Shule ya Sekondari Kisirimi iliyopo Wilayani Arumeru mkaoni Arusha
Mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kisirimi
wilayani Arumeru, Arusha, Emmanuel Kisongo amesema kufanya vizuri kwa
shule yake ni kuthibitisha shule za kata zinaweza kuwa bora nchini.
Kismiri (pichani) imeshika nafasi ya tatu kati ya
shule 10 bora nchini mwaka huu, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa
jana na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwalimu Kisongo
alisema mwaka huu wanafunzi wa shule yake wamefanya mtihani wa kidato
cha sita kwa mara ya saba na shule imefanikiwa kushika nafasi ya tatu
kitaifa kwa mara ya kwanza.
“Nimefurahi tumeingia kwenye shule 10 bora nchini
mara tano na safari hii tumeshika nafasi ya tatu. Ni wazi shule za kata
zinaweza, tofauti na fikra za wengi kuwa shule zipo chini kielimu,”
alisema.
Kisongo alisema mwaka jana walishika nafasi ya tano, kitaifa na mwaka juzi, walishika nafasi ya tatu kama mwaka huu.
“Siri ya mafanikio yetu ni ufundishaji mzuri na
ushirikiano mzuri wa walimu, wanafunzi na wazazi kwa lengo kubwa la
kuthibitisha kuwa walioanzisha shule ya kata hawakufanya makosa,”
alisema.
Alisema shule yake, ambayo ina jumla ya walimu 32
kati yao 12 wanafundisha kidato cha tano na sita, inafuata michepuo ya
sayansi na sanaa (art) na mwaka huu wanafunzi 52 walifanya mtihani.
“Tunajivunia mafanikio haya na malengo yetu
kuifanya shule hii kuwa bora nchini kwani ipo katika mazingira tulivu na
wanafunzi wa dini zote tunawajenga kuwa na hofu ya Mungu,” alisema.
Alisema kwa sasa wanafunzi wa shule hiyo,
wanajitambua na wanaheshimu masomo yao. Hawana muda wa migogoro na
shule, jambo ambalo linawapa muda mzuri kusoma.
Shule 10 bora 2013 zaporomoka
Ibrahim Yamola, Mwananchi
Dar es Salaam. Shule za sekondari zilizokuwa
kwenye orodha ya Kumi Bora ya matokeo ya kidato cha sita mwaka jana
zimeporomoka, huku shule isiyo maarufu ya Igowole, mkoa wa Iringa
ikichomoza kutoka nafasi ya nane hadi ya kwanza mwaka huu.
Mazingira ya Shule ya Sekondari ya Igowole iliyopo Wilaya ya
Mufindi ni ya kawaida sana, huku kwa muda mwingi wa msimu wanafunzi
wakipigwa na baridi kali katika eneo lilipo shule hiyo iliyozungukwa na
miti mikubwa.
Katika matokeo ya kidato cha sita mwaka jana,
Necta ilipanga shule 10 bora kulingana na idadi ya watahiniwa juu ya 30
na chini ya 30, lakini mwaka huu imeziweka kundi moja, kwa mujibu wa
kaimu katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles
E. Msonde.
Mwaka jana, kati ya shule 10 zilizokuwa na
watahiniwa zaidi ya 30, ni shule nne pekee zimeendelea kuwamo katika
kundi la shule 10 bora kitaifa mwaka huu licha ya mabadiliko hayo. Shule
hizo ni Marian Girls (Pwani) imekuwa ya sita mwaka huu wakati ilishika
nafasi ya kwanza 2013. Shule ya Feza Boys (Dar es Salaam) imeshika
nafasi ya pili mwaka huu wakati mwaka jana ilikuwa ya tatu.
Shule ya Sekondari ya Kibaha (Pwani) imeshika
nafasi ya tano wakati mwaka jana ilishika nafasi ya tisa. Kisimiri
(Arusha) imekuwa ya tatu ilhali mwaka jana ilikuwa ya tano kitaifa.
Shule zilizokuwa 10 bora mwaka jana lakini mwaka
huu hazimo katika nafasi hiyo ni; Mzumbe (Morogoro) iliyokuwa ya pili,
Ilboru Arusha (4) na Mtakatifu Mary Mazinde Juu ya Tanga (6).
Nyingine ni Tabora Girls (7) na Kifungilo Girls ya Tanga iliyoshika nafasi ya 10.
Katika kinyang’anyiro hicho, shule zilizochukua
nafasi ya shule zilizong’olewa katika kumi bora na nyingine kupanda
kutoka nafasi moja hadi nyingine ni Igowole (Iringa) iliyoshika nafasi
ya kwanza mwaka huu na mwaka jana ilikuwa ya nane. Iwawa (Njombe)
imeshika nafasi ya nne. Nyingine ni Nangwa (Manyara) nafasi ya saba,
Uwata (Mbeya-8), Kibondo (Kigoma-9) na Kawawa (Iringa) imefunga ukurasa
kwa kuwa ya kumi.
Shule zilizokuwa za mwisho mwaka jana katika kundi
la wanafunzi chini ya 30 na zaidi ya 30 mwaka huu licha ya mabadiliko
hayo ni shule tatu ziliyobaki na nyingine maarufu zikiingia kwa mara ya
kwanza.
Baadhi ya shule zilizoshika mkia ni Fidel
Castro (Pemba), Tambaza (Dar es Salaam), Muheza (Tanga), Mtwara
Technical (Mtwara) na Iyunga Technical ya Mbeya. Al-Falaah Muslim
(Unguja) na Osward Mang’ombe (Mara) zikiingia kwa mwaka wa pili
mfululizo