UMOJA wa
madereva wa magari makubwa waliopo soko kuu jijini Arusha wameishutumu kampuni
iliyopewa zabuni ya kukusanya ushuru jijini hapa kwamba imekuwa ikiwanyanyasa
kwa kuwatoza adhabu mbalimbali kinyemela sanjari na kukamata magari yao bila
sababu za msingi.
Umoja huo umeishushia lawama nzito kampuni hiyo ya Kilimanjaro Millenium Printers Ltd(KPML)
kwamba baadhi ya watumishi wake wamekuwa wakiwatoza adhabu zisizoelewaka na
kuutaka uongozi wa halmashauri ya jiji la Arusha kuingilia kati sakata hilo.
Akizungumza
kwa niaba ya madereva wengine ,mwenyekiti wa umoja huo,Lomayani Mollel alisema
kwamba baadhi ya watumishi wa kampuni hiyo wamekuwa wakiyakatia risiti za
maegesho magari yao bila taarifa yoyote kinyume na sheria.
Huku akionyesha kitabu cha sheria ndogo za ushuru wa kuegesha magari cha halmashauri ya jiji la Arusha ,Mollel alisema
kwamba wamekuwa wakitozwa adhabu mbalimbali kama kuegesha gari bila kulipia
ushuru kiasi cha sh,50,000,gharama za kupeleka gari kwenye yadi sh,30,000 na
gharama za kutunza gari hilo yadi sh,10,000 badala ya sh,50,000 iliyoanishwa kisheria.
Alitolea
mfano kwamba hivi karibuni kuna gari la mwenzao lilikamtwa majira ya saa 6;00
mchana na kuachiwa saa 2.00 mchana lakini lilitozwa ushuru kwa kuliegesha gari
hilo katika yadi ya kampuni hiyo kiasi cha sh,10,000 kinyume na sheria.
Hatahivyo,alibainisha
kwamba wao wanahitaji kikao cha pamoja baina ya uongozi wa kampuni hiyo na
halmashauri ya jiji la Arusha ili waweze kufafanuliwa sheria za ushuru kwa kuwa
wamekuwa wakitozwa ushuru huo kinyume na sheria.
Aliwatupia
lawama baadhi ya watumishi wa kampuni hiyo kwamba wamekuwa wakitumia lugha
chafu,ubabe na vitisho wakati wakitekeleza majukumu yao huku wakienda mbali
zaidi na kutaka wakala huyo atimuliwe endapo ameshindwa kutekeleza majukumu
yake kisheria.
Akijibu
shutumu hizo,mmoja wa wasimamizi wa kampuni hiyo,Eliufoo Munisi kwanza
alikanusha vikali madai hayo huku akiwataka madereva hao kuzipitia sheria ndogo
za ushuru kwa umakini badala ya kulalamika.
Naye,kaimu
mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Arusha,Omary Mkombole alikiri kupokea
malalamiko hayo huku akidai kwamba uongozi wake unafuatilia na kuyachunguza kwa
kina kabla ya kuchukua hatua zinazostahili.