MGOGORO mkubwa unafukuta kwenye Jumuiya ya
Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Kata ya Mirerani Wila ya Simanjiro Mkoani
Manyara baina ya Katibu wa jumuiya hiyo Sophia Idd na baadhi ya wanachama wake
zaidi ya 64.
Wanachama hao wanamtuhumu Katibu huyo Sophia
kwa uroho wa madaraka kwa kuficha na kugoma kutoa fomu za uchaguzi wa nafasi
hiyo na wanamtuhumu alishindwa uchaguzi kwa kupigiwa kura za hapana hadi kusababisha
apigiwe kura na mwanaume.
Wakizungumza baada ya kufanyika kikao cha
mkutano mkuu wa UWT wa kata hiyo uliolenga kupiga kura ya kutokuwa na imani na
katibu huyo walisema Sophia aliwatukana baada ya kutompigia kura ya ndiyo
kwenye uchaguzi uliopita.
“Yule alikuwa anaficha fomu za uchaguzi
nyumbani kwake na pia alipigiwa kura saba za hapana kati ya wanawake 14 ndipo
mwanaume aitwaye Kimolo naye akampiga kura,” walisema wanachama hao waligoma
kutaja majina yao.
Walisema katibu huyo ameingia kwenye nafasi
hiyo bila utashi wao na pia kwa muda mfupi aliochaguliwa amekuwa akitoa lugha
ya matusi na kuwadhalilisha hivyo wanatarajia kuhamia chama cha upinzani cha
Chadema ili kumkomesha.
“Walisema ni bora kuhamia Chadema kuliko
kuendelea kuwa kwenye chama ambacho kinawanyanyasa na kumlinda mtu mmoja
aliyejilimbikizia madaraka wakati uwezo wake ni mdogo katika kuitumikia CCM,”
walisema wanawake hao.
Hata hivyo,Sophia amekanusha vikali madai hayo
akisema kuwa hayo ni majungu ya makundi ya kisiasa kwenye kata hiyo kwani
migogoro na matatizo yao yote waliyamaliza kwenye kikao kilichofanyika juzi.
“Mimi sikumtukana mtu na wala sikuficha fomu
za kugombea uchaguzi nilikuwa nazijaza ofisini siyo nyumbani na wanaosema
nilipigiwa kura na mwanaume waambie waseme wenyewe kwani mimi nilishinda
kihalali,” alisema.