BREAKING NEWS

Friday, September 14, 2012

KATIBU UVCCM SIMANJIRO AGIZWA AKAMATWE

MKUTANO Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara umeagiza aliyekuwa Katibu wa UVCCM wa wilaya hiyo Alhaji Omari Kariati anayetuhumiwa kujufa zaidi ya sh26 milioni za umoja huo akamatwe na kufikishwa Mahakamani.

Tamko hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Mkutano mkuu wa umoja huo uliofanyika mji mdogo wa Mirerani baada ya wajumbe hao kutaka kujua hatua iliyochukuliwa kwa Kariati ambaye sasa ni Diwani wa (CCM) kata ya Kwadelo wilayani Kondoa mkoani Dodoma.

Sakata la Kariati limechukua muda mrefu hivi sasa hadi vijana hao kudai kuwa Alhaji Kariati amekuwa analindwa na kigogo mmoja aliyepo Ikulu hivyo kukwamisha upatikanaji wa fedha zao.

Akizungumza kwenye kikao hicho,Abdalah Nangu alihoji ufujaji wa fedha zao zaidi ya sh26 milioni za mradi wa gari la abiria zilizokusanywa Mei 9 mwaka 2010 katika harambee iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar Shamsi Vuai Nahodha.

Nangu alisema hawakubali mtu mmoja afuje fedha zao na kwenda kugombea udiwani kijijini kwao bila kuchukuliwa hatua yoyote kwa hofu ya kulindwa na kigogo hivyo Kariati achukuliwe hatua ikiwemo kupelekwa Mahakamani.

Ngayaila Samweli alisema Ahaji Kariati alichukua fedha hizo na kwenda nazo Kondoa kugombea udiwani na akashinda lakini anaogopwa kuchukuliwa hatua wakati alichukua fedha zilizochangwa na viongozi wakubwa.

“Hili siyo shamba la bibi kila mtu aje ajichumie fedha na kuondoka bila kuchukuliwa hatua yoyote ile mtu yupo hapa Kondoa tunashindwa kumchukulia hatua jamani akamatwe na apelekwe Mahakamani,” alisema Samweli.

Kwa upande wake,Jackline Momo alitoa wito kwa Waziri mmoja jina tunalihifadhi kutowashinikiza askari polisi kumlinda Alhaji Kariati pindi alipokamatwa wilayani Kondoa ili akashtakiwe wilayani Simanjiro.

“Alhaji Kariati alikamatwa wilayani Kondoa ili aletwe huku lakini Waziri mmoja alipiga simu na kudai kuwa siasa chafu za Simanjiro ndizo zinazosumbua hivyo aachiwe na kisha akaachiwa bila kuchukuliwa hatua yoyote,” alisema Momo.

Katibu wa CCM wa wilaya ya Simanjiro Jamila Mujungu aliwataka vijana hao kuendelea kusimama kidete kwenye kudai haki yao na wao wapo nyuma yao katika kuhakikisha kuwa fedha zao zinarudishwa.

“Hili suala la kusema kuwa wilaya ya Simanjiro kuna siasa chafu siyo jambo jema kwani wakati anachukua fedha za vijana hiyo hali ya hewa ya kisiasa ilikuwa safi awarudishie fedha zenu,” alisema Mujungu.

Mwenyekiti wa UVCCM wilayani Simanjiro,Kiria Laizer alisema yeye hakunywa hata soda kwenye fedha hizo hivyo asihusishwe kabisa na ufujaji wa fedha hizo uliofanywa na aliyekuwa Katibu wa UVCCM wa wilaya hiyo Alhaji Kariati.

“Vijana wenzangu tupo pamoja katika kuhakikisha kuwa tunapata fedha zetu na tutamkamata Kariati ili azirudishe kwani nilimkabidhi fedha hizo akazifungulie akaunti benki lakini hakufanya hivyo,” alisema Laizer. 

Hata hivyo,Alhaji Kariati hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya mkononi ila amewahi kuripotiwa na gazeti hili la Mwananchi akisema kuwa fedha hizo zipo na anasubiri hali ya hewa ya kisiasa itulie wilayani Simanjiro ili azikabidhi.

“Hizo fedha zipo na wala hakuna wasiwasi wowote ule wa kupatikana kwake ila nasubiri hali ya hewa ya kisiasa itulie wilayani Simanjiro ili niweze kukabidhi fedha hizo kwa Katibu wa UVCCM aliyepo Simanjiro,” alinukuliwa alhaji Kariati.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates