HAI YASIMAMISHA VIONGOZI WA KIJIJI
Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga amewasimamisha uongozi mwenyekiti wa kijiji cha Kwasadala na ofisa mtendaji wake pamoja na afisa mtendaji wa kata ya Masama Kusini ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhilifu wa mali za kijiji pamoja na uuzaji holela wa maeneo ya wazi ya kijiji.
Mkuu huyo wa wilaya alifikia hatua hiyo katika mkutano wa hadhara wa kijiji hicho ambapo aliagiza viongozi hao kukaa pembeni kupisha uchunguzi huo ambao ametaka ufanyike katika kipindi cha wiki moja kuanzia jumatatu ijayo.
Ameeleza kuwa baada ya uchunguzi huo ambao utafanywa na timu ya wataalamu watano kutoka katika halmashauri ya wilaya ya Hai aliowataja kuwa ni pamoja na mwanasheria,mkaguzi wa ndani,afisa ardhi,afisa utumishi na afisa ugavi pamoja na katibu tawala wa wilaya ndipo utaitishwa mkutano wa dharura wa kijiji kufikia maamuzi.
Amesema kuwa matokeo ya uchunguzi huo yatatoa mwelekeo wa hatua za kuchukuwa kwa serikali watendaji wanaowasimamia huku wananchi wakiwa na uamuzi wa mwisho wa viongozi wao waliowaweka madarakani katika serikali ya kijiji.
Viongozi hao waliosimamishwa ni pamoja na mwenyekiti wa kijiji hicho Ernest Munisi na Mtendaji wake Clare Ramadhani pamoja na Ofisa mtendaji wa kata ambayo kijiji hicho kipo ya Masama kusini.
Katika mkutano huo wa kijiji,wananchi mbalimbali walitoa tuhuma dhidi ya mwenyekiti wa kijiji hicho Munisi ya kuuza kiholela maeneo ya ardhi na fedha kuzitumia kwa matumizi binafsi.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walijitokeza na kumtetea mwenyekiti huyo kwa madai ya kuleta maendeleo makubwa yakiwemo ya ujenzi wa shule ya msingi na sekondari ya Mkwassa pamoja na kudhibiti wimbi la ujambazi
Mwananchi wa kijiji hicho Judica Swai alidai mbele ya mkuu wa wilaya hiyo kwamba maeneo ya wazi ya kijiji hicho yakiwemo ya shule ya msingi ya Msamadi yamekuwa yakiuzwa kiholela na uongozi wa kijiji hicho na kila aliyejaribu kuhoji amekuwa akifanyiwa visa vikiwemo vya kufunguliwa kesi za kubambikiwa
Naye David Swai alihutuhumu uongozi wa kijiji hicho kuuza mizani ya kupimia mazao ya kijiji hicho pamoja na uongozi wa kijiji kwa zaidi ya miaka miwili sasa kushindwa kusoma taarifa za mapato na matumizi kutokana na kutofanyika kwa mikutano mikuu ya kijiji.
Wananchi hao pia walieleza kuwa maeneo ya ardhi ya kijiji hicho yamekuwa yakiuzwa bila ya kufahamika fedha zinaenda wapi pamoja na kutokuwepo kwa taarifa ya michango inayokusanywa kutoka kwa wananchi.
Wamedai mwenyekiti wa kijiji hicho amesababisha migogoro mikubwa ukiwemo baina ya kijiji na kanisa la kiinjili la kiluteri nchini(KKKT) kuhusiana na mvutano wa ardhi ambapo mgogoro huo kwa sasa upo mahakamani.
Wananchi hao pia wamedai mwenyekiti Munisi ambaye kabla ya kuingia katika wadhifa huo alikuwa askari polisi amekuwa akiwadhalilisha wananchi kwa kuwatukana matusi ya nguoni pale wanapotka kuhoji utendaji wake wa kazi.
Aidha wananchi hao walimtuhumu afisa mtendaji wa kijiji hicho Clare Ramadhani kuiba vocha themanini za pembejeo za kilimo katika msimu uliopita zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tano kwa madai ya kutengeneza mazingira mazuri ya kijiji kupendelewa na maofisa wa halmashauri.
Kufuati malalamiko hayo ndipo mkuu wa wilaya hiyo alimtaka mtendaji wa kijiji Clare Ramadhani kujibu malalamiko hayo ambapo mtendaji huyo alianza kwa kulalamika si kweli kwamba aliiba vocha za pembejeo na kumtuhumu mwenyekiti wake kuandaa mpango wa kumchafua.
Alidai kwamba kwa muda mrefu sasa hana mahusiano mazuri ya mwenyekiti wake na kumtuhumu kusababisha matatizo yote ya kijiji ya uendeshaji wa shughuli ikiwemo ya kumiliki nyaraka ikiwemo mihuri anayoitumia kuuza maeneo ya ardhi ya kijiji.
Naye mtendaji wa kata,Hassani Mwambashiu alikiri kutofanyika kwa vikao vya kisheria vya kijiji hicho kwa muda mrefu kutokana na malumbano yaliyokuwepo kijijini hapo kwa zaidi ya miaka mitatu na kufafanua kwama taarifa zote amekuwa akiziwasilisha katika halmashauri ya wilaya.
Hata hivyo akijitetea kutoka na tuhuma hizo,mwenyekiti wa kijiji hicho alidai kuwa madai hayo yamepangwa na wabaya wake ambao amekuwa akiwadhibiti kijijini hapo wakiwemo majambazi ambao wamekuwa wakijishughulisha na uporaji majumbani na mitaani.
Ameeleza kuwa suala la uuzaji wa maeneo ya ardhi halikuwa uamuzi binafsi bali wa uongozi wote wa kijiji hicho kutokana na wananchi kukaidi kutoa michango ya shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo za ujenzi wa choo cha shule ya msingi
Mkuu wa wilaya ya Hai,Makunga mbali ya kuwasimamisha viongozi hao aliwalaumu wajumbe wa halmashauri kuu ya kijiji kwa kukaa na malalamiko hao kwa muda mrefu bila ya kuchukua hatua zozote zile.
“Kijiji ni kama bunge na halmashauri ni kama serikali kwanini mnaacha hali hiyo katika kijiji chenu,nawe mtendaji wa kata unafahamu mtafaruku wa mwenyekiti na mtendaji wake lakini hauchukui hatua,kwa hali hiyo kweli tutafika?,”alihoji Makunga.
Makunga pia aliwataka wanakijiji hao kutambua wajibu wao wa kusimamia kijiji chao kwa kuhakikisha wanatumia haki yao ya msingi ya kusimamia uwajibikaji wa kila siku ya viongozi na kutumia sheria na tararyibu kulazimisha ufanyikaji wa mikutano ya kijiji kila baada ya miezi mitatu
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia