MAREKANI KUSAIDIA LEBANONI KWA UCHUNGUZI WA SHAMBULIZI LA BOMU LILILOMUUA MKUU WA UJASUSI NCHINI HUMO



Rais wa Lebanon Michel Suleiman na waziri mkuu Najib Mikati

Marekani imesema kuwa iko tayari kuchunguza shambulizi la bomu lililomuua mkuu wa ujasusi nchini Lebanon.
Kwa mujibu wa msemaji wa serikali, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton pamoja na waziri mkuu wa Lebanon Najib Mikati wamekubaliana kuhusu uchunguzi wa pamoja.

Awali Wissam al-Hassan na watu wengine saba waliuawa katika shambulio la bomu Ijumaa iliyopita.
Makabiliano yalizuka baada ya mazishi ya afisaa huyo siku ya Jumapili, huku waaandamanaji wakimtaka bwana Mikati kujiuzulu ambapo Mjini Beirut  Polisi waliwafyatulia risasi na gesi ya kutoa machozi waandamanaji hao walipokuwa wakijaribu kuvamia ofisi za serikali mjini humo.
 Pia Kuna ripoti kuwa huenda ghasia zaidi zikatokea Kusini na Magharibi mwa Beirut ambapo viongozi wa upinzani wamelaumu nchi jirani ya Syria kwa mashambulizi hayo.
Vurugu zilizozuka siku ya Jumapili kufuatia mauaji ya Afisaa mkuu wa Ujasusi nchini Lebanon Wissam al-Hassan

Maandamano tayari yamefanyika dhidi ya Syria, nchini Leabanon na nchi washirika wake huku kukiwa na hofu ya kusambaa kwa vurugu kupitia eneo la mpakani kati ya nchi hizo mbili.
Idadi kubwa ya maafisa katika serikali ya Lebanon wanaunga mkono serikali ya Syria.
Aidha serikali ya Syria imelaani shambulizi hilo ambalo pia liliwaua walinzi wa bwana Hassan pamoja na mwanamke mmoja aliyekuwa karibu na eneo la shambulizi.
Mnamo siku ya Jumapili, Bi Clinton alisisitiza kujitolea kwa Marekani kuhakikisha uthabiti wa Lebanon, uhuru wake na muhimu kabisa usalama
Clinton ,aligusia umuhimu wa viongozi wa kisiasa kushirikiana wakati huu ili kuhakikisha hali ya utulivu inaimarishwa na kwamba wale waliohusika watawajibishwa kwa kuchukuliwa hatua za kisheria. .

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post