VIONGOZI WAWAHUDUMIA WANANCHI MAJUMBANI KWA KWA ZAIDI YA MIAKA 10 KWA KUKOSA OFISI.

Imeelezwa kwamba kijiji cha Kipok kilichoko katika kata ya Moita Wilayani Monduli hakina ofisi ya serikali ya kijiji kwa zaidi ya miaka 10, huku uongozi wa kijiji hicho ukionekana kutojali kero hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mkazi kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Melliyo Mollel alisema kuwa tatizo la ukosefu wa ofisi ya kijiji limekuwa likiwapa shida sana hasa katika kupata huduma za kiofisi kama barua za mdhamana, mihuri na sahihi ya viongozi wao hali ambayo huwalazimu kuwafuata viongozi hao majumbani mwao.

Pia alisema kuwa mbali na mafaili ya serikali kutoruhusiwa kuifadhiwa majumbani mwa watu, hali hiyo imekuwa tofauti kwao, kwani mafaili ya kijiji huifadhiwa nyumbani kwa mwenyekiti au mtandaji wa kijiji.

Mwananchi huyo alilalamika kwamba kutokana na hali hiyo, mbali na uwezekano wa kuvujisha siri za kiofisi na serikali kwa ujumla, pia mafaili hayo yanakuwa hayahifadhiwi ipasavyo na kusababisha yachakae mapema.

Mwananchi mwingine alisema kuwa mbali na matatizo hayo pia baadhi ya wananchi hukosa huduma za kiofisi au serikali kwa ujumla kutokana na kufahamu nyumbani kwa viongozi hao.

Aidha hata wale wanaopafahamu  nyumbani kwa viongozi hao wakati mwingine  hushindwa kwenda  kupata huduma stahiki kwa kuogopa kuvujisha siri zao binafsi kwa wanafamilia wa viongozi  hao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Kipok bwana Lekinderaki Maneno alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la ukosefu wa ofisi ya kijiji  lakini alikanusha madai kwamba uongozi wa kijiji haujali kulitatua.

Alisema kuwa mbali na uwezo mdogo walionao wananchi katika kuchangia ujenzi huo kwa mwingine suala hilo limekuzwa na mgogoro wa kisiasa unaofukuta kijijini hapo.

Akifafanua mgogoro huo alisema kuwa alipochaguliwa na CCM mwaka 2010 kugombea u-wenyekiti wa kijiji hicho aliyekuwa mpinzani wake ndani ya chama hicho hakuridhika na kuamua kuwafarakanisha wananchi wake kwa kuchochea mgogoro wa chini kwa chini pamoja na kuendesha kampeni za kutomtambua.

Aliongeza kuwa mbali na hilo, uwezo wa wanachi kuchangia ujenzi huo ni mdogo kutokana na kutakiwa kuchangia mradi mwingine wa ujenzi wa shule ya secondari ya Kipok unaoendelea kijijini hapo.

Pia aliongeza kuwa mbali na kuchangia ujenzi wa sekondari hiyo, uwezo wao umeathirika zaidi kutokana na tatizo la uhaba wa chakula lililosababishwa na ukame wa muda mrefu.

Maneno alielezea matumaini yake kwamba, pindi ujenzi wa shule utakapokamilika na tatizo la njaa kwisha, wananchi watakuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kuchangia ujenzi wa ofisi hiyo ya kijiji ambapo wananchi wake watapata huduma nzuri za kiserikali kupitia ofisi yao ya kijiji.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post