Wiki iliyopita tulichapisha habari ya kushtusha kwamba Watanzania milioni 14 hawajui kusoma wala kuandika. Ni habari ya kushtusha kwa sababu idadi hiyo ya wananchi mbumbumbu ni kubwa mno, kwa maana kwamba ni sawa na asilimia 33 ya Watanzania wote ambao ni milioni 44. Huu ni uthibitisho kwamba tumepoteza dira na mwelekeo kama taifa kwa kushindwa kutambua vipaumbele vya taifa, badala yake tukaelekeza rasilimali nyingi katika mambo yasiyokuwa na tija kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu.
Takwimu hizo za kushtusha zinatokana na ripoti
iliyotolewa mwishoni mwa mwaka uliopita na Shirika la Umoja wa Mataifa
la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), wakati wa maadhimisho ya Siku
ya Kujua Kusoma na Kuandika, huku Tanzania ikiwa haina taarifa rasmi
kuhusu idadi ya watu wasiojua kusoma wala kuandika.
Ripoti ya Unesco inasema kuwa, watu wasiojua
kusoma na kuandika duniani ni milioni 774 na kwamba mwaka 2002 idadi ya
mbumbumbu hapa nchini ilikuwa milioni 6.2, hali inayoonyesha kwamba
idadi ya watu hao inazidi kuongezeka siku hadi siku.
Tutakuwa hatukosei iwapo tutasema hali hiyo
inaipeleka nchi yetu kuzimu. Kama idadi ya mbumbumbu imepanda kutoka
asilimia 6.2 hadi asilimia 33 katika kipindi cha miaka 12 tu, tutegemee
kwamba miaka 15 ijayo zaidi ya nusu ya Watanzania watakuwa hawajui
kusoma wala kuandika iwapo Serikali itaendelea kupuuzia suala la elimu
kwa kisingizio cha ‘ufinyu wa bajeti’.
Nguvu na fedha nyingi vinaelekezwa katika masuala
ya kisiasa na mambo mengine ya yasiyo na tija, kwani huko ndiko kwenye
masilahi ya moja kwa moja kwa wanasiasa.
Jambo la kusikitisha ni kuwa, hata mafanikio
tuliyokuwa tumeyapata katika sekta ya elimu tumeshindwa kuyatunza,
kuyaendeleza na hata kuyaenzi.
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ilipoanzishwa kwa
Sheria Namba 12 ya mwaka 1975, Sura ya 139, ilitoa matokeo makubwa
katika muda mfupi, ambapo idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika
ilipanda kwa kasi ya ajabu, huku Tanzania ikisifika duniani kwa
kufanikisha elimu ya watu wazima.
Hata hivyo, kutokana na elimu hiyo kupuuzwa na
serikali zilizofuata, maelfu ya watu waliokuwa tayari wamejua kusoma na
kuandika walirudi kwenye umbumbumbu.
Tunachojaribu kusema hapa ni kwamba hatujawekeza
vya kutosha katika elimu, hasa Elimu ya Watu Wazima. Pamoja na taasisi
hiyo kuandaa na kutekeleza programu kwa ajili ya mafunzo ya walimu na
viongozi wa Elimu ya Watu Wazima, bado kuna upungufu mkubwa katika
kuendesha programu za waliomaliza elimu ya msingi kupitia Elimu Masafa
pamoja na programu za Elimu kwa Umma, Elimu ya Watu Wazima na Elimu
Isiyo Rasmi.
Kutokana na ufinyu wa bajeti programu hizo
haziendeshwi kwa ufanisi uliotarajiwa. Kwa mfano, umekuwapo uhaba wa
vitendea kazi na rasilimali watu, ikiwa ni pamoja na tovuti ya taasisi
hiyo kuendeshwa tu kwa lugha ya Kiingereza.
Matokeo yake ni taasisi hiyo kupoteza muda katika
kushughulikia mambo madogomadogo. Hivi sasa imeanza kuvifunga vituo
vinavyotoa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi ambavyo havijasajiliwa
chini yake. Utaratibu huo pengine umelenga kuiletea mapato, lakini
tunadhani ingebuni utaratibu mbadala wa kuviwezesha vituo hivyo kutoa
elimu bora pasipo kuviweka katika misukosuko isiyo ya lazima.