NINI CHA KUFANYA UKIONA MWENZIWAKO AMEANZA KUBADILIKA

 NAZUNGUMZIA juu ya kupoteza msisimko wa mapenzi. Hili si tatizo dogo kama ambavyo baadhi ya watu wanaweza kufikiria. Utatuzi wake unahitaji sana utulivu wa akili, kukubali kubadilika na utayari wa kujifunza! Si fedha. Si mali. Si maneno. Uelewa na utayari pekee.

Wiki iliyopita wakati nafungua mada hii nilieleza maana ya tatizo hili kitaalamu, lakini sikuishia hapo, nikaenda mbele zaidi katika kueleza dalili za tatizo hilo. Utajuaje kama mpenzi wako ana tatizo hili? Nikaeleza vipengele viwili kati ya kumi nilivyowaandalia.

Leo nitaenda moja kwa moja kwenye vipengele hivyo nane vilivyosalia, halafu wiki ijayo nitawaletea tiba ya kutibu tatizo hilo. Kabla sijaanza napenda kuwashukuru sana wasomaji wangu wote ambao baada ya kutoka kwa makala haya na kuwagusa, waliweza kunipigia simu na kueleza hisia zao.
Ni wengi, siwezi kuwataja kwa majina, lakini wanajifahamu wenyewe. Sasa tuendelee na vipengele vilivyosalia kabla ya kutoa dawa. Haya marafiki, karibuni mnisome...

(iii) Mzito kukuambia anakupenda!
Ukiwa naye katika mahaba au mtoko, ukimwambia; “Nakupenda sana mpenzi wangu,” yeye anaona shida sana kukujibu anakupenda pia. Sababu kubwa hapa ni majeraha ya moyo.
Huwa anahisi kama atakuwa anakudanganya, maana moyo wake una bandeji kila kona! Hana uhakika na mapenzi yake, inawezekana akawa kweli anahisi kukupenda, lakini bado akawa hana imani sana na maneno yanayotoka kinywani mwako.

(iv) Ana wasiwasi sana...
Mara zote amekuwa na wasiwasi, hapendi mkae sehemu za uwazi, anafikiria juu ya kuachwa, huku utumwa mkubwa zaidi ukiwa ataificha wapi aibu yake siku na wewe ukimwambia utamwacha.
Haamini kama anaweza kuwa mpenzi wako siku zote, kwahiyo kuliko ‘ajichoreshe’ kwa watu kuwa yupo na wewe ni bora akae ‘nyuma nyuma’ kwa hofu ya kuchekwa na kubezwa siku akiachana na wewe maana hana uhakika wa kudumu sana na wewe.

(v) Hapendi mahaba
Anachukia michezo ya kimahaba, hapendi utani wa kimapenzi na kumwambia unampenda kila wakati. Ni mwoga pia wa ‘surprise’. Kwake mapenzi ni kama karata tatu, kwahiyo hawezi kujiachia sawasawa kwako.
Anaogopa kukufanyia ‘surprise’ maana anaweza kuja kwako na ghafla akakutana na mtu mwingine, kitu ambacho hataki kabisa kitokee. Hataki kufanya mambo mengi sana ya mshawasha wa mahaba maana hana uhakika sana kama kweli wewe ni wake.

(vi) Anapenda kulia

Ukimuudhi kidogo, machozi yanashuka machoni mwake. Unaweza kushangaa kosa dogo tu, mwenzio analia, sababu kubwa hapa ni kwamba, halizwi na kosa lako, analizwa na makosa ya wapenzi wake wa nyuma.

Anahisi kama anaonewa, ananyanyaswa na wakati mwingine anaweza kwenda mbali zaidi akihisi yeye ameumbwa kwa ajili ya kuteswa na mapenzi, jambo ambalo halina mantiki haswa. Kikubwa ni kupoteza msisimko.

(vii) Zawadi mara nyingi
Kwakuwa anajihami na hana uhakika na anachokifanya, anaweza kuwa mtu wa zawadi mara kwa mara. Unaweza kushangaa kwa wiki akakupa zawadi zaidi ya mara mbili. Haamini ni njia ipi ya kuboresha penzi, kwa kuogopa kuachwa, anahisi kukupa zawadi nyingi ni kukushika vyema.

Hana chaguo la moja kwa moja hasa. Hii ndiyo sababu anakuletea ‘mvua’ ya zawadi akijitahidi kuangalia ni ipi itakukuna zaidi. Mtego wake mkubwa ni kwamba, angalau anahisi utakuwa na kitu cha kukufanya umfikirie sana, wakati ukianza kuwaza kuachana naye. Hajiamini tu!

(viii) Anapenda kutulia
na wewe
Anapenda kukaa na wewe muda wote, akuangalie machoni na ikiwezekana usitoke kabisa kwenda nje. Kama anajua siku yako ya mapumziko, atahakikisha anawahi asubuhi ili kukufanyia kila kitu.

Anaogopa ukienda nje, ni rahisi kukutana na wajanja zaidi yake, ambao wanaweza kukuzuzua na kumsahau! Kila wakati atakutumia meseji na ukichelewa kumjibu atakulalamikia. Anahisi kuwa naye karibu sana kutamfanya yeye awe salama zaidi kwako.
Atahakikisha anaijua ratiba yako vizuri na hakika ataifuatilia kila hatua. Ukiona dalili hii ujue upo na mgonjwa!

(ix) Anatishia kukuacha
Kosa dogo tu, anaweza kukuambia: “Kama vipi tuachane, siwezi kuendelea na wewe tena.” Ukitulia na kupima kosa la kukuambia hivyo hulioni, kinachomsumbua hapo ni uwezo wa kupenda.
Ana hasira na muda wote anawaza kuachwa, sasa angalau anataka kuweka historia kwamba safari hii hajaachwa, AMEACHA! Kubwa zaidi hataki kuumia sana moyo wake, maana tayari ameshajihisi yeye ni wa kuonewa tu.

(x) Anapasua jipu...
Akishindwa yote kabisa, anaweza kuamua kukueleza ukweli wa mambo, kwamba anahisi hakupendi. Angalau hii ni nzuri zaidi, maana utakuwa umeujua ukweli na kazi yako hapo sasa itakuwa ni kuhakikisha unatibu tatizo lake.

Kumbuka kwamba si kwamba hakupendi bali HANA UWEZO WA KUPENDA, hana msisimko tena. Nyongo yake imeshatibuliwa. Lakini hii ni angalabu sana kutokea, wengi hawasemi, vitendo vyao vitaongea!
Yes marafiki, unajua jinsi ya kumtibu mpenzi wa aina hii?!...usipate tabu, zipo njia za kitaalamu kabisa, ambazo zinaweza kutatua tatizo hili moja kwa moja, wiki ijayo si ya kukosa kwa ajili ya kujua dawa yake, katika sehemu ya mwisho ya mada hii muhimu.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Gobal Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post