Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR)
imehitimisha majadiliano na Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na
Watu (ACHPR) ili kusimamia usikilizaji wa kesi za mauaji ya kimbari
zinazopelekwa kusikilizwa nchini Rwanda.
‘’Hali
iliyopo sasa ni kwamba ICTR kupitia ofisi ya Msajili imeshahitimisha
majadiliano na ACHPR kusimamia usikilizaji wa kesi,’’ Msemaji wa
Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa, Roland Amossouga aliliambia Shirika
la Habari la Hirondelle Jumanne.
Aliongeza
kwamba,’’Hati ya makubaliano hayo itatiwa saini hivi karibuni na baada
ya hapo ACHPR ndipo itaanza rasmi kazi yake ya kusimamia kesi ya (Jean)
Uwinkindi nchini Rwanda.’’
Wafanyakazi
wawili wa ICTR waliteuliwa Aprili mwaka huu kama wasimamizi wa muda wa
kesi ya Uwinkindi, huku ACHPR ikisubiriwa kukamilisha makubaliano na
ICTR kufanya kazi hiyo. ACHPR ina majukumu ya kulinda na kukuza haki za
binadamu ikiwa ni miongoni mwa kazi zake.
Wakati
ukitolewa uamuzi wa kuhamishia kesi ya Uwinkindi kwenda Rwanda Juni
2011, Majaji walimwelekeza Msajili wa Mahakama ICTR kuingia katika
mkataba wa maandishi na ACHPR ambao utaeleza wazi maslahi, fedha
zinazohitajika na mambo mengine muhimu ambayo yatafanya taasisi hiyo
kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kwa
mujibu wa majaji ‘’ACHPR itatakiwa kuwasilisha ripoti ya mara kwa mara
kila baada ya miezi mitatu juu ya hali ya mwenendo wa kesi kwa Rais wa
ICTR kupitia kwa Msajili wake, wakati kesi itakapoanza kusikilizwa hadi
hapo itakapohitimishwa ikiwa ni pamoja na hatua ya rufaa kwa mshitakiwa
na pia katika hatua ya kusimamia adhabu itakayotolewa, kama itakuwepo.’’
Majaji
waliridhika kuwa hatua ya Kamisheni hiyo kusimamia mwendendo mzima wa
kesi utatoa hakikisho kwamba ukiukwaji wowote wa haki ya mshitakiwa
katika mwenendo wa kesi yake utapelekwa mbele ya Rais wa ICTR mara moja
ili hatua za kurekebisha zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kufikiria
kuiondoa kesi hiyo kusikilizwa mbele ya mahakama za Rwanda.
ICTR
tayari imeridhia kesi nane kwenda kusikilizwa nchini Rwanda. Uwinkindi,
ambaye ni mchungaji alihamishiwa nchini Rwanda Aprili 19, 2012, akiwa
ni mshitakiwa wa kwanza wa ICTR kesi yake kwenda kusikilizwa nchini
humo.
Nje
ya Uwinkindi, kesi nyingine zilizohamishiwa nchini Rwanda ni pomoja na
mtuhumiwa ambaye bado anashikiliwa na ICTR na kiongozi wa zamani wa
wanamgambo wa Interahamwe, watuhumiwa sita ambao bado wanasakwa,
wakiwemo mameya watatu, polisi mmoja, afisa wa zamani wa jeshi na meneja
mmoja wa mgahawa. Hata hivyo kesi nyingine mbili bado zipo mbele ya
Mahakama ya Rufaa zikisubiri uamuzi.