SAKATA la vijana wa The Dream Team ya Arumeru mkoani hapa
kutelekezwa nchini Brazil, limechukua sura nyingine baada ya Chama cha
Soka Mkoa (ARFA), kuruka kimanga kujihusisha na uratibu wa safari hiyo.
Hivi karibuni iliripotiwa vijana hao kutelekezwa nchini Brazil na
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Arumeru, Nyirembe Munassa Sabi, ambaye inaelezwa
ndiye aliyesimamia mpango huo, ikiwamo kuchangisha fedha kwa wadau
mbalimbali.
Mwakilishi wa Klabu Mkoa, Omary Walii, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati
ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema jijini hapa
jana kwamba hakuhusishwa na jambo lolote la safari ya vijana hao
kwenda Brazil, ingawa alisikia juu juu kutoka kwa wadau wa soka.
“Mimi nilisikia tu kwamba kuna vijana walioundwa na DC na wanajiita
The Dream Team na wanatarajia kwenda Brazil, lakini sikuhusishwa na
jambo lolote la kuwaratibu vijana hao, kwani nilipochunguza zaidi na
kugundua ni mkuu wa wilaya anahusika, nilipata hofu masuala haya ya
soka yanaweza kuingiliana na siasa, hivyo ndiyo nikajitoa kabisa,”
alisema na kuongeza:
“Na hata siku waliyoondoka sijui, bali nimekuja tu kusikia kuwa
vijana wameondoka na sijui hata idadi yake, hivyo kama anasema TFF
wanahusika labda niulize makao makuu Dar es Salaam juu ya hili, ila
uliza chama cha soka mkoa wanaweza kujua hili.”
Katibu Mkuu wa ARFA, Adam Brown, alisema kuwa mwanzo wa mchakato kuna
barua ilipelekwa ofisini kwake kutaarifu kuwa kuna vijana wanafanyiwa
mpango wa kwenda kushuhudia michuano wa Kombe la Dunia nchini Brazil.
“Baada ya kuletewa barua hiyo, Mkuu wa Wilaya alikuja kunitaka
nimsaidie kwenda ofisi za Uhamiaji kurahisisha vijana hao kupata
pasipoti, ambapo aliniletea majina zaidi ya 30.
“Mimi niliamua kufanya hilo, lakini unaambiwa tangu vijana hao
wafanikiwe kupata pasipoti sikujua tena kilichoendelea, wala kuhusishwa
tena kwa lolote na mimi sikufuatilia tena, bali nilipata taarifa tu juu
juu kutoka kwa watu kuwa vijana wameshaondoka kwenda Brazil, lakini
sijui ni wangapi hadi leo,” alisema Brown.
Alipotafutwa DC Nyirembe kuweka sawa tuhuma hizo, aligeuka mbogo huku
akitishia kuishitaki ARFA kwa kukana kuhusika hilo, sambamba na
mwandishi wa habari hizi.
“Wewe si ndio Bertha uliyeniandika vibaya kwa kuhongwa na watu
waliochukia vijana hawa kwenda Brazil, sasa usiniulize chochote na wala
sina jibu lolote… mimi nawafahamu sana waandishi wa habari, na mimi
namiliki chombo cha habari cha redio, hivyo hakuna nisichokijua na
nikitaka leo au kesho nakufungulia mashitaka wewe na hao viongozi wa
mpira, kwani nina mawakili wa kutosha,” alisema.
Aliongeza kuwa yeye ni mpenzi mkubwa wa soka na lengo lake la
kuanzisha timu hiyo na kuwapeleka Brazil kushuhudia Kombe la Dunia ni
kuwafanikisha vijana hao kuona na kujua mbinu mbalimbali za soka, ili
kuzitumia na kusakata soka vema na baadaye kufanikiwa kucheza Kombe la
Dunia mwaka 2025 na kuipeperusha bendera ya Tanzania.
“Mimi nina malengo makubwa sana na hii timu, ikiwemo kucheza Kombe
la Dunia mwaka 2025, lakini nashangaa watu wananipiga vita mimi badala
ya kupiga vita uzembe wao wafanikiwe hata kupata timu itakayowakilisha
Arusha Ligi Kuu,” alisema.
Alieleza kuwa vijana hao si kweli walitelekezwa, bali alikuwa nao
katika hoteli ya Mega Pool iliyoko Brazil hadi waliporejea nchini.
Awali vijana sita walifanikiwa kupata nafasi ya kwenda Brazil kwa
michango ya wahisani chini ya DC, lakini baadaye taarifa zilifika
nchini kuwa vijana hao wamekosa makazi kwa siku kadhaa na kulazimika
kulala uwanja wa ndege na stendi ya mabasi huku mkuu huyo wa wilaya
akikataa kuzungumzia chochote, kwa madai kuwa suala hilo liko mikononi
mwa TFF
Tags
matukio michezo