Mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite,Kanunga
Paulo akipokea risala toka kwa Ngisere Sumleck ya wahitimu wa darasa la saba wa
shule ya msingi Lengasiti iliyopo kijiji cha Lengasiti,Kata ya Naisinyai
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara kwenye mahafali ya shule
WITO umetolewa kwa jamii ya wafugaji nchini kuendeleza
kikamilifu juhudi za kuwapatia elimu watoto wao ambao hivi sasa wamekuwa na
mwamko mkubwa wa kupenda elimu.
Hayo yameelezwa na wanafunzi wa darasa la saba
wa shule ya msingi Lengasiti iliyopo Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara kwenye risala iliyosomwa na Ngisere Sumleck kwenye mahafali ya
kuhitimu elimu hiyo.
Mhitimu wa darasa la saba wa shule ya msingi
Lengasiti,Kata ya Naisinyai Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara,Ngishumu
Partimbo akipokea zawadi ya mwanafunzi mwenye kipaji kutoka kwa mfanyabiashara
maarufu wa madini ya Tanzanite,Kanunga Paulo kwenye mahafali ya shule
Sumleck alisema elimu ndiyo ukombozi wa jamii
ya wafugaji kupiga hatua kubwa ya maendeleo hapa nchini hivyo wazazi wanapaswa
kutoa kipaumbele kwa watoto wao ambao hivi sasa wana mwamko mkubwa wa kusoma.
Alisema hivi sasa kila eneo la jamii ya
wafugaji hapa nchini watoto wamekuwa wanapenda kupata elimu hivyo wazazi na
walezi wanatakiwa kuwaunga mkono kuliko kuwafanya kuwa wachungi wa mifugo yao.
Alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1995
ikiwa shule ya nane kusajiliwa wilayani humo na kati ya watoto 37 walioanza
darasa la saba mwaka 2006 watoto 32 walihitimu baada ya watano kuondolewa kwa
kukariri darasa la nne.
Naye,mgeni rasmi wa mahafali hayo,Kanunga
Paulo ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite,alisema
anajitolea kumalizia ujenzi wa ofisi ya walimu inayogharimu sh1.3 milioni baada
ya wazazi kuchangia sh550,000.
Kanunga alisema kuwa baada ya yeye kujitolea kujenga
madarasa mawili kwa watoto wanaosoma shule ya awali hivi sasa amejitolea
kujenga ofisi hiyo ili kuwawezesha walimu wa shule hiyo kufanya kazi zao
ipasavyo.
“Kutokana na mwamko mkubwa wa elimu waliyonayo
watoto wetu na nawapa hongera kwa kupenda elimu hivyo nitajitahidi kadiri ya
uwezo wangu katika kuhakikisha kuwa wanapata mahitaji yao hapa shuleni,”
alisema Kanunga.
Kwa upande wake,Mwalimu mkuu wa shule hiyo,Fidelis
Mtenga alitoa wito kwa jamii ya wafugaji kung’ang’ania elimu kwani umasikini
unachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa elimu.
Mtenga alisema anaunga mkono falsafa ya Waziri
Mkuu mstaafu,Edward Lowassa ya elimu kwanza kwani kilimo kwanza kimeshindwa
kufanikiwa kutokana na jamii kutokuwa na elimu hiyo.
“Hatuna elimu ya kilimo kwanza hatuna kwani
hatuwezi kutekeleza jambo lolote bila elimu na elimu ndiyo mhimili wa maisha
kwani hata kulima mtu anapaswa aelimishwe kwanza ndipo atanufaika na kilimo,”
alisema Mtenga.