WATAKA SUALA LA SYRIA LIFIKISHWE ICC,KESI YA MUGESERA KUANZA NOVEMBA 19

Wachunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wiki hii wameliomba Baraza la Usalama la Umoja huo, kulipeleka suala la hali tete ya usalama nchini Syria mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).Mahakama Kuu mjini Kigali, imeahirishwa kwa muda wa miezi miwili kuanza kusikilizwa kwa kesi ya mwanasiasa mmoja wa nchi hiyo, Leon Mugesera anayeshitakiwa kwa mauaji ya kimbari.
UN/SYRIA
Wataka hali tete ya usalama Syria ipelekwe ICC: Wachunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Jumatatu waliliomba Baraza la Usalama la Umoja huo, kulipeleka suala la hali tete ya usalama nchini Syria mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC). Wachunguzi hao wanadai kwamba wamekusanya ushahidi ambao siyo wa kawaida na wa kutosha juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo.Wamefafanua kwamba wamepata orodha mpya ya siri ya Syria na vikosi vya kijeshi vinavyodaiwa kutenda uhalifu wa kivita ambayo watampatia Kamishina wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay.
RWANDA
Kesi ya Mugesera yacheleshwa hadi Novemba 19: Mahakama Kuu mjini Kigali, Jumatatu iliahirishwa kwa muda wa miezi miwili kuanza kusikilIzwa kwa kesi ya mwanasiasa mmoja wa nchi hiyo, Leon Mugesera anayeshitakikiwa kwa mauaji ya kimbari.Kesi hiyo sasa imepangwa kuanza kusikilizwa Novemba 19, 2012. Jaji Athanase Bakuzakundi aliruhusu kuahirishwa kwa kesi hiyo ili kumpatia mtuhumiwa huyo, muda zaidi wa kupitia jalada la kesi yake kutoka Canada lenye kurasa 40,000. 
WIKI IJAYO
ICC
Kesi ya Bemba kuendelea kuunguruma Jumatatu: Kesi ya utetezi inayomkabili kiongozi wa zamani wa kundi la waasi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (MLC), Jean Pierre Bemba inatarajiwa kuendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo, mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).Bemba anakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya
binadamu na uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa kati ya mwaka 2002 na 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.  
RWANDA  
Mahakama kuamua rufaa ya Uwinkindi: Jumatatu ijayo Mahakama Kuu mjini Kigali, itatoa uamuzi wake juu ya Mchungaji Jean Uwinkindi kupinga uamuzi wa mahakama ya awali ya kukataa kumwachia kwa dhamana. 
Mugesera mahakamani tena Septemba 28:  Msomi mmoja wa Rwanda, Leon Mugesera atasimama tena mahakamani Septemba 28, kupata uamuzi wa mahakama juu ya suala la mwenendo wa kesi yake.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post