Wiki
hii nitazungumzia suala la penzi kuchuja. Ipo hali ya kujisahau baada ya
wapenzi kuwa katika uhusiano kwa muda mrefu, haieleweki kama ni tabia ya mtu
ama ni uhalisia wa mambo kwasababu ukweli ulio wazi ni kwamba, mwanzo wa
uhusiano wengi hujitahidi kufanya mambo mengi ya kuwafurahisha wapenzi wetu
lakini kadiri siku zinavyosogea, penzi huanza kuchuja.
Kama huamini katika hili, rudisha nyuma
kumbukumbu zako kipindi kile ambacho ndio jamaa kaamua kukueleza wazi kwamba
anakupenda halafu angalia na sasa hivi, utabaini kwamba kuna tofauti kubwa
sana.
Huenda
mlikuwa na desturi ya kununuliana zawadi kama maua, kadi, chokoleti tabia hiyo
huenda ikawa imeyeyuka, hakuna kati yenu atakayekumbuka kitu hicho, ni wachache
sana ambao wanakwenda na wakati ndiyo huendelea kuzingatia hayo.
Kuna
wale ambao walikuwa na tabia ya kukutana kila mara kimapenzi ambapo kila mmoja
alitaka kumuonesha mwenzie jinsi alivyo
fundi wa 'kuyarudi' ndani ya uwanja wa mapenzi lakini yale manjonjo huadimika
kabisa.
Kawaida
yenu ilikuwa kubadilisha hoteli kwa ajili ya chakula cha jioni lakini tabia
hiyo hutoweka, labda kila wiki ilikuwa lazima muende 'out' mara tatu katika
kumbi tofauti za starehe na kufurahia mapenzi yenu, hali hiyo itabaki historia
tu.
Hivi
hujawahi kusikia mtu anasema "Enzi zile naanza uhusiano na mpenzi wangu
mapenzi yalikuwa moto moto, kila wiki ilikuwa lazima twende beach lakini, siku
hizi nikigusia tu kwenda huko ni ugomvi."
Maneno
kama haya huwa yananiuma sana hasa ninapogundua kwamba walio wengi wanakuwa na
nguvu ya soda pale wanapoingia katika uhusiano lakini baada ya muda mambo
hubadilika kabisa.
Sijajua
ni kwasababu gani lakini kwa utafiti mdogo ambao nilioufanya kwa baadhi ya
wanaume ni kwamba, wao wanapofanikiwa ‘kuona ndani tu’ hujenga kiburi fulani
kwa wasichana wao huku wakiamini kwamba, hata wawe tofauti vipi hawawezi
kuachwa!
Labda
nijaribu kushauri kitu katika hili kwamba, kama uko kwenye uhusiano wa
kimapenzi ama uko ndani ya ndoa, unatakiwa kufanya kila linalowezekana
kulifanya penzi lenu lisichuje.
Wewe
ndio unaweza kulifanya likaendelea kuonekana kuwa jipya kila siku ama kulifanya
likachuja mithili ya nguo inayochuja rangi iliyotumbukiza katika ndoo ya maji
ya moto.
Hatukatai
kwamba, kuna mabadiliko ya kimaslahi, pengine mtu na mpenzi wake wameketi na
kuona wanatumia pesa nyingi viwanja, kwahiyo wanaamua kupunguza au kuacha ili
kujenga maisha bora ya baadae, si unajua tena mnapokuwa na malengo ya kimaisha
zaidi?
Lakini
ukweli unabaki palepale kwamba, penzi la dhati haliwezi kuchuja hata siku moja.
Tujue wapo ambao wameishi miaka zaidi ya hamsini lakini penzi lao bado ni moto
licha ya kuwepo kwa mabadiliko madogo ambayo hayakwepeki kutokana na umri.
Yapo
mabadiliko mengi, lakini zaidi tujirekebishe, tukumbuke kwamba baadhi ya vitu
tulivyokuwa navyo huko nyuma ndivyo viliwavutia wepenzi wetu na kukubali kuwa
nasi kwa hiyo tukiacha tunakuwa tunawakatili.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia