Mkazi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara,
Japhary Matimbwa akichangia damu juzi kwenye kituo cha Afya Mirerani,
ambapo katika zoezi la kuchangia damu (kushoto) ni mtaalamu wa maabara
wa kituo hicho, Dr Fanuel Laizer.
JAMII ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara, imeaswa kujitokeza kuchangia damu ili kuondokana na tatizo la
ukosefu wa damu pindi inapohitajika kwani ajali za mara kwa mara hutokea eneo
hilo ikiwemo za wafanyakazi migodini na madereva wa vyombo vya moto.
Ombi hilo lilitolewa juzi baada ya jamii ya eneo hilo kutojitokeza
kwenye zoezi la kuchangia damu lililokuwa linaendeshwa kwenye kituo cha afya
Mirerani, ambapo kati ya zaidi ya watu wanaoishi kwenye eneo hilo ni watu
watatu waliojitokeza hivyo kupatikana lita tatu za damu pekee.
Mmoja kati ya watu waliojitokeza kuchangia damu kwenye kituo
hicho Japhary Matimbwa aliiasa jamii ibadilike na kuchangia damu kwa ajili ya kusaidia
wagonjwa pindi itakapohitajika kwani ndugu zao wanaweza wakapata tatizo la
kuongezewa damu kisha wakakosa na kuanza kuilaumu Serikali.
“Watu wameshindwa kujitokeza kuchangia damu sijui kwa sababu
gani, hatukuwaona wanasiasa wanaotuomba kura wakijitokeza wala taasisi za
Serikali kuja kujitokeza kuchangia damu inatakiwa tubadilike jamani, kuna leo
na kesho hapa duniani ipo siku tutatakiwa kuongezewa damu,” alisema Matimbwa.
Hata hivyo, mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani, Dk
Tasen Mbwambo alisema anadhani watu wengi wameshindwa kujitokeza kuchangia damu
kwa hofu ya kupimwa kama wana maambukizi ya virusi vya ukimwi kabla ya
kufanyika kwa zoezi hilo.
“Nahisi kupia VVU kumewakwaza watu, haiwezekani eneo lenye
watu zaidi ya 50,000 washindwe kujitokeza na kupatikana lita tatu pekee ila hii
ni changamoto kwao kwani ndugu zao wanaweza kupata tatizo la kuongezewa damu na
wakashindwa kuongezewa kutokana na ukosefu wa damu,” alisema Dk Mbwambo.
Naye, mtaalamu wa maabara wa kituo cha afya Mirerani, Dk
Fanuel Laizer aliyekuwa anaendesha zoezi hilo la kuwatoa watu damu, alishangazwa
na kutojitokeza watu wengi kwenye zoezi hilo kwani, walitoa matangazo kwenye
eneo lote la mji huo.
“Hivi sasa kituo chetu cha afya kimeboreshwa hivyo jamii itumia
fursa hivyo kwa kujitolea damu pindi nafasi kama hiyo itakapopatikana tena
kutokana na kuwa kitendo cha kuongezewa damu ni jambo la kawaida kwenye jamii
kwani itahitajika pindi ajali ikitokea au mgonjwa wa kuishiwa damu,” alisema Dk
Laizer.