HAKIMU wa baraza la ardhi na nyumba mkoa wa Arusha,Maiko Makombe ametishia kuifuta kesi ya muda mrefu ya madai, iliyofunguliwa mwaka 2007 na mamlaka ya kahawa ACU mkoa wa Arusha dhidi ya raia wa Ugiriki anayeishi nchini Tanzania ,katika eneo la Usa river mkoani Arusha,Sotiris Sotirades (87) anayemiliki eneo lenye ukubwa wa hekari 7,ambapo ACU wanadai kuwa ni mali yao.
Akizungumza
mahakamani hapo, Hakimu Makombe alisema kuwa, kesi hiyo ya madai namba
209 ya mwaka 2007 ameirithi mwaka 2009,kutoka kwa hakimu mwingine
aliyekuwa anaisikiliza ambaye kwa sasa amehamia jijini Dar es salaam.
Makombe
alisema kuwa, kesi hiyo ambayo kwa sasa ipo katika hatua ya kusikilizwa
imeshindwa kuendelea kwa wakati kutokana na upande wa mashtaka kutoa
udhuru kila wanapofika mahakamani ama kutofika kabisa, hivyo endapo hawataleta mashaidi kesi itakapotajwa tena kesi hiyo itafutwa ili haki iweze kutendeka.
Alisema
kuwa,kesi hiyo imedumu kwa muda mrefu sasa na uchelewashaji huo umekuwa
hauwatendei haki upande wa mdaiwa kwani wao wamekuwa wakihudhuria
mahakamani hapo mara kwa mara na kesi kuendelea kupigwa tarehe,kitendo
ambacho kinawapa usumbufu usio na tija .
‘’Kwa
kweli kitendo hiki hakitendi haki hata kidogo mahakama zimekuwa
zikilaumiwa sana kwa kuchelewesha kesi za watu ,lakini kwa hali hii
utailaumu mahakama,na mimi leo nasisitiza awamu nyingine msipofika
naifuta kesi hii’’alisema Makombe.
Hakimu
Makombe alisema shauri hilo limekuwa la muda mrefu sana na kwamba tangu
ahamie jijini Arusha ameshasikiliza kesi zaidi ya 400 za watu
mbalimbali za aina hiyo na kumalizika kwa wakati na anashangazwa
kwanini kesi hiyo haimaliziki.
Hata
hivyo hakimu alimtaka Mwakilishi wa ACU kutoa maelezo kwanini wakili
wao hafiki mahakamani hapo mara kwa mara ndipo alijitetea kuwa wakili
wao Mahatane amekuwa akisumbuliwa na maradhi mbalimbali na kushindwa
kufika mahakamani hapo .
Kufuatia hatua hiyo , hakimu huyo aliwataka upande wa wadai kuleta mashaidi siku ya kesi hiyo oktoba 30 mwaka huu, saa tatu asubuhi na iwapo hawatafika siku hiyo , Hakimu Makombe ataifutilia mbali huku akiwataka kujipanga kufungua upya kesi hiyo iwapo hawataridhika.
Akizungumza
kwa masikitiko mahakamani hapo, mgiriki huyo alimweleza
Hakimu Makombe kuwa , upande wa madai wamekuwa wakifanya makusudi
kuahirisha kesi hiyo ili kuvuta muda mzee huyo aweze kufa na hatimaye
kesi yake ya msingi iweze kupotea.
''ndugu
hakimu mimi sasa ni mzee na ni mgonjwa hawa ACU wananiombea nife
wamekuwa wakifanya makusudi kutofika mahakamani ,mimi natumia gharama
kubwa kuendesha kesi hii na hivi sasa sina kipato chochote,lengo lao
nife nipoteze haki yangu maana mimi sina ndugu hap Tanzania naiomba
mahakama iliangalie hilo''alisema Sotirades
Alisema
kuwa,pamoja na kuwa amekuwa akihudhuria mahakamani hapo kila kesi
inapotajwa lakini cha ajabu hakuna lolote linaloendelea ,na kuwa kwa
sasa hivi anaumwa sana hivyo anahofia pindi atakapokufa haki yake ya msingi inaweza ikapotea.
Hivyo aliiomba
mahakama kuharakisha kesi hiyo ili iweze kumalizika kwa haraka kwani
imedumu kwa muda mrefu na amekuwa akitumia gharama kubwa ya uendeshaji wa kesi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwalipa mawakili na usafiri wa kwenda na kurudi kila kesi inapotajwa.