Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara
Christopher Ole Sendeka akisalimiana na baadhi ya wanachama wa kikundi cha
wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite cha Tupendane Family cha Mji mdogo wa
Mirerani ambapo jana aliongoza uzinduzi wa kikundi hicho na kupatikana sh6.2
milioni.
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani
Manyara,Christopher Ole Sendeka ameitaka Serikali kuwachukulia hatua kali watu
wanaoharibu amani kwa kuchomba moto nyumba za ibada ili kuinusuru nchi na
machafuko yanayotokea.
Ole Sendeka aliyasema hayo wakati
akizindua kikundi cha wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite cha Tupendane Family
kilichopo Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro ambapo zaidi ya sh6.2
milioni zilipatika katika uzinduzi huo.
Alisema Taifa linapita kwenye majaribu mazito
kwani kuna wahuni wachache ambao huenda wameichoka amani au wamelewa na amani
au wamekuwa makuwadi kwa kutumwa na watu wa nje ya nchi ili kuharibu amani ya
Tanzania.
Alisema kuwa Serikali inatakiwa kuonyesha
umadhubuti wa kukomesha vurugu hizo ambazo zinasababishwa na wahuni wachache
wenye dini na imani au wenye kuingia misikitini lakini wanachoma makanisa.
“Napenda kuitaka na kuihasa Serikali ingilie
kati kwenye hili kwa kuonyesha umadhubuti wa kukomesha hali hii kwani hatuwezi
kujinasibu kuwa tuna amani wakati wahuni wachache wanatia doa amani yetu, ”
alisema Ole Sendeka.
Alisema Serikali ikiendelea kuonyesha ustaarabu
kwenye hilo hali itabadilika na kusababisha machafuko ambayo yataleta vita
hivyo watumie uwezo wao katika kuhakikisha wanachukua hatua kali ili makanisa
yasiendelee kuchomwa moto.
“Muislamu anayejua maana ya uislamu hawezi
kuchoma mahali pa kuabudu na Mkristo anayejua ukristo hawezi kuchoma moto
sehemu ya kuabudia kwani haiwezekani muumini akachoma nyumba ya ibada,” alisema
Ole Sendeka.
Alisema kuna wahuni wachache wenye dini au
wanahudhuria kwenye sehemu ya ibada au wana majina ya kiislamu lakini siyo
waumini hasa wa dini ya kiislamu kwani mwislamu halisi hawezi kuchoma kanisa.
“Hata kwenye msahafu pameandikwa kabisa
waacheni wale na dini yao kwani mimi nina dini yangu na wao wana dini yao na
hii siyo kwenye hadithi za mtume ipo kwenye msahafu kabisa kila mtu na dini
yake,” alisema Ole Sendeka.
Alisema kuwa watanzania wanatakiwa
kuitunza,kuithamini na kuienzi amani iliyoasisiwa na viongozi wa mwanzo wa nchi
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.
“Serikali inapaswa ifike mahali isema basi kwa
kuchukua hatua ili kukomesha hali hiyo kwani tumechoka kuchezewa na pia haiwezi
kusema kuna amani wakati wahuni wachache wanaichezea amani hiyo” alisema Ole
Sendeka.
Pia,akizungumzia kikundi hicho alisema kina dhamira na
malengo mazuri ya maendeleo kwa kujiinua kiuchumi,zaidi ya kusaidia wagonjwa au
waliofiwa na kina sura ya kitaifa kutokana na kuwa na jamii ya makabila
mbalimbali hapa nchini.
"Kinachotakiwa
ni ninyi kujipanga muongeze mtaji na mimi nitaweza kukutana na rafiki
zangu kama kina Reginald Mengi nikawaomba waje watuunge mkono kwenye
kutunisha mfuko wetu," alisema Ole Sendeka.
Naye,Katibu wa kikundi cha Tupendane Family
Dickson Nakembetwa alisema kikundi chao kilianzishwa mwaka 2010 kikiwa na
wanachama 30 na sasa kina wanachama 74 na wana akiba ya sh3 milioni kwenye
benki ya NMB.
Nakembetwa alisema lengo la kuanzishwa kwa kikundi
hicho ni kusaidiana wakati wa matatizo na hadi hivi sasa wanakikundi saba
wameshasaidiwa matatizo mbalimbali waliyonayo
kwa kutumia sh1.1 milioni.
Alisema kiingilio cha kikundi ni sh20,000 ada
ya mwaka ni sh2,000 na hivi sasa wana mpango wa kutanua kikundi chao kwa
kuanzisha biashara na wanahitaji sh200 milioni kwa ajili ya kuanzisha miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia