CHAMA cha waandishi wa habarI mkoani Arusha kimelaani kwa nguvu zetu zote wale wote waliohusika katika mauaji ya mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari ya mkoani Iringa na kusema kuwa hayo yote ambayo yamefanyika ,kwa vyovyote vile,yamefanyika kwa makusudi na dhamira ya kuminya uhuru wa habari nchini.
Akitoa tamko hilo mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Arusha Claud Gwandu alisema kuwa wampokea kwa masikitiko makubwa na kwa mshtuko mkubwa kuuawa kikatili kwa mwanahabari mwenzetu, Daudi Mwangosi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Iringa Press Club akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kuwa wanapenda kuchukua nafasi hii kulaani kwa nguvu zetu zote wale wote waliohusika katika mauaji hayo ambayo,kwa vyovyote vile,yamefanyika kwa makusudi na dhamira ya kuminya uhuru wa habari nchini.
Gwandu alibainisha kuwa wao kama wadau katika tasnia ya habari,tunaviomba vyombo vya dola kuchunguza na kutoa taarifa SAHIHI ya nini kilichotokea na nani alihusika katika mauaji ya mwenzetu ambayo yamemgusa kila mmoja ambaye yupo katika tasnia ya habari na hata watu wanaozunguka tasnia hiyo.
Alisema kuwa wao kama chama cha waandishi wa habari mkoa wa Arusha (APC) pamoja wanatoa salamu za pole kwa familia ya marehemu Daudi Mwangosi,wanachama wa Iringa Press Club na wanahabari wote nchini kwa kumpoteza mwenzetu na kusema kuwa wapo pamoja katika kipindi hiki kigumu.
Aidha walisema kuwa wanamkumbuka na watamkumbuka Daudi Mwangosi kwa tabia yake ya unyenyekevu na ushirikiano kwa wenzake na wadau wote wa tasnia ya habari hapa nchini .
Alisema kuwa wao kama klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Arusha wanatoa rambirambi kwa familia ya marehemu Mwangosi ya kiasi cha shilingi 100,000 na kubainisha kuwa wataendelea kushirikiana nao hadi mwisho na kusema huku akimalizia kwa kusema Mungu ailazemahala pema peponi roho ya marehemu daudi mwangosi.