BUNGE wa Ubungo, John Mnyika ameiweka mtegoni Wizara ya
Maji, akiitaka iweke wazi kwa umma, ratiba ya ziara ya kikazi ya wizara hiyo
kujionea tatizo la maji katika jimbo hilo na maeneo mengine jijini Dar es
Salaam ili wananci waweze kuhudhuria na kushiriki kikamilifu.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge,
ikisainiwa na Katibu Msaidizi, Aziz Himbuka, Wizara ya Maji pia imetakiwa
kuweka wazi ripoti ya matokeo ya uchunguzi uliopaswa kufanyika ndani ya mwezi
mmoja kuanzia Mwezi Mei kubaini kama matatizo ya mara kwa mara ya Mtambo wa
maji wa Ruvu Juu yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au
makosa mengine ya kibinadamu.
Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo imesema kuwa ratiba
hiyo inapaswa kujulikana kwa umma kwa sababu mbali ya kuhusisha kutembelea
mitambo ya kusafirisha, kusukuma na kusambaza maji, itahusisha pia mikutano ya
wananchi, ambayo imeelezwa kuwa ni muhimu ikajulikana ratiba yake mapema ili wananchi
waweze kushiriki.
Katika taarifa hiyo Ofisi ya Myika imesema kuwa kufuatia
hatua ambazo mbunge huyo alichukua katika mkutano wa 15 wa Bunge uliomalizika
karibuni juu ya matatizo ya maji katika maeneo yanayohudumiwa na DAWASA na
DAWASCO hususan kutoka vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini, Wizara ya Maji
ilirekebisha baadhi ya kasoro na kuahidi kuongeza kasi zaidi ya kazi ya
kuongeza mgawo wa maji.
Taarifa ya Katibu wa Mnyika iliongeza kusema kuwa pamoja na
hatua hiyo kusaidia ongezeko la upatikanaji wa wa maji katika baadhi ya maeneo,
imesema kuwa bado yapo maeneo yanayohitaji hatua za ziada.
“Hivyo, Wizara ya Maji inapaswa kutoa taarifa kwa umma juu
ya ratiba ya ziara ya kikazi ya Waziri au Naibu Waziri wa Maji katika Jimbo la
Ubungo na maeneo mengine ya Jiji la Dar Es Salaam na Mkoa wa Pwani kuanzia wiki
hii kuendelea kusimamia kasoro zilizopo zirekebishwe.
“Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo inakumbusha umma kwamba
Naibu Waziri wa Maji Amos Makala aliahidi bungeni wakati akimjibu mbunge kwamba
ziara ya kikazi itaanza tarehe 14 Julai 2014.
“Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo inatambua kwamba Wizara
iliwasilisha mapendekezo ya awali ya ratiba ya ziara kwa mbunge akiwa bungeni
Dodoma na mbunge kupendekeza marekebisho ya ratiba kuongeza maeneo ambayo ni
muhimu kufikiwa kuongeza upatikanaji wa maji. Hata hivyo, mpaka leo tarehe 13
Julai 2014 Ofisi haijapokea ratiba ya mwisho toka Wizara ya Maji juu ya ziara
hiyo,” imesem tarifa hiyo kutoka Ofisi ya Mbunge wa Ubungo.
Kuhusu ripoti ya uchunguzi uliopaswa kufanyika ndani ya
mwezi mmoja (Mei), kubaini kama matatizo ya mara kwa mara ya Mtambo wa maji wa
Ruvu Juu yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa
mengine ya kibinadamu, Ofisi ya Mnyika imesema kuwa wizara inawajibika kutimiza
ahadi iliyotolewa bungeni wakati wa vikao vya bajeti hivi karibuni.
“Mwezi Juni 2014 Mbunge wa Ubungo, alitaka taarifa hiyo iwasilishwe
na Naibu Waziri wa Maji Amos Makala alijibu kwamba tayari Kamati hiyo
imeshamaliza kazi yake na kukabidhi ripoti hiyo kwa Wizara. Naibu Waziri
aliahidi kwamba ripoti hiyo ingetolewa hivyo ni muhimu kupitia ziara hiyo ya
kikazi ripoti hiyo ikatolewa kwa Mbunge na kwa wananchi,” imesema taarifa hiyo
ya Himbuka.
Akiweka msisitizo kuhusu ripoti hiyo kuwekwa wazi, Himbuka
alirejea kauli ya Serikali iliyotolewa bungeni hivi karibuni na Waziri wa Maji alipojibu
mwongozo ulioombwa na Mnyika, ambapo Prof. Jumanne Maghembe alikiri kwamba kwa
takribani siku 67 (kati ya tarehe 01.03.2014 na tarehe 06.05.2014) mtambo
ulizalisha maji chini ya kiwango na kufikia kati ya lita milioni 8.2 na lita
milioni 57.4 ikilinganishwa na lita milioni 82 kwa siku, ambazo ndio uwezo
halisi wa mtambo huo.
“Waziri Maghembe aliorodhesha matatizo ya mtambo wa Ruvu Juu
kuwa ni: Kuharibika kwa pampu mara kwa mara kunakosababishwa na uchakavu
unaosababishwa na umri kua mkubwa miaka (60), kukatika kwa Umeme mara kwa mara,
maji kuwa na tope jingi sana wakati wa mvua na mafuriko hali inayopunguza uwezo
wa pampu za kusukuma maji na husababisha kusagika kwa vifaa vya pampu na ugumu
wa upatikanaji wa vipuri halisi.
“Hata hivyo, Waziri Maghembe hakukiri wala kukanusha juu ya
madai ya kuwepo kwa udhaifu, uzembe, ufisadi na hujuma katika mitambo ya vyanzo
vya maji na mitandao ya mabomba ya maji,” alisema Himbuka kupitia taarifa hiyo.