MAMILIONI YA NYUMBU KUHAMA KUTOKA KUSINI KUELEKEA KASKAZINI

TUKIO la mamilioni ya nyumbu kuhama kwa makundi kutoka kusini mwa
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hadi kaskazini mwa Hifadhi ya Masai
Mara, Kenya na baadaye kurejea nyumbani Tanzania ni la pekee duniani
na huvuta maelfu ya watalii kutoka Marekani, Ulaya na Asia.
Akizungumzia tukio la kuhama kwa nyumbu hao, Meneja Uhusiano wa
Shirika la Hifadhi za Taifa, (TANAPA), Pascal Shelutete, alisema tukio
hilo linawavuta watalii wa ndani lakini hasa kutoka nje kuja
kuangalia.
“Hili tukio sio la kawaida na tunataka kuwahamasisha Watanzania na
watalii kutoka nje waje kwa wingi kujionea majaabu haya,” alisema.
Alisema makazi ya nyumbu hao ni Serengeti lakini wanaenda Masai Mara
kwa mapumziko ya muda mfupi tu na kurejea tena nyumbani ambako wanakaa
takribani miezi 10 au 11 hivi.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),
Geoffrey Tengeneza, alisema tukio hilo ndilo lililoifanya Serengeti
kuingizwa kwenye Shindano la Maajabu Saba ya Afrika.
“Ingawa yapo matukio mengine ya wanyama kuhama kutoka sehemu moja na
kwenda sehemu nyingine, lakini tukio hili hulipati hulipati eneo
lolote duniani isipokuwa hapa Tanzania.
“Ndio maana kumekuwa na shindano la Maajabu Saba ya Afrika na Tanzania
tuna maeneo matatu yaliyoingizwa kwenye shindano hilo ambalo
linaendelea,” alisema.
Aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili  Bonde la
Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na tukio la nyumbu kuhama kwa mamilioni
kutoka sehemu moja hadi nyingine na kurudi katika Hifadhi ya Serengeti
yote kwa pamoja yaweze kushinda.
Alisema katika mashindano hayo yapo maeneo 12 yanayopigiwa kura ambapo
kwa Tanzania imeweza kuingiza maeneo matatu.
Alisema zoezi la kupiga kura lilianza mwezi mmoja uliopita na litadumu
hadi Desemba mwaka huu, hivyo akawataka Watanzania kupiga kura kwa
wingi ili kivuto hicho kiweze kushinda.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post