SHIRIKA la kidini linaloshughulika na watoto la Compasion
hapa nchini limezindua miradi mikubwa ya maji yenye thamani ya zaidi ya
shilingi milioni 600 katika vituo 7 katika jijini Arusha, itakayo wanufaisha wananchi zaidi ya 200,000
waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi ya kunywa.
Uzinduzi huo ulifanywa na kaimu katibu tawala wa wilaya ya
Arusha,Yacobo Shayo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha,Magessa Mulongo mwishoni
mwa wiki katika maeneo tofauti ya Olmatejoo,Kambi ya Fisi na Unga limited jijini hapa.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa nchi wa shirika hilo la compassion
nchini,Joseph Mayalla alisema kuwa uzinduzi huo ni mwendelezo wa mkakati wa
shirika hilo katika kuwasogezea huduma mbalimbali wananchi ,ambapo katika mikoa
12 linayohudumiwa na Compasion hapa nchini mikoa miwili ya Morogoro na Singida imenufaika
na mpango wa uzinduzi wa miradi ya Maji.
Alisema kuwa shirika hilo limefanikiwa kuzindua miradi
hiyo kwa kushirikiana na washirika wake ambao ni makanisa mbalimbali ya kipentekoste ya jijini hapa,na
kwamba miradi hiyo itakuwa chini ya vituo vya kulelea watoto wasio na uwezo vilivyo chini ya makanisa hayo
.
Alifafanua kuwa miradi hiyo imezinduliwa katika vituo
vya,Pefa katika kanisa la Pentekoste lililopo Olmatejoo, kanisa la Jerusalem Baptist
lililopo kambi ya fisi,kanisa la P.AG na kanisa la Free Pentecostal(FPCT)yaliyopo
eneo la Unga limited na kanisa la Elim pentecoste lililopo kata ya daraja
mbili.
Alisema kuwa katika miradi hiyo kituo cha kanisa la Free
Pentecost Unga Limited ,kulizinduliwa
miradi mitatu ikiwemo jengo la watoto lenye gorofa tatu litakalotumika kama shule ya kufundishia watoto wanaolelewa
kwenye vituo hivyo,ofisi pamoja na huduma zingine,kituo cha maji na Jenereta
kubwa la umeme vyote kwa pamoja vimegharimu zaidi ya sh,milioni 200.
Mayala aliongeza kuwa shirika lake litaendelea kutoa
huduma kwan jamii kupitia makanisa katika kuibua miradi na kuisogeza kwa
wananchi na kwamba litaendelea kujikita zaidi kwenye miundo mbinu,Maji,usafi na
Afya.
Alisema shirika hilo ambalo lilianza kutoa huduma hapa nchini
mwaka 1999, kwa sasa linahudumia watoto zaidi ya 65,900 hapa nchini katika
mikoa 12 linayoihudumia na matarajio ni
kuifikia mikoa yote hapa nchini.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo mgeni rasimu katika
miradi hiyo,Yacob Shayo alitoa wito kwa makanisa hayo kutochoka kutoa huduma
kwa jamii kwani yamekuwa na mchango mkubwa sana katika kudumisha amani na malezi bora ya makuzi ya watoto.
Shayo aliwataka wananchi kuitunza miradi hiyo ili iweze
kudumu na kuvinufaisha pia vizazi vijavyo ,wawe tayari kujitolea na kutoa wito
kwa watu wasio taka maendeleo ama kufanya kazi waadhibiwe kwa kuchapwa viboko.