Imetolewa leo tarehe 16 Julai 2014
Na Dismas Lyassa
Mgombea Urais wa TUCTA; Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
Salaam
Wapendwa ndugu zangu wana habari…Asalam Aleikum…Tumsifu Yesu Kristo… Bwana Yesu Asifiwe…!
Shukrani
Ndugu wanahabari
Nawapenda
kuwashukuru kwa ujio wenu. Nichukue fursa hii niwatambulishe walioko
mbele yenu ili kufahamiana. Nianze kwa kujitambulisha mimi mwenyewe,
naitwa Dismas Lyassa, ni mwandishi wa habari mwenzenu…nimekuwa katika
hii kazi kwa miaka 20 sasa na nimewahi kufanyia kazi katika magazeti
mbalimbali yakiwamo Alasiri, Financial Times, Leo ni Leo na tangu 2005
nimekuwa nikifanyia kazi katika gazeti la Mwananchi hadi sasa nikiwa
mhariri anayeshughulikia masuala ya biashara na uchumi. Pia toka mwaka
2012 nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa COTWU tawi la Mwananchi
Communications Limited, nafasi ambayo kisheria mtu anapaswa kudumu kwa
miaka mitano, lakini akitaka anaweza kugombea.
Utambulisho
Ndugu wanahabari
Wengine
niliombatana nao ni mke wangu Mchungaji Rightess Lyassa wa Kanisa la
Ufufuo na Uzima, Kawe -Dar es Salaam, Mussa Mwakalinga Katibu Mkuu wa
Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Usafirishaji (COTWU) kanda ya
Dar es Salaam, wakili wangu Jebra Kambole kutoka kampuni ya Uwakili ya
Law Guards ya Jijini Dar es Salaam, na meneja kampeni Khamis Tembo.
Ndugu wanahabari
Lengo
hasa la kuwaiteni mahali hapa ni kutoa taarifa kwenu kuwa ninagombea
Urais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania, uchaguzi ambao
unatarajiwa kufanyika Agosti 4-5, Dodoma.
Vipaumbele vyangu ni vyangu
Ndugu wanahabari
Nina malengo ya kuifufua na kuleta TUCTA yenye uhai na mabadiliko ya kweli kwa kufanya yafuatayo;
Ndugu wanahabari
1. Kupigania na kulinda haki za wafanyakazi;
Katika kipaumbele hili lengo hasa ni kuondoa matatizo sugu ya wafanyakazi yakiwamo-:
i. Kulipwa ujira/mishahara duni isiyoendana na uhalisia wa maisha.
ii. Ucheleweshaji wa upatikanaji wa ujira/mishahara
iii. Ucheleweshaji fedha za kujikimu kwa waajiriwa wapya/ kiwango kidogo cha fedha za kujikimu
iv. Uhaba au kutokuwepo kabisa makazi kwa wafanyakazi wapya
v. Rushwa
na kuajiri kwa misingi ya kujuana kwa mfano katika Halmashauri ya Siha,
wilaya ambayo imegawanywa kutoka Hai, kuna pori kubwa la West
Kilimanjaro mlimani kabisa, hakuna maendeleo…ni suala la kawaida kuona
watu wakiongea kilugha ofisini kama lugha ya Taifa
vi. Wakubwa yaani mabosi kujifanya Mungu kwa kuwaendesha wafanyakazi kwa kadri wanavyotaka wao, sivyo inavyosema sheria.
vii. Uwepo wa mpangilio usio sawa wa ujira/mishahara.
viii. Kutopewa posho au kupewa kidogo au kutopewa kwa wakati
ix. Fedha
za uhamisho na likizo; kwa mfano kuna walimu ambao wameanza kazi 2004
NIT Shule ya msingi Dar es Salaam wamelipwa fedha za likizo mara moja
mwaka 2012, mfano halisi ni mwalimu Ruth Natumwa, huyo ni kati ya walimu
hao. Matatizo ya walimu kimsingi ni janga la taifa, yapo Taifa zima,
kwa mfano katika shule ya Sekondari Kizota, Dodoma kuna walimu wengi
wana madai yao dhidi ya Serikali, waliajiriwa mwaka jana Machi, wakaanza
kupata mshahara mwenzi wa tisa…walilipwa mshahara wa mwezi wa tisa tu
na kuendelea, ile mingine wanaendelea kudai.
x. Mazingira
magumu ya kazi mijini na vijijini (tunapozungumzia mazingira magumu
inahusisha kutokuwepo vitendea kazi au kuwa vichache, miundo mbinu duni
nk).
xi. Waajiri kutochangia mifuko ya jamii
xii. Fedha
za makato ya wafanyakazi kupitia mifuko ya jamii zimekuwa zikikopeshwa
watu wengine wasio wanachama wakiwamo wanasiasa huku wafanyakazi wenyewe
wakiendelea kuwa na maisha duni
xiii. Kufanya kazi kama kibarua kwa miaka mingi jambo ambalo ni tofauti za sheria za kazi
xiv. Huduma
za kifedha kuwa mbali na maeneo ya kazi, hali inayosababisha
wafanyakazi kutumia fedha nyingi kufuatilia mishahara kwa vile ni mbali
na eneo wanalofanyia kazi.
xv. Kutokuwa na mfumo unaoeleweka wa upandishaji vyeo na ujira/malipo kwa wafanyakazi/vibarua
xvi. Waajiri hasa binafsi kufukuza wafanyakazi hovyo/no job security…kufanya kazi bila mikataba
xvii. Kupambana na tatizo la kodi kubwa kwa mishahara (PAYE)
xviii. Tatizo
la mabosi kutoa upendeleo wa wazi kwa baadhi ya wafanyazi kwa sababu
zisizo za kitaalamu; wakati mwingine ni kwa sababu ya ngono; kuwataka
kimapenzi wafanyakazi ili waendelee kuwepo kazini au kupandishwa
vyeo…tatizo hili linaonekana kuwa sugu, wanawake wengi maofisini hawako
huru sana, wamekuwa wakitakwa kimapenzi mno na mabosi wao, wengi
wanashindwa kujizuia, tunataka kuona kunakuwa na sheria kali dhidi ya
mabosi wa aina hii kama ilivyo katika nchi nyingine.
Ndugu wanahabari
Tatizo la ajira kuporwa na wageni
Ingawa
sheria/sera za ajira zinaeleza wazi kwamba hairuhusiwi wageni kuingia
nchini zaidi ya watano kwa kazi ziziso na ujuzi, baadhi ya makampuni
yamekuwa yakiingiza wageni kwa kazi ambazo Watanzania wengi wanaweza
kuzifanya.
Ndugu wanahabari
Nitahakikisha
wazawa wanapewa fursa ya kufanya kazi nchini; hii ni pamoja na kuomba
CV za wageni ili tuone kama ni kweli hakuna Watanzania wenye sifa za
kufanya hiyo kazi hiyo.
-: Kumekuwa na taarifa za uwepo wageni katika makampuni kadhaa
yakiwamo mahoteli, migodi, viwanda vya sarufi nk ambao baadhi wanalipwa
malipo makubwa tofauti na wazawa japo hawana elimu au ujuzi wa kuwazidi
wazawa. Nitakuwa na kamati maalumu ya kufuatilia waajiriwa wote Tanzania
hasa wageni ili kujua kama wanazo sifa za kufanya kazi au wanapora
nafasi za Watanzania.
Ndugu wanahabari
Nitapigania kuhakikisha tabia ya waajiri kulazimisha waajiriwa lazima wawe na uzoefu mkubwa inapungua au kukoma kabisa
Kigezo
cha kupata ajira kiwe ni uwezo wa mtu wakati huo baada ya kufanyiwa
usaili, siyo lazima awe na uzoefu wa miaka mitatu au mitano kama
ambavyo waajiri wengi wanalazimisha; tunahitaji kuona Serikali
inasimamia hili. Kama hali ni hii, wahitimu wanawezaje kupata ajira? Ni
suala ambalo nitakuwa mkali nalo mno kwa sababu lina athari kubwa kwa
jamii ya Tanzania, limekuwa ni sababu ya rushwa ikiwamo ya ngono…walioko
vyuoni wengi hawana uhakika wa ajira, kwa sababu ya tabia hii. Ni
lazima tubadilike, watu waajiriwe kulingana na uwezo wao wa kazi, siyo
uzoefu.
Ndugu wanahabari
Wanafunzi shule ya Msingi/Sekondari nk wapatiwe elimu ya kujiajiri.
Kwa
nafasi nitakayokuwanayo nitaishawishi Serikali iingize elimu ya
ufundi/utengenezaji bidhaa na ujasiriamali kama mojawapo ya masomo ya
ziada kama njia ya kupambana na tatizo la ajira ambalo linaonekana kukua
nchini. Kama ambavyo kumekuwa na masomo ya dini katika shule zenu, tuwe
pia na masomo ya ujasiriamali. Nitaangalia namna ya kuzishawishi
taasisi zingine za ndani na nje kuhakikisha hili linafanyika; lengo ni
kuhakikisha hata mhitimu wa msingi au sekondari nk awe ana uwezo wa
kufanya ujuzi anaotaka kama kujenga, kushona, kufuma, kufuga,
kutengeneza batiki, vikoi, sabuni, mishumaa nk.
Ndugu wanahabari
Nitaanzisha idara mbili mpya na kuboresha zilizoko;
i. Idara ya walemavu
Hii
itahusika kuangalia hali ya maisha ya wafanyakazi walemavu nchini
ikiwamo kuwasaidia kupata baiskeli na huduma zingine muhimu.Nitatumia
uzoefu wangu kwa kushirikiana na rafiki zangu wa nje kuhakikisha hili
linafanikiwa. Tutaangalia namna ya kushirikiana na mashirika mbalimbali
yakiwamo Free Wheelchair Foundationwww.wheelchairfoundation.org.
Ndugu wanahabari
Kutakuwa
ni mikakati mbalimbali kuhusu wafanyakazi walemavu na wale wanaopata
ulemavu wakiwa kazini, kwa mfano Mwenyekiti wa Wasioona mkoani Tanga
amekuwa ni mtu ambaye ameumia kazini, lakini aliishia kulipwa Sh150,000
na bandari ambako alikuwa anafanya kazi kama kibarua. Kitendo kitakuwa
na jukumu la kufuatilia kwa ukaribu hali za wafanyakazi walemavu,
kuangalia kama wanavyotoka vyuoni wanapewa ajira au wanaishia
kunyanyapaliwa? Utafiti unaonyesha kuna wanafunzi wengi wanaohitimu
masomo wakiwa na ulemavu, hata hivyo hawaonekani kwenye maofisi
wakifanya kazi. Wanakwenda wapi? Litakuwa ni jukumu la hicho kitengo.
Ndugu wanahabari,
Idara ya pili ni
Idara ya fursa/Career Development Department na Mafunzo
Nimetembea
katika nchi tofauti Duniani ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi,
Mauritius, India, Thailand, Sweden na Marekani…nimeona fursa kadhaa
ambazo zimenishawishi kuanzisha idara maalum ya kusaidia wafanyakazi
kufahamu fursa zinazoendelea Duniani na hapa nchini. Fursa hizo zitakuwa
zinapatikana katika tovuti za TUCTA na ofisi za vyama vya wafanyakazi
mikoani. Baadhi ya fursa ni namna gani mtu anaweza kusoma nje ya nchi
bila kulipa ada kwa kozi za muda mrefu na mfupi, fursa ya mashirika
ambayo yanatoa misaada kwenye sekta mbalimbali.
-Kwa mfano kuna mashirika kama www.nuffic.nl au
vyuo ambavyo mtu anaweza kusoma bure bila kulipa chembe ya ada
kama www.berea.edu ya Marekani na fursa nyingine nyingi. Nimegundua
Watanzania wengi hawanufaiki sana na fursa hizi. Ziko pia taasisi
nyingine zinatoa.
Ndugu wanahabari
Idara hii
itakuwa na majukumu ya kutoa elimu kwa wafanyakazi kuzifahamu sheria za
kazi, hali kadhalika itakuwa inawasiliana na waajiri ili zaidi ya barua
ya ajira au mkataba wanaompa mwajiriwa, ampe pia na chapisho letu
ambalo mwajiriwa anapaswa kupewa siku ya kuajiriwa kwake ili ajue kwa
uhakika sheria za kazi zinasemaje; haki ya mwajiriwa kwa mwajiri au ipi
na haki ya mwajiri kwa mwajiriwa ni ipi; tutashawishi hili liwe ni suala
la lazima. Tutakuwa na vituo maalum vya msaada wa kisheria mikoani kote
au kwenye kanda. Tutakuwa na vipindi kwenye televisheni angalau kila
mwezi mara kuelezea masuala ya sheria za kazi. Tutaitumia tovuti ya
TUCTA kuwa ya kisasa zaidi.
Ndugu wanahabari
Kulifufua gazeti la Mfanyakazi ndani ya siku 90 ili liwe sauti thabiti ya wafanyakazi
Haijalishi
kama TUCTA itakuwa na fedha au la, nitahakikisha ndani ya siku 126
litakuwa mitaani likiandika habari mbalimbali hasa likitumika kama sauti
ya wafanyakazi na yote ambayo yataonekana ni ya maana kwa ustawi wa
taifa. Nina uzoefu zaidi ya miaka 20 katika sekya ya habari kama
Mhariri, na hata sasa ni Mhariri wa Biashara gazeti la Mwananchi,
nitahakikisha tunatafuta fedha ndani na nje ya TUCTA ikiwamo kuwatumia
wafanyabiashara kwa kubadilishana msaada kwa matangazo kwa muda, ili
hatimaye liweze kuwa mitaani. Ni aibu kubwa kuona nchi ina wafanyakazi
wengi, lakini gazeti kama hili la wafanyakazi haliko mitaani.
Ndugu wanahabari
Kuimarisha uhusiano wa vyama vya ndani na vyama vya nje
Nitahakikisha
nafanya mawasiliano na mashirika mengine yakiwamo International Trade
Union Confederation, Secretary General Sharan Barrow na mashirika
mengine ili kuona namna gani vyama vya wafanyakazi vya nchini
vinanufaika na ushirikiano huo kwa kubadilishana uzoefu na kadhalika
mara kwa mara kadri inavyowezekana.
Ndugu wanahabari
Nitatutumia
uzoefu wangu wa shughuli za kuwasiliana na vyuo vya nje na uzoefu wangu
wa kufanya kazi katika mashirika mbalimbali ya nje kama muwakilishi wao
hapa nchini, na kutembea nchi mbalimbali, kuviunganisha vyama vya
ndani vya wafanyakazi, kuwa na ukaribu zaidi na vile vya nje, na pia
kujenga uwezekano wa viongozi nchini kwenda nje kupitia ushirikiano huo.
Ndugu wanahabari
Hili
linawezekana kwa njia mbili, kwanza kama washirika wetu kwa vile
tutakuwa tuna mawasiliano ya karibu na aina ya chama ambacho mtu
anatoka, kwa mfano kama COTWU, TTU, TALGWU, TUICO, TAMICO, TEWUTA,
DOWUTA, TPAWU, RAAWU, TUGHE, CHODAWU, TRAWU. Nahitaji kuona ofisi za
vyama vya wafanyakazi nchini zinakuwa za kuvutia kwa kuzipatia vitendea
kazi, kuna mashirika nayafahamu, tunaweza kuyatumia kuwasiliana nayo
yakatusaidia kama vile Computer Aid International la Uingereza ambalo
hutoa misaada ya computer za aina mbalimbali kwa nchi maskini kama
Tanzania (www.computeraid.org).
Nje ya hiyo nitakuwa na vikao na viongozi wa chama kimoja badala ya
kingine kuangalia namna gani tunaweza kuboresha shughuli za utendaji za
ndani na nje hasa kuimarisha rasilimali watu na vifaa. Lengo kubwa la
kuomba niwe Rais wa TUCTA ni kuangalia namna gani tunaweza kushirikiana
na wafanyakazi na viongozi wa vyama katika kuimarisha wafanyakazi, kwani
malalamiko ni mengi. Tutaendeleza mali za TUCTA zikiwamo Chuo cha Wafanyakazi Mbeya na maeneo mengine.
Ndugu wanahabari
NAMNA GANI HAYA YATAWEZEKANA?
Mkakati
wa kuondoa kero zote zilizoelezwa juu utafanikiwa kwa majadiliano yenye
ukomo (deadline) na Serikali/waajiri, au kufanya chochote ambacho katiba
inaruhusu. Sheria ziko wazi, nitahamasisha zifuatwe na zifahamike.
Shida kubwa ninayoiona kwa sasa, wafanyakazi wengi hawajui haki zao pia
msaada wa vyama katika kuwasaidia wafanyakazi ni mdogo.
Ndugu wanahabari
Hata
hivyo mkakati hasa ni kuangalia TUCTA kwa kushirikiana na vyama shiriki
vinafanya nini kuondoa changamoto ambazo sisi wenyewe tunaweza
kuziondoa. Uongozi siyo kulalamika, bali kuthubutu kuchukua hatua
zinazoweza kuondoa shida zilizoko. Tayari nimeanza kuwasiliana na vyama
mbalimbali vya wafanyakazi katika mataifa ya nje ili kuangalia namna
gani tunashirikiana kwa maana ya kubadilishana uzoefu nk.
Ndugu wanahabari
Ofisi
nyingi za vyama vya wafanyakazi zimechakaa, naangalia uwezekano wa
kushirikiana nao katika hili kwa njia ya kutafuta wafadhili wa nje au
kubuni miradi itakayosaidia kuondoa hali hiyo; nataka pia maisha ya
viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi kwa ujumla yabadilike
kwa kutumia jitihada hizo nilizozieleza juu, nafahamu vizuri namna ya
kusaka wafadhili, kwani ni shughuli ambayo nimekuwa nikifanya kwa muda
mrefu kupitia taasisi yangu ya Global Source Watch, niliyoianzisha toka
mwaka 2001 ambayo imekuwa ikifanya kazi ya kuwaunganisha watu na vyuo
zaidi ya 78 vya nje kama Marekani, Canada, Greece, India, Malaysia nk.
Ndugu wanahabari
Nafahamu
kuna vyama vina miradi ya maendeleo, vinawasaidiaje wanachama wao?
Nahitaji niwe Rais ili nishirikiane na vyama vya wafanyakazi na
wafanyakazi kwa ujumla kuleta tija kwa Watanzania. Tusiwe watu wa
kunyoosheana vidole…kila mtu awe chanzo cha mabadiliko anayotaka kuyaona
Tanzania! Naamini kila mtu akifanya kazi zake vizuri…Tanzania itakuwa
na maendeleo kwa kasi. Wafanyakazi wanahitaji mambo mengi zaidi ya
kuhamasishwa migomo, lakini kama tutaamua kugoma, tunapaswa kugoma kwa
kumaanisha, hatupaswi kuogopa kutekeleza yaliyo haki yetu.
Ndugu wanahabari
Kwa
nafasi nitakayokuwa nayo nitaanzisha semina, makongamano, mijadara
itakayokuwa ya wazi na kutoa elimu ya kutosha juu ya haki za wafanyakazi
na wajibu wa waajiri kwa wafanyakazi. Hii itasaidia kupunguza migogoro
na wafanyakazi watatambua haki zao.
Ndugu wanahabari
Tunatakiwa
kuwa sauti ya wafanyakazi hapa Tanzania, TUCTA imelala, tunataka
kuikimbiza mchakamchaka,, kuna mambo mengi yanatokea dhidi ya
wafanyakazi hapa nchini lakini TUCTA haitoi hata matamko au kutetea
wafanyakazi,
Ndugu wanahabari
Natambua changamoto za wafanyakazi, tunataka kuwa na
TUCTA Mpya
Nguvu Mpya
Uongozi Mpya
Sauti Mpya
Umoja Mpya
Maendeleo Mapya
Kwa pamoja tunaweza.
Mungu awabariki!
Dismas Lyassa
Mgombea nafasi ya Urais-TUCTA
simu 0754 49 89 72