Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ASP
Lwitiko Norman Kibanda, akizungumza na madereva wa pikipiki za kubeba
abiria ambao juzi waliandamana hadi kwenye kituo hicho wakipinga kutozwa
fedha sh22,000 na maofisa biashara wa wilaya hiyo, waliodai kuwa tozo
hizo ni amri ya Mamlaka ya Usafirishari wa vyombo vya usafiri wa majini
na nchi kavu (Sumatra).
Madereva wanaoendesha pikipiki 800 wa kubeba abiria,
maarufu kama bodaboda wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiaro Mkoani
Manyara, wameandamna hadi kituo cha polisi Mirerani, wakipinga kitendo cha
maofisa biashara wa wilaya hiyo kuwataka walipe sh22,000 za tozo la Mamlaka ya
usafirishaji wa vyombo vya majini na nchi kavu nchini (Sumatra).
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa kituo cha polisi
Mirerani, ASP Lwitiko Kibanda, waendesha bodaboda hao walidai kuwa wamechoshwa
kunyonywa na maofisa biashara hao kwani tozo hizo hutolewa eneo hilo peke yake
hivyo wao wanagoma kulipa kwani wanaonewa na hawapo yatari kulipa kiasi hicho.
Mmoja kati ya madereva hao Rashid Omary alisema maofisa
biashara hao waliwaeleza suala hilo siku moja na kesho yake wakaanza zoezi la
kukamata pikipiki zao ili hali hawakupatiwa elimu wala kushirikishwa kwenye
suala hilo, hivyo hawapotayari kulipa kiwango hivyo kwani wamechoka kunyonywa
kila mara.
“Tunashangazwa kuambiwa tutoe sh22,000 za Sumatra ili hali
maeneo mengine ya Arusha, Kilimanjaro au wilaya ya Simanjiro kule Landania,
Orkesumet na Naberera hawalipishwi, kama sheria ya kunyoa nywele watu wote
imepitishwa kwanini sisi tuwe na vipara wengine wawe na nywele, hatukubali
kulipa hizo fedha,” alisema Omary.
Naye, Geofrey John alisema wabunge walifuta tozo za pikipiki
za kubebea abiria hivyo wanashangazwa na maofisa biashara wa wilaya hiyo
kuwataka walipe fedha hizo, hivyo watagoma kutoa fedha hizo kwani hivi sasa
kila mmoja anatambua haki zake na hawatakubali kuburuzwa tena.
Kwa upande wake, Mkuu wa kituo cha
polisi Mirerani, ASP
Lwitiko Kibanda aliwaeleza waendesha bodaboda hao kuwa wanatakiwa
wakutane tena na maofisa biashara hao ili kuzungumzia suala hilo kwani
kodi ya Serikali ni lazima ilipwe.'
“Tatizo ni kutotolewa kwa elimu juu ya suala hili kwani
wengine waendesha bodaboda siyo mali zao ni
waajiriwa hivyo, tujipange upya kwa maofisa biashara na ninyi bodaboda
tukutane na viongozi wenu ili mueleze ipasavyo na mshirikishwe kutokana na
jambo hili,” alisema Kibanda.
Hata hivyo, Ofisa biashara wa wilaya ya Simanjiro, Peter
Sanga alisema wanatoza sh22,000 za Sumatra wilayani humo, kwa pikipiki
inayosafirisha abiria yenye magurudumu
mawili na pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) na texi kwa mujibu wa sheria
ya Bunge.
“Tozo hiyo ni halali
kulipwa na hudumu kwa muda wa mwaka mmoja na endapo mtu akilipia mwezi Mei au
Julai mwaka huu, atatakiwa kulipa tena mwakani mwezi Mei au Julai na siyo
vinginevyo, hivyo waendesha pikipiki za kubebea abiria ni lazima walipie
pikipiki hiyo,”alisema Sanga.
Alisema Bunge halikufuta tozo hizo, kwani waliziachia na pia
ada ya zimamoto kwenye pikipiki zinazolipiwa sh10,000, bima ambayo hutozwa
wastani wa sh50,000 na sh22,000 ya ada ya Sumatra na ombi la kukatiwa tozo hiyo,
hivyo pikipiki za kubebea abiria zinatakiwa kulipa fedha hizo za Serikali.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia