WAKAZI wa Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara ambao nyumba zao zilizopo pembeni ya barabara ya Kia-Mirerani zimewekwa alama ya X na wakala wa barabara nchini (Tanroads) mkoani humo wameazimia kuifikisha Serikali Mahakamani kutokana na kutowafahamisha namna ya kuwalipa fidia hasa wakati huu barabara hiyo inapotarajiwa kujengwa.

Katika kuunga mkono suala hilo watu 77 kati ya 97 waliohudhuria kikao hicho walichanga sh1.5 milioni kwa ajili ya kuwasilisha kisheria suala hilo kupitia kwa wakili wao ambapo gharna ya awali imebainika kuwa ni sh800,000.

Akizungumza jana kwenye ukumbi wa hoteli ya Kangaroo mjini humo Mwenyekiti wa kamati ya watu waliowekewa alama ya X kwenye mali zao Nobert Olomi alisema wakili wao anatarajia kuandika barua ya kusudio la kuishtaki Serikali kupitia halmashauri ya wilay aya Simanjiro na Tanroads Manyara.

Olomi alisema hawapingi maendeleo ya ujenzi wa barabara ila wanachopinga ni kutobainishwa haki zao za msingi kwani barabara hiyo imepandishwa hadhi na kuwa ya wilaya na mkoa wakati wao walishajenga hivyo barabara hiyo imewakuta wao.

Alisema Serikali kupitia mkuu wa mkoa huo Elaston Mbwilo na Meneja wa Tanroads mkoa huo Yohani Kasaini walipokuta nao Septemba mwaka jana walipewa mapendekezo matatu ambayo bado hayajatekelezwa hadi sasa.

“Walipendekeza kuwa watatulipa fidia au kuangalia uwezekano wa barabara kupita nje ya mji au barabara hiyo kutenganezwa bila kubomoa mali yoyote lakini hadi sasa hakuna jibu na sisi hatuwezi kukaa kimya,” alisema Olomi.  

Alisema kila barua waliyoandika walisisitiza kupatiwa majibu kwa njia ya maandishi lakini hawakupatiwa majibu yoyote na zaidi mbunge wa Jimbo hilo Christopher Ole Sendeka ambaye walitarajia angewatetea amekaa kimya bila kuwasemea chochote.

Naye,Mwenyekiti wa mtaa wa Songambele A,Ombeni Charles alisema alimsikia Meneja wa Tanroads mkoa wa Manyara Yohane Kasaini akisema watalipa fidia kuanzia mita 15 kutoka barabarani na kuacha mita 7.5 zilipwe na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro.

“Serikali inatakiwa kulichukulia jambo hili kwa umakini mkubwa na isilifanye suala la kisiasa kwani watu wanadai haki zao na wanatakiwa kupatiwa haki hiyo kwani barabara ndiyo imewakuta,wao hawakujenga barabarani,” alisema Charles.

Kwa upande wake,mmoja kati ya waathirika wa tatizo hilo John Ninie alisema nyumba zao zimewekewa alama ya X bila wao kupewa taarifa wala kushirikishwa na wataweka wakili ili wapate haki zao.

“Hatuwezi kukubali hali hii ni bora twende kwenye vyombo vya sheria ili tujue kuwa tunapata haki zetu au tunakosa kuliko kusubiri na kukaa mali zetu zibomolewe huku tunaangalia,” alisema Ninie.