JESHI la polisi mkoa wa Arusha,limewatia mbaroni wafanyabiashara
wawili katika eneo la mto Nduruma wilayani
Arumeru ,kwa kosa la kuwakuta na noti bandia zenye thamani ya shilingi milioni
18 zote zikiwa noti za shilingi 10,000.
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha,Liberatus Sabasi
alisema kuwa tukio hilo,limetokea jana majira ya saa 8 mchana katika eneo hilo
baada ya polisi kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema na kuandaa mtego uliofanikiwa kuwanasa wakielekea mjini Moshi.
Sabas aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kamran Ahmed (30)mkazi
wa kaloleni na Nick Joseph mkazi waKijenge Mwanama katika jiji la Arusha, ambapo
watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa kwenye gari dogo aina ya Maark II lenye namba za usajiri T 512 BVG,
wakielekea mjini Moshi kuzifanyia biashara.
Alisema polisi baada ya kuwakamata na kuwafanyia upekuzi
walikuta boksi dogo la simu za mezani likiwa limewekwa chini ya kiti cha dereva
na baada ya kulifungua walikuta jumla ya noti 1,800 za shilingi elfu 10 zikiwa
zimefungwa na mpira.
Watuhumiwa hao bado wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa
mahakamani baada ya upelelezi wa polisi kukamilika.
Wakati huo huo; Bweni la shule ya sekondari Manyara,iliyopo
Mto wa Mbu,wilayani Monduli linalotumiwa na wanafunzi 148 limeteketea kwa moto
na kuteketeza malizote za wanafunzi zilichokuwa
ndani ya bweni hilo.
Kamanda Sabasi alisema kuwa tukio hilo limetokea jana
majira ya saa 2 usiku wakati wanafunzi hao wakijisomea darasani na kwamba
chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na polisi wameanza uchunguzi wa tukio
hilo pamoja na thamani ya vitu vilivyoteketea.