya
Kizanzibari kufikiwa na fikra na mawazo mapya ya kimaendeleo, Karume alipiga
marufuku vijana wa Kizanzibari kwenda nje kwa masomo ya juu ikiwa ni pamoja na
Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam; alipiga marufuku pia ujenzi wa Chuo Kikuu
Visiwani.
Mbali na kutokuwapo
kwa utawala wa sheria enzi za Karume, unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi kwa
misingi ya historia na kisiasa ulitia fora. Kwa mfano, mwaka 1966, alitoa amri
(decree) kuwanyima wazazi haki ya kuwakataa wanaume walioposa binti zao kama
njia ya kuondoa ubaguzi wa rangi.
Kwa sababu hii,
wasichana, hasa wale wa Kiarabu walilazimishwa kwa nguvu ya Serikali kuolewa
kwa nguvu. Karume mwenyewe, wakati huo akiwa na umri wa miaka 65, aliwania kuoa
kwa nguvu, wasichana wanne wa Kiajemi, na alipokataliwa, aliamrisha wazazi wao
watiwe kizuizini na kuchapwa viboko kwa kosa la kuzuia mpango wa ndoa
mchanganyiko, na baadaye kutimuliwa Zanzibar.
Chini ya mpango huo,
raia wa kigeni waliotaka kuchumbia wasichana wa Kizanzibari walitakiwa kuilipa
Serikali Sh. 64,000,000, bila hivyo hawakuruhusiwa kuwaoa.
Karume alikuwa ameanza
kuwa mwiba kwa Mwalimu Nyerere pia juu ya Muungano. Kwa mfano, alimkatalia
Nyerere kwa lugha ya dharau na kejeli juu ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na
Azimio la Arusha kutumika Zanzibar.
Na kuhusu akiba ya
fedha za kigeni ya Zanzibar iliyofikia dola milioni 80 mwaka 1972, alimuonya
asithubutu kuitolea macho, akamwambia: “Fedha ya kichwa cha Malkia si
yako na usiniulize, labda niulize juu ya hii (sh.) yenye picha ya kichwa
chako”.
Na kuhusu Muungano,
Karume alikuwa ameanza kuchoka nao. Siku moja alisema, “Muungano ni kama koti
tu; likikubana unalivua”.
Ufa huu kati ya
viongozi hao wawili juu ya Muungano, ndio uliosababisha kamati ya kupendekeza
Katiba (Constitutional Committee) isiundwe na Bunge la Katiba (Constitutional
assembly) lisiteuliwe ndani ya muda wa mwaka mmoja tangu Muungano, kama
ilivyotakiwa chini ya Mkataba wa Muungano wa Sheria ya Muungano ya 1964.
Wadadisi wa mambo ya
siasa wanakubaliana kuwa, kama Karume angeendelea kutawala miaka kadhaa baada
ya 1972, Muungano ungefikia kikomo kwa njia ya kutisha na kusikitisha.
Kufikia mwaka 1972,
upinzani kwa Serikali ya Karume ulikuwa umechukua harakati za uasi wa umma,
chini kwa chini kwa mara ya kwanza tangu Hanga na wenzake wanyongwe mwaka 1969.