BREAKING NEWS

Sunday, September 16, 2012

WATATU KUWANIA NAFASI YA NAIBU MWENDESHA MASHITAKA ICC,MAHAKAMA YA RUFAA ICTR KUWA NA VIKAO VIWILI OKTOBA

Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Fatou Bensouda, wiki hii emetoa majina ya watu watatu watakaogombea nafasi ya Naibu Mwendesha Mashitaka huku Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) imetangaza kuwepo kwa vikao viwili mwezi Oktoba.
ICC
Majina ya wagombea nafasi ya Naibu Mwendesha Mashitaka yatajwa: Mwendesha mashitaka wa ICC, Fatou Bensouda Jumatano aliwasilisha majina ya watu watatu watakaowania nafasi ya Naibu Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo. Wagombea hao ni pamoja na Raija Toiviainen wa Finland, Paul Rutledge kutoka Australia na James Stewart wa Canada. Majina hayo yamechunjwa kutoka wagombea 126 waliomba nafasi hiyo. Naibu Mwendesha Mashitaka atachaguliwa na nchi wanachama 121 wanaounda mahakama hiyo  katika kikao chao cha 11 kinachotarajiwa kufanyika mjini The Hague, Uholanzi kati ya Novemba 14 na 22.
DRC
Wapigania haki za binadamu washutumu waasi wa DRC kwa uhalifu wa kivita: Kikundi cha Wapigania Haki za Binadamu cha Human Right Watch (HRW) kimelishutumu kundi la waasi la M23 kwa kufanya uhalifu wa kivita wa kutisha Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ikiwa ni pamoja na ubakaji na mauaji.Katika ripoti iliyotolewa Jumanne na HRW ilifafanua kwamba miongoni mwa watu waliouawa, 33 walikuwa vijana na watoto waliokuwa wanajaribu kulikwepa kundi hilo la waasi ambapo wengine 15 waliuawa katika maeneo yanadhibitiwa na waasi hao.Wapiganaji hao pia wanadaiwa kuwabaka wanawake na wasichana 46. Kundi hilo la Haki za binadamu limetoa wito wa kuwajibishwa kwa makamanda wa M23 na maafisa wa Rwanda ambao wanadaiwa kuliunga mkono kundi hilo, kwa kuwafikisha kwenye mkondo wa sheria.      
ICTR
Mahakama ya Rufaa kusikiliza kesi mbili Oktoba: Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa itakuwa na vikao viwili mwezi ujao. Mahakama hiyo Oktoba 8 itasikiliza kesi ya rufaa inayowahusu mawaziri wawili wa zamani wa Rwanda, Justin Mugenzi na Prosper Mugiraneza ambao wote wawili wanapinga adhabu ya vifungo vya miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari na uchochezi. Siku itakayofuata, Oktoba 9, majaji watatoa hukumu ya kesi ya rufaa ya Mkurugenzi wa zamani wa Wizara ya Wanawake na Masuala ya Familia, Jean-Baptiste Gatete, ambaye katika mahakama ya awali alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu.
WIKI IJAYO
ICC
Kesi ya Bemba kuendelea kuunguruma Jumatatu: Kesi ya utetezi inayomkabili kiongozi wa zamani wa kundi la waasi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (MLC), Jean Pierre Bemba inatarajiwa kuendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo, Septemba 17, mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).Bemba anakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa kati ya mwaka 2002 na 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.   
RWANDA  
Mugesera mahakamani wiki ijayo: Msomi mmoja wa Rwanda Leon Mugesera anatarajiwa kupanda kizimbani tena Jumatatu ijayo, Septemba 17, nchini Rwanda mbele ya Mahakama Kuu ambako kesi yake inatarajiwa kuanza kusikilizwa. Mugesera anashitakiwa kwa kuchochea mauaji ya kimbari mwaka 1992 kupitia hotuba yake ya uchochezi aliyoitoa kwa lugha ya Kinyarwanda katika mkutano wa chama chake cha siasa, Kaskazini mwa Rwanda.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates