Mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR),ameiomba mahakama hiyo kutupilia mbali maombi ya Waziri wa zamani wa Habari wa Rwanda na mfungwa wa mauaji ya kimbari, Eliezer Niyitegeka, anayetaka kufanyika kwa uchunguzi dhidi ya madai ya mashahidi kutoa ushahidi wa uongo katika kesi yake.
‘’Niyitegeka hajatoa kitu chochote kipya cha kuonyesha kuwepo kwa ushahidi wa uongo. Juhudi zake za kujaribu kwa mara nyingine kupinga matokeo yaliyobainishwa dhidi yake hapo awali hazina budi kutupiliwa mbali,’’ anaeleza James Arguin, Mkuu wa Kitengo cha Rufaa na Ushauri wa Kisheria, katika ofisi ya Mwendesha Mashitaka anaeleza katika hati ya kujibu maombi ya mfungwa huyo Jumatatu.
Waziri huyo wa zamani ambaye hivi sasa anatumikia kifungo cha maisha jela nchini Mali, alitiwa hatiani na mahakama ya awali Mei 23, 2003 kwa tuhuma za mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu. Mahakama ya Rufaa nayo ilithibitisha hukumu na adhabu aliyopewa Julai 9, 2004.
Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa imeshayakataa maombi matano kutoka kwa mfungwa huyo yaliyotaka mahakama ifanye marejeo ya hukumu yake.
Katika maombi yake, Niyitegeka anataka Mahakama imwamuru Msajili wa Mahakama hiyo, imteue rafiki wa mahakama, kuchunguza ushahidi wa mashahidi wa mwendesha mashitaka hususan ni shahidi mwenye jina bandia la GGV, kwa lengo la kutaka hatimaye ashitakiwe kwa kutoa ushahidi wa uongo.
Kama ombi hilo la awali halitakubalika mfungwa huyo anaomba afikiriwe ombi lingine la kuondoa amri inayomlinda shahidi huyo kutotoa ushahidi wake hadharani kwa kutumia jina bandia ili asitambulike kwa sababu za kiusalama ili sasa atambulike hadharani na kisha ashitakiwe mbele ya mahakama nyingine.
Maombi ya Niyitegeka ya kuunda jopo la kusikiliza madai yake yalikubaliwa Septemba 7, 2012 na tayari yamepangiwa jopo la majaji watatu kuyasikiliza akiwemo Rais wa ICTR.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia