MKUTANO Mkuu
wa jumuiya ya Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wilaya ya Monduli
jana walikataa kupigia kura nafasi ya uenyekiti baada ya mgombea waliyemtaka
kukatwa jina.
Uamuzi wa
kugoma kupiga kura ulilenga kupinga maamuzi ya kamati ya siasa mkoa wa Arusha
inayodaiwa kukata jina la Diwani Kimay anayeaminika kuungwa mkono na vijana
wengi wa Monduli na kurejesha majina mawili ya Dominic Ole Lenga na Mbayani
Tayay.
Wajumbe
zaidi ya 285 waliohudhuria mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha
Maendeleo ya Jamii (CDTI), mjini Monduli kwa kauli moja waliazimia kuendelea
kupigia kura nafasi zingine na kutishia kutoka nje kususia kikao iwapo
watalazimishwa kupiga kura za uenyekiti.
Lewanga
Kipuyo ndiye alikuwa mjumbe wa kwanza kutoa hoja ya kugomea kura ya uenyekiti
mara baada ya uongozi wa zamani chini ya Julius Kalanga kujiuzulu kwa kusema
hawataki kumchagua kiongozi wasiyemtaka ambaye watamsusia mara baada ya kuingia
madarakani.
“Sisi vijana
wa Monduli kwa pamoja tumekubaliana kutopiga kura kwenye nafasi ya uenyekiti
kupinga mgombea tuliyemtaka kuondolewa kwa hila,” alisema Kipuyo
Mjumbe
mwingine Michael Laizer yeye alikwenda mbali kwa kukituhumu kamati ya siasa ya
mkoa wa Arusha kuwa imekosa sifa ya kuendelea kuwepo na kupendekeza ijiuzulu
kwa kuvujisha siri za vikao hata kabla ya taarifa kufikishwa kwa wahusika.
Msimamizi
msaidizi wa uchaguzi huo, Ally Rajabu alilazimika kutoka nje ya ukumbi
kuwasiliana na uongozi wa juu wa UVCCM taifa kwa maelekezo ambapo aliporejea ukumbini alitangaza
kukubaliana na hoja ya wajumbe ya kutopigia kura nafasi ya uenyekiti akisema
ndivyo alivyoelekezwa na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigella.
“Wenye
maamuzi nini kifanyike ndani ya UVCCM Monduli ni wajumbe wa mkutano mkuu wa
wilaya ambao ndio ninyi, mtakachoamua ndicho kitakachofanyika.
Kutokana na hali
halisi inayojionyesha ndani ya ukumbi huu, natangaza kuwa nafasi ya uenyekiti
haitapigiwa kura hadi itakapotangazwa baadaye na watu kujitokeza kuomba upya,”
alitangaza Rajabu na kushangiliwa kwa nguvu.
Wakazungumza
nje ya ukumbi muda mfupi baada ya uamuzi wa kutopigiwa kura kutolewa, waliokuwa
wagombea wa nafasi ya uenyekiti, Dominic Ole Lenga na mwenzake Mbayani Tayay
walisema wanakusudia kutoa msimamo wao baada ya kutafakari.
“Haya ni
moja ya gharama za demokrasia, wengi pale ukumbini wamepiga kura kuunga mkono
hoja ya nafasi ya uenyekiti kutopigiwa kura. Hilo ndilo ninaloweza kusema kwa
sasa, mengi nitaongea baadaye,” alisema Ole Lenga
Kwa upande
wake, Tayay licha ya kukubaliana na uamuzi huo, lakini alisema anaamini
umetokana na ushawishi wa kundi la watu alioahidi kuwataja kwenye vikao aliodai
waliendesha kampeni za kukwamisha uchaguzi huo usiku wa kuamkia jana.
“Siku zote
nimesikia tu kutoka kwa watu wengine kuwa haki inaweza kununuliwa kwa
ushawishi, leo nimeshuhudia kwa macho yangu mwenyewe. Kifupi haki
haikutendeka,” alisema Tayay
Awali,
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Julius kalanga aliwataka vijana wa Monduli
kuchagua viongozi wanaowaamini watakaoongoza kwa kujibu mahitaji yao na kamwe
wasikubali kunyang’anywa haki ya kujichagulia viongozi wao na mtu au kundi la
watu.