Mwendesha
mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda
(ICTR) ameiomba mahakama hiyo iwatie hatiani kwa tuhuma nyingine
walizoachiwa huru wafungwa wawili, akiwemo Waziri wa zamani wa Vijana wa
Rwanda, Callixte Nzabonimana na afisa wa zamani wa jeshi la nchi hiyo,
Ildephonse Nizeyimana.
Katika
taarifa fupi ya rufaa dhidi kesi ya Nzabonimana, mwendesha mashitaka
anaiomba Mahakama ya Rufaa kuachana na uamuzi uliotolewa na mahakama ya
awali kuhusu matukio ya uhalifu yaliyofanywa Aprili 15 na 17, 1994
katika wilaya za Nyabikenke na Rutobwe katika mkoa wa Gitarama, katikati
ya Rwanda.
Mei
31, 2012, mahakama ya awali ilimtia hatiani Nzabonimana kwa mauaji ya
kimbari,kula njama za kufanya mauaji hayo,uchochezi na kuteketeza kizazi
katika matukio mengine na kumhukumu kifungo cha maisha jela, lakini
aliachiwa huru kwa uhalifu uliofanyika katika maeneo hayo mawili
yanayotajwa na mwendesha mashitaka.
Kwa
mujibu wa mwendesha mashitaka katika rufaa yake ya Septemba 12, 2012,
anadai kwamba majaji wa mahakama ya awali wamekosea kisheria kwa kumwona
Nzabonimana kuwa alichochea tu mauaji yaliyofanyika katika ofisi za
wilaya ya Nyabikenke Aprili 15, 1994, badala ya kumtia hatiani kwa
kushiriki au kuamuru kufanyika kwa mauaji hayo.
Mwendesha
mashitaka anadai kwamba majaji wangemtia hatiani Nzabonimana pia kwa
kosa la kusaidia na kuunga mkono mauaji dhidi ya Watutsi katika wilaya
ya Rutobwe Aprili 17, 1994, kwa kusababisha kuachiwa huru watuhumiwa wa
mauaji waliotiwa kizuizini na maafisa wa serikali za mitaa kutokana na
vitendo vyao. Lakini majaji walimwachia huru kwa kosa hilo kwa maelezo
ya kukosa ushahidi wa kutosha.
Kwa
upande wa Kapteni Nizeyimana, mwendesha mashitaka anataka atiwe hatiani
pia kutokana na nafasi yake kama kiongozi wa askari waliodaiwa kutenda
uhalifu kwenye Chuo Kikuu cha Butare na Hospitali ya Butare, Kusini mwa
Rwanda.
Juni
19, 2012, majaji wa mahakama ya awali walimtia hatiani Nizeyimana kwa
mauaji ya kimbari,uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita katika
maeneo mbalimbali kwenye mkoa huo wa Butare na kuhukumiwa kifungo cha
maisha jela.