WANAFUNZI wanaohitimu
masomo yao nchini wametakiwa kuepukana na tabia ya kudanganyika kuiba
mitihani kwani kwa kufanya hivyo ni kujipotezea malengo yao ya baadaye.
Hayo yalisemwa jana na Meneja wa shule ya sekondari Enaboishu,Loiruk Ritti ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 44 ya kidato cha nne ambapo jumla ya wanafunzi 155 walihitimu masomo yao shuleni hapo.
Ritti
alisema kuwa, katika shule nyingi nchini kumekuwepo na wizi mkubwa sana
wa mitihani unaofanywa na waalimu kwa kushirikiana na wazazi wa
wanafunzi hali ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi
kutofikia malengo yao kutokana na kutokuwa na mwanya wa kufikiria.
Alisema kuwa,swala la wanafunzi kupewa majibu ya mitihani limekuwa likiendelea kufanyika kwa siri katika
maeneo mbalimbali nchini ,hivyo aliwataka wanafunzi hao kutobweteka na
hali hiyo badala yake wajipange kikamilifu katika kufanya mitihani yao
na kutokutegemea kupewa majibu.
Aidha Ritti aliongeza kuwa, pamoja na kuwa wanafunzi hao wamekuwa wakiiba majibu ya mitihani
na wakati mwingine kutoshikwa na wahusika lakini baadaye kunakuwepo na
madhara makubwa sana kwani wengi wao wakifika kidato cha tano na sita
wamekuwa waksihindwa kumudu masomo na wengine kuishia kufeli kutokana na
kuzoeshwa kupewa majibu mara kwa mara.
‘Wanafunzi
ninachowaomba ombeni Mungu na someni sana kwa ajili ya kujiandaa na
mitihani yenu na mtafanya vizuri lakini swala la kusubiri kupewa majibu
ni hasara kubwa sana kwani huko mbeleni utashindwa kuendelea na masomo
kutokana na kutokuwa na uelewa na masomo hayo kutokana na ulivyo zoea
hapo awali’alisema Ritti.
Aidha
aliwataka walimu kutowafanya wanafunzi kukariri majibu badala yake
wawaandae wanafunzi hao ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao
ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kusoma kwa bidii badala ya
kuwafanya wabweteke na baadaye kupata madhara makubwa.
Naye
Mkuu wa shule hiyo, Lession Sakinoy alisema kuwa,shule hiyo wana
matarajio mbalimbali ikiwemo ya kupanua maktaba ya shule na maabara
ambayo itakagharimu kiasi cha shs 12.5 na wanajipanga katika kuhakikisha
wamepata fedha hizo ili kuweza kufanikisha swala hilo.
Aidha
alisema kuwa wana matarajio ya kununua gari la shule kwa ajili ya
kuwasaidia wanafunzi wanotoka maeneo ya mbali kuwahi masomo yao ambapo
jumla ya shs 30 milioni zitahitajika kwa ajili ya kununua gari hilo la
shule.
Alitaja changamoto zinazowakabili kuwa kuwepo kwa idadi ndogo ya kompyuta ambapo kwa sasa kuna kompyuta 25 tu ambazo hazitoshelezi kulingana na idadi ya wanafunzi walivyo
wengi , hivyo wana mpango wa kufanya harambee kwa ajili ya kuchangia
kompyuta ambapo shule hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwemo upungufu wa vitabu katika maktaba ya shule, wanafunzi kutofika
shuleni kwa wakati pindi shule inapofunguliwa wakiwa wanasubiri ada ya
shule inayosababisha wanafunzi hao kushuka kitaaluma.
Aidha
litaja changamoto nyingine kuwa ni wazazi wengi kuchelewa kuwalipia ada
watoto wao kwa wakati hali ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa
kukwama kwa maendeleo mbalimbali shuleni hapo kwani fedha hizo ndizo
zinategemewa katika kuiendesha shule hiyo