MWALIMU MKUU WA SEKONDARI ILBORU ASIMAMISHWA KAZI



SERIKALI imemsimamisha kazi, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya
Ilboru, Jovinus Mutabuzi, kufuatia madai ya tuhuma mbalimbali za fedha
na matumizi mabaya ya madaraka yaliyosababisha wanafunzi  kuandamana
hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakishinikiza ang’olewe kutokana na tuhuma
ulaji fedha na matumizi mabaya ya madaraka.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, anayeshughulikia Elimu, Kasimu Majaliwa, alitangaza uamuzi huo
jana  baada ya kusikiliza madai ya wanafunzi katika mkutano wa hadhara
uliofanyika shuleni hapo.

Pamoja na kusimamishwa kazi, Naibu Waziri Majaliwa, amemteua Mwalimu
Mkuu Msaidizi wa shule hiyo ya wanafunzi wenye vipaji maalum, iliyopo
wilayani Arumeru, mkoani Arusha, Lorna Nteles, kukaimu nafasi ya
Mwalimu Mkuu.

Katika hatua nyingine, Majaliwa, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Arusha, Halfa Hida, kuteua mkaguzi wa ndani kufanya
uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili Mutabuzi, ikiwemo ya kutumia
stakabadhi bandia anazodaiwa kuhalalisha malipo ya wanafunzi.

Katika mkutano wake wa hadhara na wanafunzi hao, Majaliwa, alibaini
kuwa hoja zao ikiwemo ya matumizi mabaya ya fedha kiasi cha Sh.
milioni 800 kuziingiza kwenye Chama cha Kuweka na Kukopa (SACCOS)
ambapo alikuwa akizikopesha kwa riba kwa walimu na watumishi wa shule
hiyo.

Jumatatu wiki hii, wanafunzi wa shule hiyo waliandamana hadi ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, kwa lengo la kushinikiza
kung’olewa kwa mkuu huyo, ambapo pamoja na mambo mengine walidai kuwa
ameshiriki kuifanya shule hiyo kudorora kitaaluma na kuwadhalilisha
wanafunzi kwa kuwaita mashoga.

 










Mkuu wa Mkoa Magesa aliwasihi wanafunzi hao kurejea shuleni na
kuendelea na masomo wakati suala lao likishughulikiwa, hata hivyo,
baaada ya kurudi shuleni walianzaisha mgomo wa kutoingia darasani
ikiwemo kutokula chakula cha shule hiyo.

Hatua  hiyo,  ilimlazimu Naibu Waziri, kufika shuleni hapo na
kuwasikiliza wanafunzi hao, ambapo kabla ya kufanya mkutano
alitembelea maeneo yote yanayolalamikiwa na wanafunzi hao ikiwemo,
jiko la chakula, mabweni pamoja na choo cha matundu mawili kinachodai
kujengwa kwa Sh. milioni 25.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara shuleni hapo, Majaliwa aliwasihi
wanafunzi hao kutovunja sheria kwa kuitisha migomo na maandamano
yasiyo rasmi huku akimtaka makamu wa shule hiyo kusimamia nidhamu kwa
wanafunzi hao.

Naibu waziri akiwa ameandamana na askari wa kikosi cha  kutuliza
ghasia waliokuwa na mabomu na silaha za moto, alilazimika kutumia saa
zaidi ya tano kutoa ufafanuzi wa madai ya wanafunzi hao ambao muda
wote walionyesha kumsikiliza kwa makini huku hoja yao kubwa wakidai
hawamtaki mkuu huyo.


Hata hivyo,  Mjaliwa alikerwa na mabango aliyoyakuta yamebandikwa
kwenye kuta katika majengo yote ya shule yakiwa na ujumbe mbalimbali
wa kumpinga Mwalimu Mutabuzi huku baadhi yake yakiwa yamechorwa
vikaragosi vinavyomfananisha utawala wa  mkuu huyo na ule wa marehemu
Nduli Idd Amini dada wa Uganda.

Pamoja na kuwasihi kuwa wawe wavumilivu wakati hatua zaidi
zikichukuliwa lakini walipaza sauti wakidai kuwa hawapo tayari kuingia
darasani bila kuondolewa kwa mkuu wao hali iliyomlazimu Naibu Waziri
kutamka kuwa amemsimamisha kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo, hali
iliyoamsha shangwe na nderemo kwa wanafunzi hao.

Naibu waziri amepiga marufuku michango isiyo na tija mashuleni,
matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi, adhabu za malipo ya fedha,
matumizi ya M-Pesa mashuleni pamoja na kuziagiza bodi za shule kutatua
matatizo ya wanafunzi pale yanapoibuka kabla ya kuleta madhara

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post