BREAKING NEWS

Wednesday, September 5, 2012

WANANCHI KAMBARAGE ARUSHA WAITAKA SERIKALI ITEKELEZE AGIZO LAKE



ZAIDI ya wakazi 300 wa eneo la Kambarage kata ya Themi ndani ya manispaa ya jiji la Arusha wameitaka serikali itekeleze agizo lake ililolitoa mnamo mwaka 1995 la kuwafutia hati miliki wafanyabiashara wawili wenye asili ya kiasia kwa kutafutiwa viwanja vingine kwa kuwa walivamia maeneo yao.

Wakazi hao wameitaka serikali itekeleze agizo hilo la kuvifuta viwanja nambari 12 na 13 lililotolewa na waziri mkuu mstaafu aliyejiuzulu ,Edward Lowasa  mwaka 1995 wakati alipotembelea eneo hilo kuwasikiliza akiwa waziri wa ardhi na makazi.

Wakizungumza katika mkutano uliotishwa na kamati waliyoiunda kushughulikia madai yao juzi ambao ulihudhuriwa na meya wa jiji la Arusha,Gaudence Lyimo  wakazi hao walilalamika kwamba wamestukia  njama za chini kwa chini zinazosukwa  kwa lengo la kutaka kupindisha agizo hilo ili waporwe ardhi yao.

Wakazi hao walisema kwamba tangu mwaka 1994 hadi sasa wamekuwa wakifuatilia utekelezaji wa agizo hilo  kupitia ngazi mbalimbali serikalini lakini hawajapatiwa ufumbuzi kitendo kinachowatia mashaka kwamba huenda kuna njama za wao kutaka kuporwa ardhi yao.

Ally Kaniki,ambaye ni miongoni mwa wakazi wa eneo hilo alisema kwamba wamejenga nyumba,maeneo ya ibada,mazao ya kudumu na makaburi ya muda mrefu lakini cha ajabu  wameshangaa wafanyabiashara wawili wenye asili ya kiasia kupatiwa eneo lao.

“Tumekuwa tukiishi hapa tangu enzi na enzi na kuna makaburi ya babu na bibi zetu hapa tangu mwaka 1994 tumehangaikia kupimiwa viwanja vyetu ili tupatiwe hatimili lakini cha ajabu tumeshangaa wamekuja kpatiwa wafanyabiashara wawili wenye asili ya kiasia”alisema Kaniki

Hatahivyo,mkazi mwingine ,Zaituni  Marunda alilalamika ya kwamba wanashangaa serikali kushindwa kutekeleza agizo alilolitoa  waziri mkuu mstaafu aliyejiuzulu,Edward Lowasa miaka ya tisini wakati akiwa waziri wa ardhi nyumba na makazi baada ya kuwatembelea na kisha kutoa maagizo ya kufuta hatimiliki za viwanja walivyopatiwa wafanyabiashara hao.

Alisema kwamba kama haitoshi suala hilo pia walilifishika kwa waliowahi kuwa wakuu wa mkoa wa Arusha,Daniel Ole Njoolay na Mohamed Babu ambapo walitoa maagizo ya kufutwa kwa hatimiliki hizo kwa  kupatiwa maeneo mengine lakini cha ajabu maagizo hayo hayajatekelezeka hadi sasa.

Huku wakionyesha taarifa,vielelezo  na mukhtasari mbalimbali wa vikao walivyokaa miaka ya nyuma na hivi karibuni wakazi hao walisema kwamba serikali imeshindwa kuwajali wazawa kwa kuwapatia haki yao na kuwakumbatia watu wenye ushawishi wa fedha.

“Tumekaa hapa miaka mingi tangu kukiwa mashamba ya mikonge na kahawa tangu tukiwa na watoto hadi sasa tumezaa na watoto tumezeeka tukiwa na wajukuu na vitukuu lakini leo serikali inawapatia wafanyabiashara hati miliki ya maeneo yetu hii ni ajabu”alisema kikongwe huyo mwenye umri wa zaidi ya miaka 60

Akijibu malalamiko hayo,meya wa jiji la Arusha,Lyimo alisema kwamba wao kama serikali wameyapokea malalamiko hayo kwa uzito mkubwa na watakutana na upande wa pili ambao ni wafanyabishara hao ili waweze kupata ukweli wa jambo hilo.

Hatahivyo,alisisitiza kwamba  katika kipindi chake cha uongozi amejidhatiti kutatua kero hiyo na kuwahaidi ya kwamba mnamo septemba 7 mwaka huu watatoa msimamo wa jambo hilo.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates